Misri (1805-1881)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Misri (1805-1881) ni kipindi katika historia ya nchi ya Misri ambako mabadiliko mengi yalitokea yaliyopelekea jinsi Misri ya leo ilivyo. Mabadiliko haya yalikuwa ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. Kilikuwa ni kipindi cha mvuvuko wa nchi kutoka hali ya ukabaila kwenda katika uchumi wa kibepari. Ndani ya kipindi hiki Misri iliweza kujizatiti kutoka tawala za nje na hasa zile za Ulaya. Mifumo mbalimbali ya elimu ilianzishwa katika kipindi hiki. Pia mapinduzi ya nchi hii mnamo miaka ya 1881/1882 yalileta sura mpya katika nchi ya Misri hasa katika mtazamo wa dini ya kiislamu. Halikadhalika mapinduzi yalijaribu kuinasua nchi kutoka katika ukandamizaji wa Kiingereza kitendo ambacho hakikufanikiwa kwa kiwango cha juu.

Mjongeo wa taifa la Misri[hariri | hariri chanzo]

Mizizi ya utaifa wa Misri inarudi nyuma zaidi. Katika kipindi cha karne ya kumi na nane kinapaswa kuangaliwa kama maabara ambamo Misri mpya ilitungwa. Maelemeo matatu katika karne ya kumi na nane yaliashiria mwelekeo huu.

  • Kwanza ni mageuzi ya watu kama vile Ali Bey al-Kabir yaliyojaribu kupunguza idadi ya miundo ya kikabaila iliyothibitiwa na Mamluki katika delta ya Misri ya Chini.
  • Kisha kulikuwepo na vuguvugu la uhuishaji katika Uislamu lililoongozwa na Sheikh Hassan al-Attar.
  • Na tatu, kuibuka katika majiji ya Cairo, Alexandria na mengineyo, kwa kikundi cha watu mashuhuri, wasomi na wafanyabiashara, waliotarijika hasa kutokana na ardhi, waliokuwa tayari kutoa rasilimali zao kuendeleza kile kilichokuja kujulikana kama “juhudi ya kitaifa”.

Yote haya yaliungana na mambo mengine na kuzaa vuguvugu la kitaifa la Misri lililokuwa na athari kubwa iliyoenea kote. Uhamishwaji wa jeshi la wavamizi wa Kifaransa mwaka 1801 ulitoa nafasi kwa vuguvugu la kitaifa la Misri kujiimarisha na kutaka kujitawala ndani ya himaya ya Kituruki. Hata hivyo, hadhi ya Misri kunako 1805 bado ilikuwa ile ya jimbo la himaya ya Kituruki.

Muhammad Ali Pasha[hariri | hariri chanzo]

Muhammad Ali Pasha al-Mas'ud ibn Agha

Wazo la Misri huru halikutoka kwa Muhammad Ali Pasha. “Jeshi la Makhufu” (Coptic Legion) la jumuiya ya “Ndugu Huru” ya Jenerali Yakub lilikuwa tayari limekwisha kulitangaza, lakini vuguvugu lao lilivunjika kufuatia kumalizika kwa Msafara wa Wafaransa na kuondolewa kwa kiongozi wao. Wafaransa walihimiza wazo la Misri huru kupinga utamalaki wa Waingereza. Hata hivyo, mawazo ya Muhammad Ali Pasha ya uhuru wa Misri yalitofautiana na yale ya Waingereza au Wafaransa.

Baada ya kushika madaraka huko Misri, Ali alijizatiti kuimarisha nafasi yake na kulijenga taifa lake. Katika harakati hizo, kunako 1807 aliwashinda Waingereza ambao walikuwa wakifanya hujuma dhidi ya mamlaka yake. Kisha alikomesha athari za Mamluki katika Misri ya Juu, hasa kwa vile walikuwa wakishirikiana na Waingereza. Kunako 1811, aliwafutilia mbali viongozi wa upinzani wa Mamluki ambao walikuwa wakikwamisha juhudi zake za kupata mamlaka ya kisiasa katika Misri ya Chini. Baada ya kuwaondoa Mamluki, Ali alishughulikia ujenzi wa himaya na jukumu la ufufuaji wa taifa.

Mtoto wa Muhammad Ali Pasha, Ibrahim Pasha ambaye pia alikuwa jenerali mkuu, aliyashitua mataifa ya Ulaya kutokana na ushindi wa awali alioupata kutoka kwenye vita kati ya Uturuki na Misri. Mataifa ya Ulaya yaliamua kumuokoa Sultani wa Uturuki. Hii ni kwa sabubu walijua kwamba kama Muhammad Ali Pasha angeachiwa kuiangamiza himaya ya Kituruki na kuanzisha mamlaka yake, upanuzi wa ukoloni wao ungepingwa, na majimbo mengine ya himaya ya Kituruki yangehuishwa na kuimarishwa chini ya uongozi wake.

