Nash MC

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Nash MC
Nash MC (kushoto) na Hashim Rungwe—Agosti 2018, Berlin Ujerumani.
Taarifa za awali
Jina la kuzaliwaMutalemwa Jason Mushumbusi
Pia anajulikana kamaMaalim
Chizi
Zuzu
Nash Kenyatta Jicho Nyanya
Amezaliwa1 Januari 1985 (1985-01-01) (umri 39)
Dar es Salaam,
Tanzania
Kazi yakeMchanaji, mtunzi, mshairi
Miaka ya kazi1999-
Ameshirikiana naP the MC, Fanani wa HBC, Nillah Voice, Chaba, Maulo, Wakazi, Songa, One the Incredible, Zaiid, Stereo, Nikki Mbishi

"Mutalemwa Jason Theobard Mushumbusi" (anafahamika zaidi kwa jina la kisanii kama Nash MC; amezaliwa 1 Januari 1985) ni msanii wa muziki wa Hip Hop kutoka nchini Tanzania.

Ni msanii mwenye msimamo wa mrengo wa kushoto. Muundo wa mashairi yake ni kusimamia misingi ya utetezi wa wanyonge wa Tanzania. Tungo za kukemea maovu wanayotendewa wavuja jasho wa Tanzania. Alianza kurap mwishoni mwa miaka ya 1990 na umaarufu alipata 2001 baada ya kutoa "Kisa cha Mwanafunzi" aliomshirikisha Dully Sykes katika kiitikio na Dogo Lecha — kazi iliyotayarishwa kwa Miikka Mwamba wakati huo FM Studio Kinondoni.

Baadaye, kwenye mwaka 2002, wanakutana tena na wasanii wengine na kuanzisha kundi la Bronx Family maeneo ya majumba ya TAZARA bloku B. Ndani ya kundi kulikuwa na wasanii tisa. Ikiwa ni pamoja na Nash MC, Erasto, Willy G, Bernard, Posse, A-One, Michael Kimati (marehemu sasa), Philipo (kwa sasa hali yake kidogo si nzuri kiakili) na Dogo Lecha. Hicho ndicho kikosi kamili cha The Bronx. Kwa pamoja walifanya ngoma moja inaitwa "Mambo Yote" wakimshirikisha marehemu Mez B. Wimbo ulifanywa kwa Mikka Mwamba.

Nash ni kizazi cha wasanii waliowahi kuwa chini ya G-Lover na Far Lover waliokuwa wanaisimamia "New Jack Family" ya Kariakoo. Kupitia mlango huu, wasanii wengi waliweza kutoa nyimbo chungumzima zilizokuwa chini yao. Msanii maarufu wa kwanza kutoka chini ya New Jack Family ni Dully Sykes. Baadaye akina Zahran lakabu "Big Punisher wa Bongo", Abby Skills, Nash na wasanii wengine kibao. Baada ya kutoa kibao cha Kisa cha Mwanafunzi, Nash aliendelea kufanya kazi lakini hazijavuma sana. Akarudi shule hadi kwenye 2003/2004 aliamua kujisomea masuala ya hip-hip ili aweze kumudu vyema katika uwanja huo.

Alipitia mengi yanayohitajika ili kuwa mchanaji hasa. Alipata msaada kutoka kwa wasanii wakongwe wa hip hop ya Tanzania kama akina Lindu Lindulu, Zavara Mponjika, Saigon na wengine wengi tu. Kwenye mwaka wa 2009 alifanya mahojiano ya nguvu na Saigon wakati huo mtangazaji katika kipindi cha "HIP-HOP Base" cha EATV. Mahojiano haya Nash aliongea mengi ya msingi kuhusu uwanja wa hip-hop na alivyorudi katika kuchana alikuwa tofauti na zamani kabisa. Baadaye akaja kutoa "Nani Mkali Kwenye Game" chini ya mtayarishaji Kita ndani Ramo Records huko Magomeni, Dar es Salaam. Hiyo ilikuwa mwaka 2010. Mwaka 2011 anatoa kandamseto ya kwanza "Hazina Sura ya Kwanza" halafu akaendelea kutoa albamu kila mwaka uliofuata hadi 2014. Mwaka wa 2012 "Mzimu wa Shaaban Robert", mwaka wa 2013 "Chizi", mwaka wa 2014 Mchochezi. Albamu zote zimetazamia maisha halisi ya raia wa Tanzania na Afrika kwa ujumla jinsi wanavyopitia magumu yao ya kila siku.[1]

Kwa misimamo yake, ameonakana kukwazana sana na mamlaka nchini Tanzania hasa kwa kufuatia mashairi ya nyimbo zake baadhi zilipigwa marufuku zisipigwe kwenye TV na vyombo vya habari.

