Nenda kwa yaliyomo

Nini Chanzo (wimbo)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
"Nini Chanzo"
"Nini Chanzo" kava
Wimbo wa Juma Nature

kutoka katika albamu ya Nini Chanzo

Umetolewa 2001
Umerekodiwa 2001
Aina ya wimbo Hip hop
Urefu 4:09
Studio Bongo Records
Mtunzi Juma Nature
Mtayarishaji P. Funk
Nini Chanzo orodha ya nyimbo
  1. "Kighettoghetto"
  2. "Sonia"
  3. "Wimbi la Njaa" (remix 2001)
  4. "Jinsi Kijana"
  5. "Tumepigika"
  6. "Nini Chanzo"
  7. "Juu kwa Juu"
  8. "Hili Game"
  9. "Jinsi Kijana" (remix)
  10. "Haya We"
  11. Wimbi la Njaa (orijino 2000)

"Nini Chanzo" ni jina la wimbo wa sita kati ya nyimbo 11 zinazopatikana kutoka kwenye tepu ya kwanza ya albamu ya Nini Chanzo na wa kwanza kwa upande B kutoka kwa msanii wa muziki wa hip hop kutoka nchini Tanzania, Juma Nature. Wimbo umetayarishwa na P. Funk ndani ya Bongo Records. Wimbo huu ndio pekee kutoka katika albamu ambao umejihusisha na masuala mbalimbali ya kisiasa ya Tanzania na nchi nyingine za Afrika. Nature anajaribu kuelezea hali halisi ya siasa ya Afrika na hila zake. Jinsi wanasiasa wanavyoweza kuingiza watu mkenge kwa manufaa, huku wakifahamu fika atakayeteseka ni mwananchi wa kawaida wakati huo yeye yupo uhamishoni anakula nchi.

Ubeti wa kwanza

[hariri | hariri chanzo]

Kwa siasa ya Tanzania, ambayo tangu imeanza mabadiliko yake ni machache sana. Hasa ukizingatia awali ilikuwa siasa ya vyama vingi, lakini miaka ya 1960 kumetokea mabadiliko mengi kwenye uwanja wa siasa hasa kwa kufuatia mkanganyiko na mvurugano wa kiongozi wa juu na wale wa chini ambao waliamini wamepigania uhuru na kuanzisha vyama vyao vya kupambana katika chaguzi mbalimbali. Ili kuondoa fujo za kisiasa kwa wakati ule wa miaka ya 1960, ilikuwa kuna ulazima wa kusitisha vyama vingi kwa muda hasa kwa kufuatia uchanga wa nchi na malumbano tena, kwa busara, babu akaona ngoja kwanza. Sasa mwenyekiti wa chama ndiye Rais wa nchi, kama ilivyo sasa japo tangu 1992 siasa imekuwa ya vyama vingi na kumetokea mabadiliko mengi kwenye uwanja huo lakini si urais, ambapo mwenyekiti ndiye rais. Mstari wa kwanza tu anaanza:
"Rais sio msaliti tumekuchagua kuwa mwenyekiti, Kwenye suala la uongozi umetuonesha kwamba uko fiti"
Halafu anatoa angalizo: "Lazima ukumbuke kuwa ukitenda dhambi zitakutafuna"
"Kwa kuwa shukurani huna, ni vyema kufanya kazi kwa manufaa ya Afrika"
Maneno haya ya Juma Nature yanaakisi siasa kubwa ya Afrika. Wapo viongozi waliofanya kazi kwa manufaa ya Afrika na dunia au Afrika ikafurahi. Japo kinafiki, lakini wamefurahi. Mmoja wapo ni kiongozi wetu Baba wa Taifa hayati Julius Kambarage Nyerere. Baada ya Tanganyika kupata uhuru, hajakomea kwake. Kahakikisha majirani na baadhi ya Waafrika wenzake wanakuwa huru, ikiwa ni pamoja na Zambia, Afrika Kusini, Mozambique, Zimbabwe, Uganda na ushirika kiasi kwa chi jirani na Tanzania. Viongozi kama akina Ghadaffi ni miongoni mwa viongozi waliopendwa Afrika japo siasa za kuchafuana kutoka ughaibuni zilipelekea mambo kwenda kusi.

