Nenda kwa yaliyomo

Nagib Mahfuz

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Nagib Mahfuz

Nagib Mahfuz (1911 - 2006) (kwa Kiarabu: نجيب محفوظ) alikuwa mwandishi nchini Misri aliyepokea Tuzo ya Nobel mwaka 1988 akiwa mshindi wa pili kutoka Afrika aliyepokea tuzo hiyo. Katika muda wa miaka 70 ya kazi alitunga riwaya 34, hadithi fupi zaidi ya 350, makumi ya mswada andishi ya filamu na tamthiliya 5. Nyingi za kazi zake zimechukuliwa kuwa filamu nchini Misri na nje ya Misri.

Maisha na elimu[hariri | hariri chanzo]

Mahfuz alizaliwa 11 Desemba 1911 katika familia ya wastani ya Waislamu kwenye eneo la Gamaliya mjini Kairo. Wazazi walimpa jina kulingana na profesa Naguib Pasha Mahfouz (1882–1974) tabibu mashuhuri Mkopti aliyesimamia kuzaliwa kwake. Katika familia yake alikuwa mtoto wa saba na mdogo kati ya akina kaka wanne na akina dada wawili.

Familia iliishi kwanza katika mtaa wa Bayt al-Qadi wa eneo la Gamaliya kwenye mji wa kale wa Kairo. 1924 walihamia Abbaseya iliyokuwa mtaa mpya upande wa kaskazini ya mji wa kale. Maeneo yote mawili yalirudia baadaye katika masimulizi na riwaya zake.

Babake Abdel-Aziz Ibrahim alikuwa mtumishi wa serikali na Mahfouz hatimaye alifuata mfano wake baada ya kumaliza shule na chuo. Mamake Fatimah alikuwa binti wa shehe kwenye chuo kikuu cha Al-Azhar. Hata kama yeye mwenyewe hakuweza kusoma wala kuandika alienda mara kwa mara pamoja na mtoto Mahfouz kutembelea na kuona mahali pa utamaduni kama Makumbusho ya Misri na Piramidi za Giza.[1]

Familia ya Mahfouz walikuwa Waislamu waaminifu na ulezi wa Mahfouz ulifuata kanuni za dini hii. Baadaye aliona ya kwamba msimamo katika familia yake ulikuwa kali kiasi akashangaa alipokuwa mzee: Usingefikiri ya kwamba siku moja msanii atatoka katika familia hii". [2]

Mahfouz alipokuwa na miaka 7 alishuhudia mapinduzi ya Misri ya 1919 akitazama kutoka dirisha ya nyumba jinsi gani wanajeshi walivyofyatulia risasi dhidi ya wanaume na wanawake walioandamana. Alisema baadaye "tukio moja lililonishtusha na kuvunja hisia ya usalama katika utoto wangu lilikuwa mapinduzi ya 1919".

Mahfouz alianza kusoma mapema akiathiriwa na Hafiz Najib, Taha Hussein na Salama Moussa aliyekuwa mfuasi wa shirika la kisoshalisti la Fabian Society.[3]

Baada ya kumaliza shule ya sekondari Mahfouz alisoma falsafa kwenye chuo kikuu cha Kairo alipomaliza kwa cheti ya BA mwaka 1934. Alianza tasnifa ya MA lakini aliiacha baada ya mwaka mmoja akaamua kufuata uandishi kama wito wake.

Ajira katika utumishi wa serikali na mwandishi[hariri | hariri chanzo]

Alitafuta ajira katika utumishi wa serikali akifuata nyayo za babake lakini wakati huohuo alianza pia kuchangia taarifa na hadithi fupi katika magazeti mbalimbali kama vile Al-Risala, Al-Hilal na Al-Ahram.