Maisha ya awali[hariri | hariri chanzo]

Nash amezaliwa na jina la "Mutalemwa Jason Theobard Mushumbusi." Jina lina maana ya “mpambanaji”, “mpiganaji”. Alizaliwa mnamo tarehe 1 Januari 1985 katika hospitali ya Hindu Mandal, jijini Dar es Salaam. Wakati huo anazaliwa mama yake na baba yake walikuwa wakiishi katika Mtaa wa Pazi, Temeke Dar es Salaam. Baadaye wakahamia mtaa wa Ruvuma karibu na shule ya Madenge, Temeke Kata 14. Maisha yake yote amekuwa akiishi Temeke, na mara kadhaa alisafiri kwenda kijijini Chigugu Masasi ambapo ni nyumbani kwao kwa asili anapotokea mama yake, Bi. Arafa Nashir Adnan. Nyumba yao ya mtaa wa Ruvuma inatazama na shule. Ambayo baadaye aliandikishwa katika shule hiyo hiyo mnamo mwaka wa 1989—shule ya Kata ya 14 CCM. Mutalemwa akiwa mdogo amekuwa mtu wa misukusuko na utundu kupita kiasi. Katika hangai zake za ukorofi, ikatoka akiwa shuleni amewahi kuvunja mkono mara mbili. Alisoma hadi 1992 mwishoni. Baadaye kwenye 1993 alianza dara la kwanza na kumaliza 1999. Mwaka wa 2000 anjiunga na shule ya Sekondari ya Benjamin Mkapa zamani City High School na kumaliza 2003.

Kazi ya muziki[hariri | hariri chanzo]

Nash MC akitumbuiza katika tamasha la "Rap Kwa Ajili ya Wakimbizi" huko jijini Berlin, Ujerumani — mnamo tarehe 25 Agosti, 2018.
Moja ya nguzo za mzuki wa hip-hop ni machata. Katika jengo hili liliopo maeneo ya Mabibo, Dar es Salaam—chini ya mlango kumechorwa jina la Nash MC.

Nash MC alianza kazi ya sanaa mnamo mwaka wa 1999. Hapa ndipo alipoanza hamasa ya kutaka kuwa MC. Vuguvugu hili liliendelea hadi kufikia kuwa huyu Nash wa leo. Miaka hii ya mwanzoni, alikuwa na washirika wenzake katika kazi. Washirika hao ni pamoja na Goodluck na Mlolwa. Hawa baadaye walisimama kuchana. Wakabaki katika kitengo cha kuandika mashairi. Kuandika mashairi kwa maana ya kwamba, Nash anachana, wao wanaandika. Ili kupunguza kazi ya mmoja. Yote hiyo lengo ilikuwa kutoa ngoma. Vilevile aliwachukulia kama marafiki zake wa karibu. Mwaka wa 2000, anaingia kidato cha kwanza pale City High School kabla ya kubadilishwa jina na kuitwa Benjamin William Mkapa High School. Akiwa anasoma hapa, aliweza kukutana na marafiki zake akina Pingu na Deso. Jina la zamani walijiita Gorilla Killer. Ili kutoa ngoma, Nash anaona amcheki "First Soldier" (Deso), anampa habari ya kwamba anataka atoe dude. Deso anatoa wazo kama vipi twenzetu kwa Henrico.

Wanaingia kwa Henrico wakiwa na mistari yao tayari kwa mashambulizi, wanafanikisha, licha ya kupata changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutimuliwa na Henrico kutokana na mazoezi hafifu. Zama hizi, vyombo ya kidijitali vilikuwa hakuna. Kulikuwa na ulazima kwanza wa kuushika wimbo wote ndipo uweze kuingia studio. Hali haikuwa ya mchezomchezo. Iko tofauti sana na sasa. Kazi hii ya kwanza iligharimu kiasi cha shilingi za Kitanzania 37,000.

