Anzwani
Anzwani (Kikomori: Ndzuani, Ndzuwani au Nzwani), ikijulikana kama ni moja kati ya visiwa vinne vya funguvisiwa vya Komoro. Eneo lake ni 424 km² na jumla kuna wakazi 240,000. Ni jimbo la kujitawala ndani ya jamhuri ya Komoro. Mji mkuu unaitwa Mutsamudu.
Historia
[hariri | hariri chanzo]Wakazi asilia walikuwa walowezi kutoka visiwa vya Indonesia ya leo waliofika kwa jahazi katika karne za kale. Mabaki ya makazi ya kale yametambuliwa na wana akiolojia na kukadiriwa kuwa wa karne ya 9. Baadaye wafanyabiashara Waarabu, Waajemi na Waswahili walifika kwenye Komoro na kuingiza visiwa pamoja na Anzwani katika nyavu ya biahara ya Bahari Hindi.
Mnamo mwaka 1500 Usultani wa Anzwani ukaundwa ukaendelea kuwa dola lenye nguvu kwenye Komoro. Mwaka 1816 Sultani Alawi bin Husein aliona hatari ya kushambuliwa na Usultani wa Zanzibar akaomba usaidizi wa Ufaransa. Mwaka 1866 Wafaransa walitangaza Anzwani kuwa eneo lindwa na 1912 wakaitwaa kabisa pamoja na visiwa vyote vya Komoro kama sehemu ya koloni yao ya Madagaska.
Wakati wa uhuru 1975 Anzwani ikajiunga na jamhuri ya Komoro.
Tangu 1997 uhusiano kati ya Anzwani na Komoro ulikuwa na mabadaliko mbalimbali kutokana na mipango ya wanasiasa wale. Mwaka 1997 Anzwani pamoja na Mohéli ikajitenga na Komoro na kutangaza uhuru wake kama Dola la Anzwani (État d’Anjouan) chini ya rais Fundi Abdallah Ibrahim. Kisiwa kiliomba kuunganishwa tena na Ufaransa kama Mayotte lakini serikali ya Ufaransa ilikataa. Mwaka 1999 rais mzee Fundi Abdallah Ibrahim akajiuzulu na serikali iliyomfuata ikapinduliwa mwaka 2001 na kamati ya kijeshi. Chini ya kiongozi wa kijeshi Mohamed Bacar kisiwa kikajiunga tena na Komoro iliyokuwa na katiba na muundo mpya kama "Umoja wa Komoro" tangu 2002. Anzwani sasa ilikuwa jamhuri au jimbo la kujitawala ndani ya Umoja wa Komoro. Bacar alichaguliwa kuwa rais wa Umoja kwa miaka 5 chini ya katiba ya Umoja.
Baada ya mwisho wa kipindi chake mwaka 2007 mwenyekiti wa bunge kama rais mtendaji alikuwa na jukumu ya kuandaa uchaguzi lakini wanajeshi walimpindua na kumrudisha Bacar. Bacar aliandaa uchaguzi ulioshatkiwa kuwa bandia akatangaza ushindi wake kwa 90% za kura. Serikali ya umoja haukutambua tokeo hili. Bacar alijibu kwa kutangaza tena uhuru wa Anzwani.
Serikali ya Komoro iliomba msaada wa Umoja wa Afrika na tarehe 25 Machi 2008 jeshi la Komoro pamoja na kikosi cha Umoja wa Afrika chenye askari kutoka Tansania, Senegal, Sudan na Libya kikisaidiwa na Ufaransa likavamia kisiwa. Bacar alikimbialia Mayotte akaomba kimbilio; Ufaransa umekataa kumkubali kama mkimbizi wa kisiasa lakini vilevile haikumrudisha Komoro kwa hofu anaweza kuuawa.
Tar. 15 Juni 2008 uchaguzi mpya chini ya usimamizi wa serikali ya Komoro ulifanywa. Rais mpya wa Anzwani ni muhandisi Moussa Toybou.
Viungo vya Nje
[hariri | hariri chanzo]- Anjouan.net (tovuti kwa Kiingereza na Kifaransa)
- Tovuti ya Benki Kuu ya Komoro Ilihifadhiwa 29 Aprili 2011 kwenye Wayback Machine.