Nature anashangaa inakuwa mahusiano ya nchi yaingie dosari, eti kisa tu, kuna viongozi wawili wanatunishiana misuli mimi mwamba, wewe si lolote si chochote. Huku wananchi wanateseka. Wakati wao wanatunishiana, huku polisi wa nchi hizo mbili hasimu wanatesa raia wa nchi jirani. Mifano hii leo hii ipo, hata huko Afrika Kusini ilitokea mwaka 2015. Japo inasemekana kabla ya uongozi kuwa chini ya watu weusi (kuanzia 1994 kurudi nyuma), mambo ya kubagua wageni yalikuwa makubwa hasa Wazungu walikuwa hawataki wa wageni. Chakushangaza sasa unaambiwa baada ya nchi kuwa mikononi mwa Waafrika sasa, balaa la kutia mangumi wageni warudi kwao liliongozeka maradufu. Nature mambo haya kayaona kitambo lakini mwaka 2001 alirudia kama kukazia jinsi viongozi wa Waafrika walivyo wabinafsi. Anarudi Tanzania pekee na si Afrika kwa ujumla wake. Nature anashangaa bunge linakaa vikao kila siku wanajadili ongezeko la posho tu wakati huku Uswazi mambo sio mazuri kabisa. Tena mijitu mingine mikubwa mizima ina familia lakini wakiwa bungeni wanalala. Nature anafunguka zaidi na kushangazwa na muundo wa vyama vya siasa vinavyotaka kugombea kila mmoja kivyake, hawataki kuungana? Nature anaona siasa ya namna hiyo inakuwa ngumu kufikia malengo hata kama hawataki. Je, maneno yake na na tokeo la kuungana la vyama siasa kwa mwaka 2015 matunda yalionekana. Katika ubeti huu Nature anashangaa wanasiasa wanaoligalambua eti kisa wana uwezo wa kusafirisha familia nzima nje ya nchi, halafu huku aliowaachia sheshe wanatafuta pa kutokea. Familia zinatengana kwa yale uliyoyasababisha wewe chatne, tazama Kenya 2007 watu walivyokufa. Leo wao wanacheka, wenzao wanalia. Hakika kwa shujaa kwenda kilio na kwa moga kwenda kicheko!

Ubeti wa pili

[hariri | hariri chanzo]

Ubeti huu Nature karudi tena kwa Afrika nzima, anatetea wakimbizi wanaodhulumiwa misaada yao na viongozi au wasimamizi walafi. Watu wanachukulia shida za watu kama mtaji kwao. Shida zako ndiyo faida yangu kwako. Misaada inatolewa, watu wanalamba. Wananyanyapaliwa. Unakuta jitu lina miguvu bado linakula misaada ya walemavu. Nature anahamia Afrika Kusini jinsi watu wanavyotengana. Mtu akifanya kazi kwa Wazungu jamii yake ina mtenga. Visasi vya kisiasa vinavyopelekea chuki kubwa miongoni mwao. Nature anaona ajabu na hajui ni lini na wapi hizi tabia ilizaliwa, kuwafanya wenzao wafiwa au wakiwa. Nature anarudia anaenda mbali zaidio, unaishi maisha ya kuganga njaa fulu udananda na mbaya zaidi ukipelekwa jela ndio kabisa yaani mazingira mabovu katika jela nyingi. Utaomba ardhi ipasuke hayo mazingira yake. Halafu viongozi weusi wanajua kama wageni na weusi wenzao wanateswa lakini hakuna hatua inayochukuliwa. Hofu ya Juma Nature isije ikatokea malipizi ya visasi kama vya Maumau huko Kenya, eti kisa tu viongozi hawajali.

Ubeti wa tatu

[hariri | hariri chanzo]
Sampuli ya ubeti wa mwisho wa Nini Chanzo kama jinsi alivyokuwa anaelezea kwa kutaka watu waishi kwa amani na si fujo. Kupunguza ubinafsi ili kuepusha mabalaa yasiyo ya lazima.

Sehemu ya mwisho ndio anamaliza na kukata mzizi wa fitna katika vyombo ya habari. Nature anaumizwa na ufinywaji na upikaji wa taarifa za watu waliokufa aidha kwa kutokana na matatizo ya kivita au migogoro. Takwimu zinazotolewa daima zinakuwa za ovyo ili kudhibiti mchecheto kwa raia husika. Mkanganyiko mkubwa katika vyombo vya habari, redio zinasema 50, magazeti yatasema 60. Mbaya zaidi huwezi jua ni nani umauti utamfika kama si wewe basi jirani yako. Maiti zinazotupwa ovyo zimefungwafungwa (haya tumeyaona hivi karibuni maiti kuokotwa kwenye sandarusi). Nature anataka amani tu, anasihi athali za vita ni kubwa na bab-kubwa hakuna mfano. Bora uungwana watu wasali na kumuomba Mungu ili kupukana na dhima ya vita katika nchi. Nature analia na vita mbaya, wanaoteseka ni wengi na wengine hata chanzo cha vita hawakijui. Kuna bwege tu kaligalambua kimenuka, kasepa anaachia wenye meno watafune.

Viungo vya Nje

[hariri | hariri chanzo]


Kigezo:Juma Nature