Wimbo huu haujafanya vyema sana na ulibahatika kupigwa Classic FM tu. Alifanya nayo tamasha moja kisha ikapotea. Hili linathibtisha ng’ombe wa maskini hazai. CD hii alimpa mwanawe wa karibu kipindi hiko Kaboka Mchizi wa Kiwalani. Kifupi wimbo huu haijafanya maajabu sana. Mwaka wa 2001, alijichanga tena na kupata fedha ya kwenda kwa Miikka Mwamba kuandaa dude jipya. Safari hii karudi na Dogo Lecha katika Kisa cha Mwanafunzi. Yeye, Dully na Dogo Lecha wakaingia zao kwa Mikka na kurekodi wimbo wa “Kisa cha Mwanafunzi”. Wakati huu wote alikuwa chini ya ulezi wa New Jack Family watoto wa Kariakoo.

Baada ya ngoma kutoka zikaanza harakati ya kuipeleka ngoma maredioni. Kazi hiyo ilifanywa na DJ G Lover. Wa kwanza kupiga ngoma hii alikuwa DJ Venture saa saba mchana Clouds FM. Wakati ngoma inapigwa, alikuwa hajui. Mtaani kwao kulikuwa na wauza mkaa wakamhabarisha ya kwamba ngoma yako inapigwa. Zama hizi aliitwa “NASH Y”. Ikawa "oyaa Nash Y, ngoma yako inapigwa huku". Usiku kucha hajala alikuwa akifikiria kazi yake imepigwa redioni. Hii ndio safari sasa ya muziki ya Nash ilipoanza. Aliona bora aendelee maana uraibu wa muziki ulishaingia mwilini. Katika kazi ya muziki wa Nash, G Lover ana mchango mkubwa sana katika maisha yake.

Achilia hayo, pale New Jack Family kulikuwa na G Lover na Far Lover. Huyu Far Lover alikuwa anae anatoa sapoti kubwa sana kwa wasanii wa New Jack. Wasanii wengi wamesaidiwa na huyu, ila tu habari zake zipo kimya sio wengi wanaofahamu. Wimbo wa Kisa cha Mwanafunzi uliendelea kutoboa mbele zaidi, hali ambayo ilipelekea watu wengine wajue uwepo wake.

Akawa anapata maonyesho kibao. Umaarufu ulitamba sana, akawa anajiunga kundi la wasanii maarufu wenzie katika vijiwe vyao, hasa kwa kipindi kile ilikuwa Zero Brain, kule Posta Mpya. Wimbo ulipasua anga ukaja kuingizwa kwenye kanda yenye nyimbo mchanganyiko ya DJ John Dillinger wakati huo ilijulikana kama “Bongo Explosion Vol. 1”, ndani yake kulikuwa na ngoma kibao moja wapo ikiwa “Friday Night” ya Mr. Nice wakati huo, Mwanamkiwa wa K-Salu na ngoma nyengine za kina Bambo wakati huo.

Zama hizo ilikuwa kawaida sana kwa Ma-DJ wakubwa kutoa tepu zao zenye nyimbo mchanganyiko. Wimbo huo wa Kisa cha Mwanafunzi uliuzwa kwa kiasi cha 100,000. Kilikuwa kiasi kikubwa sana kwa wakati huo. Hata hivyo, kwa sababu mbalimbali utamaduni huo umekufa sasa. Miaka inaenda wakati unasogea na mwaka wa 2002, wanakutana tena na wasanii wengine na kuanzisha kundi la the Bronx Family maeneo ya fleti za TAZARA bloku B. Ndani ya kundi kulikuwa na wasanii tisa. Ikiwa ni pamoja na Nash MC, Erasto, Willy G, Bernard, Posse?, A-One, Michael Kimati (marehemu sasa), Philipo (sasa kidogo hali yake si nzuri kiakili) na Dogo Lecha. Hicho ndicho kikosi kamili cha The Bronx. Kwa pamoja walifanya ngoma moja inaitwa “Mambo Yote” wakimshirikisha marehemu Mez B. Wimbo ulifanywa kwa Mikka Mwamba. Pamoja na kufanya ngoma hii na the Bronx Family, bado alikuwa chini ya “New Jack Family”. Wakati huu hamasa ya muziki wa hip hop ilizidi kumjia juu.

Wakati unaenda, the Bronx inabaki, Nash anaulizana na mwanawe wa faida kitambo, Dogo Lecha katika suala zima la kukaza buti katika sanaa. Si ajabu sana katika makundi mengi ya muziki, Bronx Family wanagombana. Nash na Dogo Lecha wanabaki wana, wanachama wengine wakaenda kurekodi wimbo mwengine. Nash anaamua kutoka mazima kundini. Tangu akiwa humo kundini, yeye alikuwa ndiye mwandishi wa mashairi ya wasanii wengi tu.

