Nenda kwa yaliyomo

Habib Swaleh Jamali Layl

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Habib Swaleh bin Alawy (1853 - 1935) alikuwa ulama na sufii aliyeanzisha na kuunda msikiti wa Riyadha pamoja na madrasa yake kwenye mji wa Lamu (leo nchini Kenya). Anakumbukwa kwa mafundisho yake na athira yake katika Uislamu wa Lamu na Afrika ya Mashariki kwa jumla.

Aliimarisha kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad na hivyo msingi kwa sherehe maarufu ya Maulidi inayokusanyisha Waislamu kutoka nchi mbalimbali pale Lamu.

Alizaliwa Ngazija (Komoro) katika kijiji cha Sanghani mnamo mwaka 1853 BK sawa na mwaka 1269 Hijriyah. Mama yake aliitwa Mariam binti Ali, mwenye asili ya Kingazija (Komoro) kutokana na ukoo wa Nye Rajab. Baba yake aliitwa Sayyid Alwy bin Abdallah Jamali layl (Fundi Alawi).

Nasabu yake[hariri | hariri chanzo]

Swaleh bin Alwy (Fundi Alawi) bin Abdallah bin Hassan bin Ahmad bin Abdallah (Swahib Tuyyur) bin Ahmad bin Harun bin Abdul-Rahman bin Ahmad bin Abdallah bin Shaykh Muhammad Jamali layl bin Hassan bin Muhammad Bin Hassan Al-Taraaby bin Ali bin (Faqiihul-Muqaddam) Muhammad bin Ali Ba’alawy bin Muhammad (Swahibul-Mirbat) bin Ali (Khali-Qassam) bin Alwy bin Muhammad (Swahib-Sawma’ah) bin Alwy bin Ubeidi llah bin (Al-Imam Al-Muhajir Ila-llahi) Ahmad bin Issa bin Muhammad An-Naqib bin Ali Al-Ureidhy bin Ja’afar Al-Swadiq bin Muhammad Al-Baqir bin Ali (Zain Al-Abidin) bin Hussein Al-Sibt bin Ali bin Abi Twalib, vile vile Hussein Al-Sibt bin Fatma Al-Zahra binti Rasuuli llah.

Elimu yake[hariri | hariri chanzo]

Al-Habib Swaleh alipata malezi bora na mazuri kutoka kwa wazazi wake, Sayyid Alwy na Bi Mariam Ali, na akapata kusoma Qurani na baadhi ya masomo kwa babake kwa kuwa alikuwa ni mwalimu wa Qurani tena hodari sana, na kutokana na uhodari wake wa kufunza alipewa jina la lakabu (nick name) la Fundi Alawi na pia alikuwa ni fundi mahiri sana wa ushonaji nguo, na alifariki katika mwaka wa 1895 AD akiwa na umri wa zaidi ya miaka mia.

Habib Swaleh baada ya kusoma kwa babake na kuweza kumiliki baadhi ya mas-ala ya dini ya kiislamu, pia alipata fursa ya kuendeleza masomo yake ya juu kwa aliyekuwa binamu wake, Sayyid Abal Hassan bin Ahmad bin Abdallah Jamali layl [Mwenye Bahassan], ambaye pia alikuwa mwalimu wa Sayyid Ahmad bin Abubakar bin Sumeit, Sayyid Abal Hassan alifariki katika mwaka wa 1883 BK.

Habib Swaleh kisha katika mwaka wa 1862 AD (sawa na 1287 Hijriya) wakati huo akiwa na miaka 18, alisafiri kuelekea Lamu kwa ajili ya matibabu kutokana na maradhi ya miguu yaliyokuwa yamemkumba, na huko akashukia kwa ami yake Sayyid Ali bin Abdallah Jamali layl.

Al-Habib Swaleh alipokuwa Lamu akiendelea na matibabu, alikuwa pia yuaendeleza masomo yake kwa ami yake Sayyid Ali, baada ya mwaka babake akamtaka arudi Ngazija na akamtuma ndugu yake mkubwa Sayyid Muhammad akamfuate.

Al-Habib Swaleh baada ya kurudi Comoro na kukaa karibu mwaka huko, babake alimruhusu kusafiri kurudi tena Lamu. Hapa Lamu alikamilisha masomo yake yaka akawa kiongozi wa sala na mwalimu kwenye msikiti wa Sheikh Biladi hadi kuanzisha madrasa na msikiti wa Riyadha.

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Makala hii kuhusu mtu huyo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Habib Swaleh Jamali Layl kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.