Nenda kwa yaliyomo

Rusu (mnyoo)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Enterobius vermicularis)
Rusu
Jike la rusu (Enterobius vermicularis)
Jike la rusu (Enterobius vermicularis)
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia
Nusuhimaya: Eumetazoa
(bila tabaka): Bilateria
(bila tabaka): Protostomia
Faila ya juu: Ecdysozoa
Faila: Nematoda
Ngeli: Chromadorea
Oda: Oxyurida
Familia ya juu: Oxyuroidea
Familia: Oxyuridae
Nusufamilia: Enterobiinae
Jenasi: Enterobius
Leach, 1853
Spishi: E. vermicularis
(Linnaeus, 1758)

Rusu (Enterobius vermicularis) ni spishi ya mnyoo kidusia wa familia Oxyuridae katika faila Nematoda anayeishi katika utumbo mpana wa watu. Husababisha mwasho katika eneo la mkundu. Ambukizo la rusu linaitwa enterobiasisi.

Mofolojia

[hariri | hariri chanzo]

Jike mpevu ana ncha kali ya nyuma na ana urefu wa mm 8-13 mm na unene wa mm 0.5. Dume mpevu ni mdogo sana kuliko hiyo na ana urefu wa mm 2-5 na unene wa mm 0.2 Ncha ya nyuma ya dume iliyopindika. Mayai hupitisha nuru na kuwa na uso anaonata vitu. Mayai hupima µm 50-60 kwa µm 20-30 na huwa na ganda nene limetandazwa upande mmoja. Ukubwa mdogo na kutokuwa na rangi kwa mayai huwafanya wasionekane kwa macho, isipokuwa kwa mkusanyiko wa maelfu ya mayai. Mayai yanaweza kuwa na kiinitete kinachokua au lava kamili ya mnyoo. Lava hukua hadi urefu wa µm 140-150.

Mzunguko wa maisha

[hariri | hariri chanzo]

Mzunguko mzima wa maisha, kutoka yai hadi mpevu, hufanyika katika mfereji wa utumbo wa kidusiwa mmoja na hudumu wiki 2-6. Rusu hubambua mara nne: mara mbili za kwanza ndani ya yai kabla ya kutoka na mara mbili kabla ya kuwa mnyoo mpevu.

Ingawa maambukizo mara nyingi hutukia kupitia kumeza mayai yenye viinitete kwa sababu ya watu hawanawi mikono ya kutosha au kung'ata kucha, kuvuta mayai ndani ya hewa ikifuatiwa na kuyameza, kunaweza kutokea mara chache. Mayai hutoa lava kwenye mbuti (yaani, sehemu ya kwanza ya utumbo mwembamba). Lava wa rusu wanaoibuka hukua haraka hadi saizi ya µm 140-150 na huhama kupitia utumbo mwembamba kuelekea utumbo mpana. Wakati wa uhamiaji huo, hubambua mara mbili na kuwa wapevu. Majike wanaishi kwa wiki 5-13 na madume karibu wiki 7. Rusu wa kiume na wa kike hupandana katika ileamu (yaani sehemu ya mwisho ya utumbo mwembamba), kisha rusu wa kiume hufa kwa kawaida na hupitishwa na kinyesi. Rusu wa kike wenye mayai hukaa kwenye ileamu, sikamu (yaani, mwanzo wa utumbo mpana), kibole na utumbo mpana unaoinuka, ambapo hujiunga na kiwambo-ute na kumeza yaliyomo ndani ya utumbo mpana.

Takriban mwili mzima wa jike hujaza na mayai. Makadirio ya idadi ya mayai kwenye rusu wa kike yanaenda kutoka 11,000 hadi 16,000. Mchakato wa kutaga mayai huanza takriban wiki tano baada ya kumeza mayai ya rusu na binadamu kidusiwa. Rusu wa kike huhamia kupitia utumbo mpana kuelekea kwenye puru kwa kasi ya sm 12-14 kwa saa. Wanaibuka kutoka kwenye mkundu ili kupata oksijeni kwa kukomaa kwa mayai au ili kutaga mayai. Kusogea kwao kwenye ngozi karibu na mkundu husababisha mwasho. Majike hutaga mayai ama kupitia (1) kufupisha na kufukuza mayai, na kufa baadaye, (2) kufa na kisha kusambaratika au (3) kupasuka kwa sababu ya kukuna rusu na kidusiwa.