Ismail[hariri | hariri chanzo]

Ismail (1863-79) aliyerithi baada ya tawala fupi za al-Abbas na Said, aliona kuwa tatizo la kitaifa lilihusu uhuru na kujitawala kitaifa. Alibuni mkakati wa kupunguza utegemezi wa Misri kwa Uturuki kwa njia ya mazungumzo, ambapo baadaye angeifanya Misri iwe nchi huru na kisha angeanzisha asasi za serikali ya ndani. Kwa maneno mengine, Ismail alidhani kwamba njia za taratibu za kulishughulikia suala la uhuru wa Misri zingekuwa bora zaidi kuliko papara za kutumia nguvu. Ili kuimarisha nafasi yake, alianzisha mfumo wa kurithishana ufalme wa Misri, na pia akajipatia cheo cha Khedive. Zaidi ya hayo alijitwalia haki ya kutangaza sheria za kiutawala na ya kujadiliana juu ya mipango ya kiuchumi na nchi za kigeni bila kulazimika kuidhinishwa kwanza na Sultani. Na mnamo 1873 aliifasili Misri kama “taifa/dola”.

Kilimo na matumizi ya ardhi[hariri | hariri chanzo]

Kabla ya karne ya kumi na tisa, ardhi ilisimamiwa na wamultazim ambao jukumu lao kuu lilikuwa kukusanya mapato yaliyohitajika toka kwenye vijiji vyao na kuyapeleka hazina kuu. Hata hivyo, madaraka waliyokuwa nayo wamultazim juu ya ardhi yalionekana kwamba yangekwamisha maendeleo ya Misri kama taifa unganifu la kisasa. Ili kutatua tatizo hili, Muhammad Ali Pasha alibuni sera ya mgawanyo wa ardhi ambapo ardhi yote inayofaa kwa kilimo nchini Misri iligawanywa katika baadhi (kategoria) sita ambazo ziligawiwa kwa matabaka ya watu yafuatayo: familia ya Muhammad Ali Pasha na maofisa wa kijeshi; Mamluki; Maulama; watawala wa kigeni nchini Misri; Mafallahin (wakulima wadogo wadogo); na Mabedui.

Sera hii ya mgawanyo wa ardhi haikupokewa vizuri na watu, hususani wale waliopokonywa ardhi yao na dola. Hata hivyo, sera ya ardhi ya Muhammad Ali yapaswa kuchukuliwa kama hatua ya mpito kati ya ukabaila na ubepari. Kwa maneno mengine, ilikuwa ni hatua ya lazima endapo Misri ilitaka kujitoa kutoka taifa lenye utegemezi mkubwa wa ardhi na kuwa taifa linalotegemea nguvu za mitaji na masoko.

Muhammad Ali pia aliugeuza uchumi wa kilimo wa Misri kutoka ngazi ya kijungujiko na kuwa uchumi wa mazao ya biashara kwa kuhimiza ulimaji wa pamba sambamba na kilimo cha nafaka. Zaidi ya mifereji thelathini ilichimbwa kwa ajili ya kumwagilia mashamba ya taifa.

Kipindi cha 1840-79 ndicho kilikuwa cha mpito kwa Misri kutoka ukabaila kwenda kwenye hatua za mwanzo za uchumi wa kibepari ambao kwa kiwango kikubwa ulikuwa wa kilimo. Kwa kweli, sera ya serikali kumilki ardhi ilikuwa ni matayarisho ya umilikaji ardhi wa binafsi. Mwaka 1858, sheria ilipitishwa ambayo ilianzisha haki ya umilikaji binafsi wa ardhi na ilipofika 1880 watu kadhaa walikuwa wameshajitwalia maeneo makubwa ya ardhi.

Maendeleo ya kitamaduni[hariri | hariri chanzo]

Katika kutafuta mvuvumko wa kitaifa, suala la maendeleo ya kitamaduni linahitaji kutiliwa maanani. Baadhi ya watu walifikiri kwamba usasishaji wa uchumi, viwanda na siasa lazima uambatane na uigaji wa maadili ya nchi za Magharibi, ilihali wengine waliamini katika uanzishwaji wa falsafa halisi ya utamaduni wa kitaifa. Maandishi na mawazo ya Sheikh Rifaa al-Tahtawi (1801-73) yalikuwa muhimu katika mchakato huu.

Asasi za elimu zilizoendelea za wakati wa Muhammad Ali zilipanuliwa na kupatiwa nguvu za kisheria na sera ya elimu ya taifa ya Ismail. Mfumo wa elimu wa Misri ulichanganya sifa za kimapokeo na za kisasa; ulikuwa na chuo kikuu cha kimapokeo chenye kiwango cha juu kabisa cha taaluma, asasi nyingi za kisayansi zenye mtaala uliokitwa katika mawazo ya kisasa ya kisayansi na kielimu-jamii.