Ajira yake ya kwanza ilikuwa kama karani kwenye chuo kikuu, tangu 1938 katika wizara ya waqf. 1945 aliomba kuhamishwa kwenda maktaba ya makumbusho ya Sultan Al-Ghuri. Hapa alichukua nafasi ya kufanya mahojiano na wakazi wa mtaa penye maktaba. [4] Aliendelea na wajibu mbalimbali katika wizara ya utamaduni. [5]

Uandishi wake[hariri | hariri chanzo]

Katika muda wa miaka 70 ya kazi Mahfouz alitunga riwaya 34, hadithi fupi zaidi ya 350, makumi ya mswada andishi ya filamu na tamthiliya 5. Nyingi za kazi zake zimechukuliwa kuwa filamu nchini Misri na nje ya Misri.

Riwaya zake za kwanza kuanzia mwaka 1939 zilihusu maisha ya Misri ya kale wakati wa Mafarao.

Katika miaka ya 1940 alianza kusimulia habari za Misri ya kisasa. Riwaya yake ya 1959 "Watoto wa mtaa wetu" ilisababisha ugomvi na wataalamu waislamu waliodai inakashifu imani. Riwaya inatoa mfano wa historia ya binadamu wakiwemo watu wanaofanana na Adamu, Musa, Isa na Mohamad. Kitabu kilitolewa kimilango katika gazeti, lakini upinzani wa wataalamu Waislamu uliwalazimisha wahariri kusimamisha riwaya. Hadi leo haikuchapishwa kwa lugha ya Kiarabu katika nchi ya Misri ingawa inapatikana kwa Kiingereza pia toleo la Kiarabu kutoka Lebanon inapatikana kwa siri.

Riwaya yake mashuhuri zaidi ni "Thelathiya Alqahira" (Riwaya ya Kairo kwa sehemu tatu, ing. Cairo trilogy) anamosimulia maisha ya vizazi vitatu vya familia mbalimbali mjini Kairo kuanzia Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia hadi mapinduzi ya 1952 iliyomfukuza Mfalme Farouk. sehemu za riwaya zake zilitolewa mlango kwa mlango katika gazeti Al-Ahram na kufikia wasomaji wengi sana. Alipopokea Tuzo ya Nobel ya Fasiki kulikuwa na riwaya chache tu zilizotafsiriwa hadi wakati ule kwa lugha za Ulaya.[6]

Mwaka 1989 shehe Mmisri Omar Abdul-Rahman alitamka mbele ya wanahabari ya kwamba heri Mahfuz angeadhibiwa wakati ule. Tamko hili lilisababisha jaribio la Waislamu wakali la kumwua Mahfuz. Hadi kifo chake aliishi chini ya ulinzi wa Polisi.

Orodha ya maandiko yake[hariri | hariri chanzo]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. El-Enany, Naguib Mahfouz: The Pursuit of Meaning, Psychology Press 1993, isbn=978-0-415-07395-0
  2. "You would never have thought that an artist would emerge from that family." Rasheed El-Enany, Naguib Mahfouz: The Pursuit of Meaning, Psychology Press 1993, isbn=978-0-415-07395-0, iliangaliwa kupitia google books
  3. Charlotte El Shabrawy (Summer 1992). "Naguib Mahfouz, The Art of Fiction No. 129". The Paris Review. Iliwekwa mnamo Septemba 25, 2012.{{cite journal}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  4. El-Enany, Rasheed. "Naguib Mahfouz: His Life and Times". Cairo:AUC Press, 2007. pp 170-174
  5. Tore Frängsmyr; Sture Allén (1993). Nobel Lectures: Literature, 1981-1990. World Scientific. uk. 121. ISBN 978-981-02-1177-6. Iliwekwa mnamo 26 Septemba 2012.{{cite book}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  6. "The Novel~Tea Book Club discussion". GoodReads. Iliwekwa mnamo 24 Oktoba 2013.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)

Viungo vya Nje[hariri | hariri chanzo]

Wikiquote ina mkusanyiko wa dondoo kuhusu:
Wikimedia Commons ina media kuhusu: