Alinikisa Cheyo
Alinikisa Cheyo (alizaliwa Ndawa, kijiji cha Mwembe, Wilaya ya Mbozi, (mkoa wa Mbeya, 27 Machi 1960) ni askofu wa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Kusini Magharibi.
Alizaliwa katika familia yenye watoto 9 yeye akiwa wa 6. Baba yake Felick Cheyo na mama yake Ndimbumi Sinyanga ni wakulima na ni Wakristo wa Kanisa la Moravian Tanzania.
Elimu yake
[hariri | hariri chanzo]Alisoma Shule ya Msingi Mwembe tangu mwaka 1969 na kisha alijiunga na shule ya kati Haloli mjini Vwawa Mbozi. Baada ya hapo alijiunga na Chuo Cha Biblia cha Kanisa la Africa Inland cha Majahida kilichopo wilaya ya Bariadi Mkoa wa Shinyanga mwaka 1979 hadi 1981. Mwaka 1983 alijiunga na Chuo Cha Theologia cha Kanisa la Moravian kilichopo Mbeya (Motheco) ambapo alimaliza masomo mwaka 1986 na kutunukiwa cheti cha theologia. Akiwa Mbeya aliweza kujiendeleza kielimu kwa kujiunga na masomo ya Sekondari na mwaka 1987 aliweza kufanya mtihani wa kidato cha nne katika shule ya sekondari Mbeya Day. Alifanya tena mtihani wa sekondari katika kituo hicho hicho cha Mbeya Day Secondary mwaka 1999 na kutunukiwa cheti.
Mwaka 1994 mwishoni alikuwa nchini Ujerumani akichukua kozi ya lugha ya Kijerumani katika Taasisi ya Goethe Schwaebisch Hall ambako alihitimu mwaka 1995 na kutunukiwa cheti. Mwaka huohuo 1995 alijiunga na Chuo Cha Diakonia - Martin-Luther-Kolleg nchini Austria katika mji wa Feldkirchen karibu na Klagenfurt. Alimaliza masomo yake ya diakonia mwaka 1997 na kurudi Tanzania. Mwaka 2003 alijiunga na Chuo Kikuu Cha St. Paul Limuru Kenya na Kutunukiwa Shahada ya Kwanza ya Theologia (BD) mwaka 2006. Mwaka 2007 alijiunga na Catholic University of Eastern Africa na kutunukiwa shahada ya Uzamili katika Theologia (Master's in Theology) mwaka 2010. Mwaka huohuo 2010, aliendelea na masomo ya shahada ya uzamivu (doctorate) hapohapo Catholic University.
Askofu
[hariri | hariri chanzo]Amechaguliwa kuwa askofu wa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Kusini Magharibi tangu mwaka 2000. Amekuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji tangu mwaka 2011.