Kwa hiyo, palitokea jumuiya ya wasomi nchini Misri ambayo, kwa upande wake, iliwezesha usitawi wa vyombo vya habari na vuguvugu la uchapishaji. Zaidi ya hayo Misri ilikuwa kimbilio la wasomi na waandishi kutoka sehemu mbalimbali za himaya ya Kituruki waliokimbia mateso kutoka utawala wa kifalme.

Mapinduzi ya Urabi: 1881-82[hariri | hariri chanzo]

Wakati ambapo mabwenyenye wa Misri walipata umashuhuri baada ya 1840 na watu kama vile Tahtawi na A. Mubarak wakaanzisha utamaduni halisi wa kitaifa, jeshi la Misri lilikuwa ndio lenye nguvu zaidi katika Afrika. Jeshi hili lilikuwa na dhima kubwa katika jitihada za kuleta mapinduzi nchini Misri. Kuibuka kwa kikundi chenye nguvu kiitwacho “Kikundi cha Hilwan” kikiongozwa na Urabi kilikuwa ndio mwanzo wa mapinduzi. Kikundi kilishinikiza matakwa yake kwa taifa na kikafanikiwa wakati mwingine. Hatimaye kilibadilika kabisa na kuwa chama cha kitaifa mwaka 1879, ambacho kilishirikiana kwa karibu na vikundi vyenye wafuasi wengi nchini na kufungamana mno na jeshi.

Kufuatia kung’atuliwa kwa nguvu kwa Ismail kunako 1879, chama cha kitaifa, kikiungwa mkono na jeshi, kilimdhibiti kwa werevu mtawala mpya, Khedive Tawfik, na kumfanya kibaraka. Kutokana na hali hii, mataifa ya Ulaya yaliamua kulishughulikia suala la Misri kwa uvamizi wa kijeshi. Hivyo, kunako 1882 kikosi cha manowari cha Waingereza kiliishambulia kwa mabomu Alexandria. Uvamizi huu uliangamiza jeshi la Misri na Urabi.

Ingawa mapinduzi ya Misri hayakutekeleza malengo yake ya muda mfupi, yalikuwepo mafanikio kadha wa kadha yaliyotokana na kipindi hicho. La kwanza ni uhuishaji wa fikra za Kiislamu. Hili lilitumiwa kuhamasisha uungaji mkono wa mapinduzi. Chimbuko la uozo wa kitaifa uliochochea ari ya mapinduzi lilionekana kama ni upotoshaji wa Uislamu. Hivyo mageuzi yoyote ya maana nchini ilibidi yafungamane na misingi ya dini. Uislamu huu wa siasa kali kwa hiyo ulikuwa na nafasi muhimu sio tu katika uhuishaji wa kisiasa uliopelekea kwenye mapinduzi yaliyoshindwa, bali pia katika masuala ya kijamii ya ufufuaji wa taifa.

Tukio jingine muhimu la kipindi hiki cha historia ya Misri ni kuibuka kwa Abdallah al-Nadim (1843-96), aliyefundisha umma misingi na mawazo ya utaifa. Aliweza kuamsha maoni ya umma kupitia magazeti yake. Kupitia maandishi yake alichochea itikadi ya kitaifa ambayo wakati huo ilizidi kuwa kali na kuwa chachu muhimu kwa ufufuaji wa taifa. Hivyo alikuwa msemaji mkuu wa umma wa wafallahin ambao baadaye aliwatangaza kuwa wadhibiti wa mapinduzi.

Taathira ya Misri[hariri | hariri chanzo]

Ufufuaji wa Misri ulikuwa na athari iliyofika mbali. Baadhi ya maeneo barani Afrika kama vile Sudan, Ethiopia, Pembe ya Afrika (eneo la Kaskazini mashariki mwa Afrika) na eneo la Maziwa Makuu katika Afrika ya Kati yalipambana kwa mara ya kwanza na ubepari wa Misri uliobuniwa wakati wa kipindi cha mvuvumko. Mzinduko wa Misri pia ulitishia “mpango wa dunia” kama ulivyokuwa wakati huo, na mataifa yenye makoloni yaliona suluhisho la tishio hili ni upunguzaji wa silaha kwa Afrika.

Tazama Pia[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya Nje[hariri | hariri chanzo]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. Dodwell, H. H. (1976) The Founder of Modern Egypt; a Study of Muhammad Ali (Cambridge: CUP)
  2. Vatikiotis, J. Panayiotis (1980) The History of Egypt, Weidenfeld and Nicolson, London
  3. Baer, Gabriel (1962) A history of landownership in modern Egypt, 1800-1950, Oxford University Press, London
  4. Nchi ya Misri
  5. Mapinduzi ya Urabi, Cambridge[dead link]