Nenda kwa yaliyomo

Watroia

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Watroia wa Mshtarii ni nukta za kibichi kwenye obiti yake

Watroia (kwa Kiingereza: Trojans) ni jina la makundi ya asteroidi zinazozunguka Jua zikitumia obiti ya Mshtarii. Huko hukaa kwa umbali wa pembe 60° na Mshtarii kwenye nukta msawazo ya obiti yake.

Kwenye sehemu zao kani za uvutano wa Mshtarii na Jua zimefikia uwiano na kwa sababu hii asteroidi ndogo pamoja na magimba mengine madogo hayakuvutwa na sayari na kuanguka kwake.

Jina linarejelea mitholojia ya Ugiriki wa Kale; zilitambuliwa na kupokea majina kuanzia mwaka 1906; majina yao yalichaguliwa kutoka idadi ya wahusika wa utenzi wa Iliadi kuhusu vita ya Troia. Watroia wa Mshtarii wakati mwingine hutofautishwa pia kwa Watroia na Wagiriki, kwa sababu kundi linalotangulia sayari limepokea majina ya Wagiriki katika Iliadi, ilhali astroidi zinazofuata zimepokea majina ya Watroia wenyewe katika utenzi huo.

Kuna makadirio kuwa Watroia (na Wagiriki) wa Mshtarii ni zaidi ya milioni moja zenye kipenyo cha kilomita moja na zaidi[1].

Asteroidi zinazozunguka kwenye obiti ya sayari kubwa zimepatikana pia kwingineko katika mfumo wa Jua, yaani kwenye obiti za Neptuni, Uranus, Mirihi na Zuhura. Hizo zote huitwa "Watroia". Mmoja iko pia kwenye obiti ya Dunia.

  1. David C. Jewitt, Chadwick A. Trujillo, Jane X. Luu: Population and Size Distribution of Small Jovian Trojan Asteroids, The Astronomical Journal, Volume 120, Number 2, uk. 1140-147 online hapa