Nenda kwa yaliyomo

Kamusi Hai ya Kiswahili Mtandaoni

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka The Kamusi Project)
Saa ya Kiswahili inayotolewa na mradi wa Kamusi Hai

Kamusi Hai ya Kiswahili Mtandaoni ilikuwa kamusi ya Kiswahili kwenye intaneti. Tangu kuhamishwa kwa mradi mnamo mwaka 2014 haipatikani tena kwa lugha ya Kiswahili ikionyesha lugha nyingine.

Ilijulikana kwa Kiingereza kama "Kamusi Global Online Living Dictionary". Zamani iliitwa "Internet Living Swahili Dictionary" (kifupi: ILSD) au pia "Kamusi Project".

Huu ni mradi ulioanzishwa kwenye Chuo Kikuu cha Yale (Marekani) hasa katika idara yake ya lugha za Kiafrika. Mradi huu unakusanya maneno ya Kiswahili pamoja na maana zake kwa Kiingereza. Unaongozwa na mwanzilishi na mhariri wake, Martin Benjamin.

Kamusi hiyo inapatikana kwa njia ya tovuti yake. Mtumiaji anaweza kuingiza neno lolote la Kiswahili au Kiingereza katika dirisha lake. Kama neno lipo tayari kwenye kamusi atapata tafsiri yake katika maana mbalimbali.

Mradi ulikuwa na matatizo ya kifedha tangu mwanzo wa mwaka 2006 lakini uliweza kuanza upya kwa muda tangu Julai 2006. Mtu yeyote aliyejiandikisha alikaribishwa kuchangia mle.

Matatizo ya Kamusi Hai mwaka 2007 na kuhamia anwani mpya

Mwezi Septemba 2007 tovuti ya Kamusi ilifungwa kwa sababu za matatizo ya ndani ya utawala wa chuo kikuu (tazama: Ukurasa wa majadiliano).

Tangu Novemba 2007 Kamusi Hai imepatikana kwenye anwani ya www.kamusi.org

Mwaka 2013 kamusi hii ilipanuliwa kupokea pia lugha nyingine. Inaeleza sasa shabaha yake kuwa: "Our goal is to provide every word in every language, for free to everyone, everywhere."

Hadi 2014 bado ilikuwa kimsingi kamusi ya Kiswahili yenye maneno zaidi ya 60,000 pamoja na tafsiri yake kwa Kiingereza au kinyume. Kando yake kulikuwa pia na vyanzo vya kamusi za lugha za Kiafrika (kama vile Gusii, Kinyarwanda, Luganda, Songhai), za Kiulaya (kama vile Kifaransa, Kiitalia, Kijerumani) na za Kiasia (Kichina) zenye maneno kati ya makumi na mamia machache.

Viungo vya Nje