Bosi wa kundi wakati huo alikuwa jamaa mmoja anayekwenda kwa jina la “Agu Fulani”. Huyu jamaa naye alikuwa anakaa maeneo yaleyale ya TAZARA. Baadaye kundi likarudi tena, wakarekodi kwa Effector, safari hii walimshirikisha Banana Zoro. Hata suala la kumtafuta Mez B katika ngoma ya kwanza ya Bronx Family ilikuwa juhudi binafsi kutoka kwa Nash. Wakati huo, Nash ndiye alikuwa msanii pekee mwenye jina. Wimbo huu wa mara ya pili haujafanya vizuri. Licha ya wakati wanarekodi zilikuwa zama za Effector.

Kipindi hiki chote bado aliendelea kujihusisha na New Jack Family. Baadaye Nash anaona sasa kuna ulazima wa kuomba wimbo wa Abby Skillz aliyofanya na msichana mmoja kipindi hiko alijulikana kwa jina la Mwamvua. Huyu binti alikuwa na uwezo wa juu sana katika suala zima la kuimba. Wakati huo wote walikuwa New Jack, hata Abby Skillz nae alikuwapo. Wimbo huu aliununua kwa kiasi cha 15,000 na kuingizia maneno, lakini haukufika popote pale. Kipindi hiki chote kilikuwa cha mwaka wa 2002.

Hakufanya jitihada zozote katika kuupaisha wimbo huu. Mwaka wa 2003, ndio mwaka aliomaliza elimu ya sekondari. Hapa alisimama kwa kiasi kikubwa na kujishughulisha na masuala ya muziki. Maisha yake yalikuwa yakudundadunda tu, mara hiki mara kile. Mwaka wa 2004 anajisogeza huko mjini Zanzibar. Huu sasa ulikuwa mwaliko kutoka kwa Dully Sykes. Dully aliambiwa aje na Nash Y katika onyesho atakayofanya huko Zanzibar.

Kutwa nzima alizungushwa katika Datsun kutwa nzima kwa wimbo wake uleule tu wa “Kisa cha Mwanafunzi”. Huko Zanzibar thamani yake ilikuwa juu sana. Lazima ieleweke kupitia wimbo wa “Kisa cha Mwanafunzi” ndipo Dully alipoanza kutumia jina la Prince Dully Sykes hadi hapo baadaye alipokuja kujiongezea neno la “Misifa” na kujiita “Mr. Misifa”.

Pamoja na safari hii, Nash aliambulia patupu alidhulumiwa na promota wake hukohuko Zanzibar. Ilimbidi aondoke usiku-usiku na boti ya bei rahisi wakati huo ilikuwa 4,000. Safari ya Zanzibar ilimuwia vigumu mno. Alipata tabu sana. Ilibidi aombe ufadhili kutoka kwa rafiki yake wa karibu wakati huo wa kuitwa Shaka Zulu ili aweze kumsitiri kwa usiku mmoja.

Kurudi upya na hip-hop ya Kiunaharakati[hariri | hariri chanzo]

Tangazo linaloonesha ratiba ya watakaotumbuiza katika tamasha la "Rap kwa Ajili ya Wakimbizi" lililofanyika mnamo tarehe 25-Agosti-2018 huko mjini Berlin, Ujerumani. Jina la Nash limo upande wa kushoto chini kabisa.

Mwaka wa 2005 aliamua kukaa chini na kuanza kuusoma muziki wa hip hop nje ndani ili aujue unatakaje na upoje. Alisoma vitabu mbalimbali vinavyoelezea na kuchambua muziki wa hip hop. Kilichomfanya atake kujua ni kwamba, alifahamu kiasi tu, labda baadhi ya albamu. Lakini miiko ya hip hop na misingi yake alikuwa haifahamu. Mwaka wa 2006 alikuwa ameanza kwiva sasa. Anakutana na kina mkubwa Zavara wa Kwanza Unit, mtayarishaji Lindu kwa pamoja walimweka chini mdogo wao na kumpa madini ya hatari katika kufanikisha suala zima la kuzama ndani ya maisha ya hip hop. Lindu amegonga ngoma kibao ikiwa ni pamoja na Kimbia ya Babuu wa Kitaa, Wakati Ndio Huu, Natubu ya Chidi Benz na ngoma nyengine kibao.

