Nenda kwa yaliyomo

Machafuko ya Darfur

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mama na mtoto wake mgonjwa katika kambi ya walifurushwa makwao ya Abu Shouk katika eneo la Kaskazini la Darfur.

Machafuko ya Darfur yalianza katika eneo la Darfur, Sudan, mnamo Februari mwaka wa 2003 wakati ambapo Jeshi la Ukombozi la Sudan na Harakati ya Haki na Usawa zilichukua silaha na kuanza kushutumu serikali kwa kuwadhulumu wananchi Waafrika huku ikiwapendelea Waarabu.

Wahusika[hariri | hariri chanzo]

Upande mmoja, ambao unajumuisha jeshi la Sudan na Janjaweed, kundi la wanamgambo lenye wapiganaji kutoka makabila ya Abbala ambayo ni mchanganyiko wa Waarabu na Waafrika wa kanda ya kaskazini katika eneo la Rizeigat la Sudan. Makabila haya haswa ni wafugaji wa kuhamahama ambao huchunga wanyama kama vile ngamia.

Upande mwingine ulikuwa wa makundi ya waasi, hasa Jeshi la Ukombozi la Sudan na Harakati ya Haki na Usawa, ambayo yalipata wapiganaji kutoka makabila ambayo si ya Kiarabu wala ya Kiislamu, kama vile Fur, Zaghawa, na Masalit.

Serikali ya Sudan, ingawa imekana hadharani kuwa haiwasaidii wanamgambo wa Janjaweed, inashutumiwa kwa kuwasaidia kifedha, na kwa kuhusika katika mashambulizi ya pamoja yanayolenga raia. Serikali ya Sudan imelaumiwa kwa kuharibu ushahidi, kama vile kufunika makaburi ambapo watu wengi wamezikwa. Pia serikali hiyo imewakamata na kuwanyanyasa wanahabari, hivyo kufanya ripoti za habari kutoka eneo la Darfur kuwa chache. Nyuma ya serikali, China na Iran zimeunga mkono sana mauaji kwa kutoa silaha nyingi za aina mbalimbali, zikiwemo za kikemia.

Itikio la kimataifa[hariri | hariri chanzo]

Ingawa serikali ya Marekani imeufafanua mgogoro katika eneo hilo kama mauaji ya kimbari, Umoja wa Mataifa tarehe 31 Januari 2005 ulitoa ripoti ya kurasa 176 ikisema kuwa, ingawa kulikuwa na mauaji kwa wingi na ubakaji wa raia wa eneo la Darfur, haingeweza kuyatambua mateso hayo kama "mauaji ya kimbari" kwa sababu "nia ya kufanya mauaji ya kimbari haikuwepo".

Wanaharakati wengi, hata hivyo, wanatambua mgogoro katika eneo la Darfur kama mauaji ya kimbari, kama vile mashirika ya Save Darfur Coalition, Aegis Trust na Genocide Intervention Network. Mashirika hayo yanaashiria matamshi ya Katibu Mkuu wa zamani wa Marekani Colin Powell, yaliyotambua mgogoro kama mauaji ya kimbari. Mashirika mengine ya kiharakati, kama vile Amnesty International, ingawa yanaomba hatua ya kimataifa ichukuliwe, wanakataa kutumia maneno mauaji ya kimbari.

Kuna makadirio mbalimbali ya idadi ya watu waliouawa. Serikali inadai ni 10,000 tu, lakini Umoja wa Mataifa unasema ni 300,000. Vilevile waliokimbia eneo lao ni 450,000 tu kadiri ya serikali, bali 2,850,000-3,000,000 kadiri ya UM.

Mbali ya hayo, ubakaji wa watoto na wanawake umezidi, hasa kutokana na hamu ya serikali ya kufuta uwepo wa wasio Waarabu nchini.

Kwa sababu hiyo, rais wa Sudan, Omar al-Bashir amekuwa rais wa kwanza kufunguliwa kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai akiwa madarakani. Mashtaka ni mauaji wa kimbari, makosa ya jinai ya kivita na makosa ya jinai dhidi ya utu. [1]

Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Machafuko ya Darfur kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. "The Prosecutor v. Omar Hassan Ahmad Al Bashir". International Criminal Court. Retrieved 24 April 2016.

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]