Samia Yusuf Omar

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Samia Yusuf Omar au Samiyo Omar (25 Machi 1991 – Aprili 2012) alikuwa mwanariadha wa mbio fupi kutoka nchini Somalia . Alikuwa mmoja kati ya Wasomalia wawili walioshiriki kwenye Michezo ya Olimpiki 2008 huko Beijing, China.

Baada ya kutishiwa na wanamgambo wenye itikadi kali wa Al-Shabaab alikimbilia Ethiopia akaendelea hadi Lybia na wakati wa kuvuka bahari ya Mediteranea pamoja na wakimbizi wengine alikufa maji.

Familia na utoto[hariri | hariri chanzo]

Samia Yusuf Omar alizaliwa Somalia mnamo 25 Machi 1991,[1] kwa Omar Yusuf na Dahabo Ali akiwa wa kwanza kati ya watoto sita.[2] Mama yake aliwahi kuwa mwanariadha kwenye ngazi ya kitaifa.[3]

Wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe ya Somalia baba yake aliuawa na bomu lililolipuka sokoni alipofanya kazi wakati Samia alikuwa katika darasa la nane. Wakati ule aliacha shule akaangalia wadogo ilhali mama aliendelea kufanya biashara ndogondogo.[2] Mama alimpa moyo kufanya mazoezi ya mbio. [3] Alienda kwa mazoezi kwenye uwanja wa michezo penye njia ya mbio iliyokuwa na mashimo kutokana na milipuko ya mabomu. Kama hakuweza kuingia uwanjani alikimbia kwenye barabara za miji hata akishikwa mara kwa mara na wanamgambo na kurudishwa nyumbani kutokana an iamni zao za kidini eti mwanamke Mwislamu asishiriki katika riadha.[2]

Mashindano[hariri | hariri chanzo]

Mwezi wa Aprili mwaka 2008 alishiriki katika Ubingwa wa riadha wa Afrika huko Addis Ababa, Ethiopia alipopata nafasi ya mwisho.[2] Hata hivyo aliteuliwa na Kamati Olimpiki ya Somalia kushiriki katika mashindani ya mbio wa mita 200 kwenye Michezo ya Olimpiki ya 2008 huko Beijing, China. Wakati ule alisema ya kwamba hakutegemea kuteuliwa kwa sababi ya umri wake mdogo na kwa sababu familia yake alitoka katika jamii lisilo la Kisomali.[3]

Alishiriki katika viatu na nguo zilizotolewa na timu ya Sudani kwa sababu mwenyewe au kamati ya Somalia walikosa pesa.[2] Alimaliza wa mwisho lakini kwa makofi ya watazamaji wote katika sekunde 32.16.[4] [5] Habari zake akiwa mwanamke wa pekee kutoka Somalia ziliripotiwa na magazeti na vituo vya runinga vingi duniani.[2]

Baada ya Olimpiki[hariri | hariri chanzo]

Kushiriki kwake kwenye Olimpiki haikuripotiwa sana katika Somalia iliyoendelea kuwa na hali ya vita tena bila programu zozote za runinga nchini. Aliporudi kundi la al-Shabaab lilipanua utawala wake juu ya sehemu kubwa za Mogadishu na baada ya kutishwa na wanamgambo wao alijaribu kuficha kuwa yeye ni mwanariadha. Mwaka 2009 alihamia pamoja na mama na wadogo zake katika kambi la wakimbizi ndani ya Somalia. Al-Shabaab ilikataa wanawake wote wasihudhurie au kutazama michezo tena.[2]

Mwaka 2011 Samia aliona hawezi kuendelea tena Somalia alikimbia Ethiopia bila famila yake. Hapo Addis Abeba aliruhusiwa kushiriki katika mazoezi ya timu ya Ethiopia. Aliona ya kwamba alihitaji mazoezi zaidi na kocha ya binafsi ili akubaliwe kwa Olimpiki za mwaka 2012. Hivyo aliamua kuelekea Ulaya kwa matumaini ya kumpata kocha pale.[2]

Dhidi ya ushauri wa marafiki na familia aliondoka katika Ethiopia akitumia pesa yake kulipa watu waliomfikisha hadi Lybia.[6] Huko alifungwa jela pamoja na wakimbizi wengine Waafrika kwa muda.[7]

Kifo[hariri | hariri chanzo]

Mwezi wa Aprili alifaulu kupata nafasi kwenye mashua iliyopangwa kuwapeleka wakimbizi 70 Italia kwa siri. Mashua iliishiwa petroli ikaelea ovyo baharini kati ya Lybia na Sisilia. Manowari ya Kiitalia ilikaribia na wakati mabaharia walirusha kamba kwa mashua ndogo kulitokea msongamano mkubwa na watu kadhaa walisukumwa na kuanguka kwenye maji. Samia alikuwa mmojawao akazama akafa.[5]

Habari zake zimesimuliwa katika kitabu Non dirmi che hai paura ("Usiniambie kwamba unaogopa") cha mwandishi na mwanahabri Giuseppe Catozzella. Hakimiliki zimenunuliwa na shirika la Penguin Books kulikuwa na mipango ya kupiga filamu ya historia hii.[8] Mwaka 2015 mwandishi na mchoraji Mjerumani Reinhard Kleist alitoa kitabu Der Traum von Olympia – Die Geschichte von Samia Yusuf Omar ("An Olympic Dream – The Story of Samia Yusuf Omar") kilichotafsiriwa pia kwa Kiingereza na kutolewa mwaka 2016.[9]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. Samiya Yuusf Omar. International Association of Athletics Federations. Iliwekwa mnamo 15 October 2016.
  2. 2.0 2.1 2.2 2.3 2.4 2.5 2.6 2.7 "Somali inspiration battles against the odds", Al Jazeera, 20 August 2012. Retrieved on 15 October 2016. 
  3. 3.0 3.1 3.2 "Against the Odds: Samiya Yuusf Omar", BBC News, 21 July 2008. Retrieved on 15 October 2016. 
  4. 200 Metres – W. International Association of Athletics Federations. Jalada kutoka ya awali juu ya 21 August 2008. Iliwekwa mnamo 2008-08-21.
  5. 5.0 5.1 "The story of Samia Omar, the Olympic runner who drowned in the Med", The Guardian, 3 August 2016. Retrieved on 15 October 2016. 
  6. "Grieving for Somali Olympian Samia Omar", Al-Jazeera, 27 August 2012. Retrieved on 15 October 2016. 
  7. A Rosebud Exclusive: Samia Yusuf Omar’s Italian dream. An interview with Teresa Krug of Al Jazeera. Rosebud. Iliwekwa mnamo 15 October 2016.
  8. "“Non dirmi che hai paura”, la storia di Samia Yusuf Omar raccontata in un libro", il Bo, 19 March 2014. Retrieved on 15 October 2016. Archived from the original on 2017-04-09. 
  9. "An Olympic Dream: The Story of Samia Yusuf Omar", Publisher's Weekly. Retrieved on 15 October 2016. 

Viungo vya Nje[hariri | hariri chanzo]