Watu hawa walimjenga Nash katika misingi imara ya hip hop aliyonayo leo. Walimpa miradi mbalimbali kwa ajili ya kuboresha uwezo wake. Walimshirikisha na wasanii mbalimbali wa nje na, hasa walimtaka atumie Kiswahili kama nguzo kuu. [2]Yale mambo ya zamani kutia maneno ya Kiingereza kwenye wimbo yasiwe sehemu ya ujio huu mpya. Uhusiano na wasanii hawa wakongwe ulipelekea kumpa taarifa juu ya tamasha la “WAPI” (Words And Pictures)” lililoandaliwa na British Council. Jukwaa hili lilikuwa chini ya usimamizi wa Zavara Mponjika. Jukwaa hili lilikuwa na faida kubwa kwa Nash. Aliweza kupata ufahamu mwingi sana.

Tamasha hili MC wa shughuli hii alikuwa Evans Bukuku, ndugu wa marehemu Roy Bukuku wa G Records. Akiwa hapa, anajenga ukaribu mkubwa sana na msanii mpya P the MC] kwa wakati huo, baada ya kuwa mbali kiasi na Dogo Lecha kwa sababu mbalimbali za kimaisha na kadhalika. Huyu P the MC aliletwa na jamaa mmoja wa kuitwa Eddy. Kwa lengo la kuungana na msanii mwengine ili wafanye kazi ote kama washirika.

Pamoja na P walifanya mengi ya kupendeza, walipanda wote kwenye majukwaa mbalimbali. Kipindi cha tamasha la wapi ilikuwa kati ya 2009/2010. Mwaka wa 2009 alifanya mahojiano na Saigon wa kipindi hiko alikuwa anaendesha show ya Hip Hop Base. Alifunguka mambo mengi sana yaliyongeza ujulikanaji wa uwepo wa Nash katika mazingira ya Watanzania. Aliielezea hip hop katika misingi yake na namna ya kuishi katika utamaduni wa hip hop.

Madini haya aliyotema kwa Saigon ilikuwa gumzo. Ikawa kama vile Nash katoa ngoma au albamu vile, kumbe ilikuwa mahojiano tu ya kawaida. Wakati anafanya mahojiano haya, pembeni alikuwa na marafiki zake wa karibu, wana wa faida, kina “Dullah the Black Death” na “D Theory”. Mahojiano haya yaliyofana, bahati mbaya hayapatikani popote pale tangu kufanywa kwakwe. Wakati unaenda, dawa imeingia baada ya kukutana na wakongwe hao, na mwaka wa 2010 akitumia muundo mpya wa kuchana anatoa ngoma inaitwa “Nani Mkali Kwenye Game” chini ya mtayarishaji Kita ndani Ramo Records huko Magomeni, Dar es Salaam. Wimbo huu ulipelekwa Clouds ukakataliwa kwa madai ya kwamba uchangaji mbovu. Ajabu iliyoje redio nyengine zote ulikuwa unapigwa. Wimbo huu ulileta sasa sura mpya ya Nash MC katika muziki.

Shukrani za dhati zimwendee DJ Jeff Jay aliyethubutu kuipiga ngoma hiyo kwa kadiri alivyoweza katika redio ya Kiss FM. Aliupigwa mara chungumzima bila hesabu kamili. Wimbo huu ilisafisha njia vizuri sana kwa kazi ya Nash kati ya 2009-2010. Mwaka wa 2010, anakutana na mtayarishaji Palla, mtayarishaji ambaye alikuja kutayarisha ngoma kibao za Nash MC. Wimbo wa kwanza kufanya na Nash ni rudio la “Homa Imenizidia” iliyotandikwa katika mahadhi ya kihip-hop.

Hii ni asili ya tangu enzi na enzi kwa muziki wa hip hop kuchukua sampuli ya nyimbo aidha za dance, pop, classic ballad na nyenginezo na kuzitumia katika muziki wa hip hop. Muungano huu wa Nash na Palla, unazua balaa kubwa katika tasnia. Wimbo ulipotoka ulileta sura mpya kwa wasikilizaji wa hip hop ya Tanzania. Nash anapata mahojiano rasmi ya kwanza na DJ Fetty wa Clouds FM. Mwaliko huo uliokuwa gumzo kituoni hapo kwa Nash kuongelea kwa kina dhima na nia ya hip hop katika jamii ya watu wa Tanzania kwa mapana yake.

