Nenda kwa yaliyomo

Yordani (mto)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mto wa Yordani
Mto Yordani
Chanzo Mlima Hermoni (mpakani wa Israel na Lebanon]])
Mdomo Bahari ya Chumvi
Nchi Lebanon, Syria, Israel, Yordani, Palestina
Urefu 400 km (170 km mwendo wa ndege)
Kimo cha chanzo takriban 300 m juu ya UB
Tawimito Hazbani, Dan, Banyas, Yarmuk
Eneo la beseni km²

Yordani (kwa Kiebrania: נהר הירדן nehar hayarden; kwa Kiarabu: نهر الأردن nahr al-urdun) ni mto mdogo katika Mashariki ya Kati lakini ni kati ya mito inayojulikana sana duniani kwa sababu imetajwa mara nyingi katika Biblia.

Hivyo katika dini za Uyahudi na Ukristo Yordani ina maana ya pekee: kwa Wayahudi unakumbusha tukio la Yoshua kuwaongoza babu zao kuuvusha pakavu wakati wa kuvamia nchi ya Kanaani. Kwa Wakristo unakumbusha pia ubatizo wa Yesu kwa mikono ya Yohane Mbatizaji.

Kwa sehemu kubwa ya njia yake uko chini ya usawa wa bahari na ni mpaka kati ya ufalme wa Yordani upande wa mashariki na maeneo ya Palestina na Israel upande wa magharibi.

Chanzo cha Yordani ni mito minne inayobubujika karibu na mlima Hermoni mpakani kwa Israel, Lebanon na Syria.

Mito ya chanzo inaungana katika Israel ya kaskazini.

Yordani hupita eneo la Galilaya inapounda ziwa Genesareti na baada ya kutoka hapo inatelemka kwa kupindapinda mara nyingi hadi Bahari ya Chumvi.

Mdomo wake uko m 400 chini ya usawa wa bahari, hivyo Yordani ni mto wa pekee kabisa duniani.

Kiasi cha maji kwenye sehemu ya kusini ya mto kimepungua sana kwa sababu Israel inavuta sehemu kubwa ya maji kwa ajili ya matumizi ya binadamu katika miji yake.

Bonde la Yordani ni sehemu ya kaskazini ya Bonde la Ufa la Afrika ya Mashariki linaloendelea katika bonde la Araba na kupita Bahari ya Shamu hadi kuonekana tena Eritrea.