Hannibal

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Sanamu ya Kiroma, inaaminiwa ni Hannibal.
Kampeni maarufu ya Hannibal ya kuvuka Alpi pamoja na Tembo wa vita; picha ya 1510, Makavazi ya Capitoline, Roma.

Hannibal (Hǎnnibal Barca, 247 KK - 183 au 181 KK), alikuwa mwanasiasa na mwanajeshi wa nchi ya Karthago katika Afrika ya Kaskazini. Anakumbukwa kama adui mkuu wa Jamhuri ya Roma.

Baba yake alikuwa Hamilkar Barka, kiongozi wa jeshi la Karthago katika Vita ya kwanza kati ya Roma na Karthago.

Hannibal anajulikana hasa kwa uongozi wake wa jeshi la Karthago katika Vita ya Pili kati ya Roma na Karthago kati ya 218 KK hadi 201 KK.

Hannibal kama kiongozi wa jeshi[hariri | hariri chanzo]

Mwaka 218 aliongoza jeshi lake kutoka Hispania kupitia Gallia hadi Italia akivuka milima ya Alpi na jeshi lake la askari 40,000 na tembo wa vita[1]. Aliwashinda Waroma katika mfululizo wa mapigano pamoja na Mapigano ya Cannae ambako aliua sehemu kubwa ya jeshi la Roma[2].

Hata hivyo alikosa nguvu na mitambo ili aweze kuteka mji wa Roma[3], hivyo alizungukazunguka na jeshi lake katika Italia kwa miaka kadhaa. Sehemu ya viongozi wa Karthago waliogopa uwezo wake wakazuia asipate misaada na wanajeshi wapya kutoka nyumbani; baadaye Jeshi la majini la Roma lilizuia jitihada ya kutuma misaada kwake.

Hatimaye kwenye mwaka 204 Roma ilituma jeshi huko Afrika ya Kaskazini ambalo lilishinda Wakarthago mara mbili. Hannibal alipaswa kurudi nyumbani akaongoza jeshi la nyumbani lililoundwa na askari wapya wasio na uzoefu na hapo alishindwa mara ya kwanza katika mapigano ya Zama. Karthago ilipaswa kukubali masharti ya amani na kulipa fidia kubwa.

Baada ya vita[hariri | hariri chanzo]

Baada ya vita Hannibal alishiriki kwa miaka kadhaa kwenye serikali ya mji[4] wake lakini hatimaye kwenye mwaka 195 maadui walimlazimisha kuondoka na kwenda ugenini[5].

Hannibal alipokewa na mtawala wa Syria Antioko III akimshauri katika mambo ya kijeshi katika vita yake dhidi ya Roma. Baada ya ushindi wa Roma alipaswa kuondoka katika Syria akazunguka katika falme za Asia Ndogo.

Alipokuwa mgeni wa mfalme wa Bitinia, Waroma walimlazimisha mfalme huyu kumkabidhi Hannibal kwao. Lakini kabla hajakamatwa, Hannibal alijiua [6].

Jinsi alivyotazamwa baadaye[hariri | hariri chanzo]

Ramani ya Mapigano ya Cannae ambako Hannibal aliangamiza jeshi la Roma mnamo mwaka 206.

Wanahistoria wa kijeshi wanamwona Hannibal kama kiongozi wa kijeshi mwenye uwezo mkubwa. Hasa mikakati aliyotumia huko Cannae ilichunguliwa na kufundishwa katika vyuo vya kijeshi kote duniani. [7] Lakini pia uwezo wake kudumu katika nchi ya kigeni, bila misaada kutoka nyumbani kwake, na kushinda au kujitetea miaka mingi dhidi ya jeshi kubwa unasifiwa[8].

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. Lancel, Serge (1999). Hannibal. Wiley. ISBN 978-0-631-21848-7. , p. 60]
  2. https://archive.org/details/ospreycam036cannae216bc Mark Healey: Cannae 216 BC: Hannibal smashes Rome's Army, Campaign series 36
  3. Prevas, John, Hannibal Crosses the Alps, p. xv
  4. De Beer, Sir Gavin (1969). Hannibal: Challenging Rome's Supremacy p.291.
  5. De Beer, Sir Gavin (1969). Hannibal: Challenging Rome's Supremacy p.296.
  6. "Appian, The Syrian Wars 3 - Livius". www.livius.org. Iliwekwa mnamo 5 October 2020.  Check date values in: |accessdate= (help)
  7. RICK JAY MESSER. "THE INFLUENCE OF HANNIBAL OF CARTHAGE ON THE ART OF WAR AND HOW HIS LEGACY HAS BEEN INTERPRETED". CiteSeerX 10.1.1.582.1385.
  8. Hannibal Archived 17 Oktoba 2011 at the Wayback Machine at CarpeNoctem.tv

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]