DJ Fetty ilibidi anyamaze kimya akimwachia Nash aungurume katika kipindi. Hali hii ilikuja kuzua taharuki hadi kwa wakurugenzi wa usimamizi wa vipindi na utayarishaji ya kwamba, inakuwaje mgeni mwalikwa kaja kuhojiwa anakuwa ana hodhi kipindi? Huu umekuwa utaratibu wa kawaida sana kwa NASH MC kutoa maneno mazito na hoja za msingi akiwa amepewa fursa ajielezee au aelezee jambo fulani. Muda huu ilikuwa kati ya 2011-2012 ndio wimbo wa “Homa Imenizidia” umetoka. Wimbo huo ulimpeleka katika tamasha la Fiesta 2012.

Safari hii inatoka mbali tangu kipinhdi hicho katika maonesho ya malipo ya ujiria wa kiasi cha shilingi elfu moja—elfu moja yaliyokuwa yanaandaliwa na maporomota mbalimbali ikiwa ni pamoja na kina King Sapeto. Wakati unaenda, anatoa ngoma nyengine iliyokwenda kwa jina la “Kwako Nash MC”. Baadaye akatoa kandamseto ya “Hazina Sura ya Kwanza”. Kanda hii alienda kuiuza sehemu mbalimbali za nchi na hasa alienda Chuo Kikuu cha Dodoma na kuunza kanda hizi kwa wanafunzi. Yaani, mwanzo mwisho utamaduni wa handakini unavyotaka. Hiyo ilikuwa mwaka 2011. Tangu ameanza kujihusisha na muziki hajawahi kuimba zaidi ya kughani tu. Tangu 2011, ilikuwa kawaida sasa kutoa albamu kila mwaka, 2012 "Mzimu wa Shaaban Robert", 2013 "Chizi" na 2014 "Mchochezi".

Nash na Tamaduni Muzik[hariri | hariri chanzo]

Tamaduni ni lebo ambayo NASH alifanya nayo kazi kwa mafanikio makubwa sana. Kupitia Tamaduni Muzik waliweza kubadilisha na kutimiza nguzo karibia zote za hip hop zinavyotaka. Maoni ya NASH kuhusu Tamaduni Muzik ni kwamba ndio wao waliobadilisha mtazamo na mwelekeo mzimaa wa muziki wa hip hop ya Tanzania. Kupitia wao, tuliweza kuona kutolewa kwa albamu kwa sana hata kwa wasanii wachanga, kutoa kandamseto, kurudisha maonesho ya hip hop kukusanya wasanii “Kilingeni” huko Msasani Club.

Tamaduni Muzik laiti kama wangelikuwa wamesajiliwa au kutoa mikataba kwa wasanii, leo hii ingekuwa moja ya taasisi kubwa sana katika muziki wa Tanzania. Uzuri uliopo mahali ambapo shughuli za Tamaduni Muzik zilizokuwa zinafanyika ni karibu kabisa na ubalozi wa Marekani. Matukio yote walikuwa wanayaona, ila hila, urasimu na ubinafsi ulipo miongoni mwetu umepelekea kutopata msaada wowote kwa Tamaduni Muzik. Kifupi Tamaduni Muzik imehakikisha sanaa ya muziki wa hip hop inapata nafasi kubwa katika jamii ya Watanzania. Wameutetea mno muziki huu.

Diskografia[hariri | hariri chanzo]

Hii ni orodha ya albamu za Nash MC.

Na. Jina la albamu Mwaka Maelezo
1. Hazina Sura ya Kwanza 2011 Kandamseto ya kwanza kutoka kwa Nash tangu arudi rasmi kwenye muziki wa rap.
2. Mzimu wa Shaaban Robert 2012 Albamu rasmi ya kwanza kutoka kwa Nash
3. Chizi 2013
4. Mchochezi 2014 Albamu ya tatu kutoka kwa Nash
5. Diwani ya Maalim 2019 Albamu ya mwisho kutoa— Hii ni baada ya kuachia singo tu kwa muda mrefu
6. Mhadhiri (albamu) 2022 Albamu mpya imetoka 27 Novemba, 2022.

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. "Nash MC – Hip Hop African". hiphopafrican.com (kwa Kiingereza). Iliwekwa mnamo 2018-10-31. 
  2. Welle (www.dw.com), Deutsche, Nash MC na "Uzuri wa Kiswahili" | DW | 13.08.2018 (kwa sw-TZ), iliwekwa mnamo 2019-10-01