Uteuzi asilia
Uteuzi asilia ni mchakato unaosababisha viumbehai wenye tabia maalum kuzaa kuliko viumbe wengine na kwa njia hiyo kuongeza idadi ya viumbehai wenye tabia zilezile. Muhimu ni jinsi tabia hizo zinavyolingana vizuri zaidi na mazingira na mabadiliko yake. Kwa kufanya hivyo, hupitisha tabia hizo kwa kizazi kijacho. Kinyume chake, kama kiumbehai ana tabia zisizolingana na mazingira, ataona matatizo, ataishi kwa muda mfupi na hivyo hawezi kuzaa sawa na mwenzake mwenye tabia zinazolingana nayo.
Katika spishi (viumbehai wa aina moja) moja kila kiumbe binafsi ana tabia tofauti kidogo kuliko wenzake. Tabia kadhaa zinaweza kumsaidia kufaulu kuishi na kuzaa kuliko wenzake, kutegemeana na mazingira na mabadiliko yake.
Tabia za aina hii ni, kwa mfano:
- rangi inayomsaidia kiumbehai kujificha mbele ya maadui au kuwasaidia maadui kumtambua haraka zaidi
- uwezo wa kukimbia haraka zaidi, labda pamoja na musuli kubwa zaidi au miguu mirefu zaidi
- mdomo mkubwa wa ndege unaomwezesha kufungua mbegu ngumu
- ustahimilivu kwa magonjwa fulani
- uwezo wa kumeng'enya vyakula tofauti na wenzake
- uwezo wa kuvumilia joto au baridi tofauti na wenzake
Uteuzi asilia hutazamwa kama msingi wa mageuko ya spishi (evolution) ya viumbehai. Dhana hiyo iliitwa pia "survival of the fittest" (kusalia kwa wanaofaa zaidi) [1]. Mtaalamu Charles Darwin alionyesha umuhimu wa mchakato huo akauita "uteuzi asilia" kwa kudokeza unavyolingana na "uteuzi wa binadamu" katika ufugaji ambao watu huteua wanyama wenye tabia zinazotakiwa kama rangi, uwezo wa kuwa na nyama au maziwa mengi, kuvumilia baridi au joto na kadhalika.
Mchakato
[hariri | hariri chanzo]Uteuzi asilia unaelezea kwa nini viumbe hai hubadilika kwa muda kuwa na kuwa na maumbile, uwezo na tabia walizo nazo. Inafanya kazi kama hii:
- Vitu vyote vilivyo hai vina uwezo wa kuzaa kiasi kwamba idadi yao inaweza kuongezeka haraka kupita kiasi.
- Hali halisi idadi ya viumbehai haiongezeki kwa kiwango hicho. Kwa kawaida, idadi inabaki takriban sawa.
- Chakula na rasilimali nyingine vinapatikana kwa kiwango fulani tu. Kwa hivyo, kuna mashindano ya chakula na rasilimali.
- Hakuna viumbehai wawili wanaofanana kabisa katika tabia zao. Kwa hiyo, hawana uwezo sawa ya kustawi na kuzaa.
- Tofauti nyingi za tabia hizo hurithiwa. Wazazi hurithisha tabia kwa watoto kupitia jeni zao.
- Kizazi kijacho kinatoka kutoka hao wanadumu na kuzaa. Kuondolewa kwa wengine husababishwa na kiasi jinsi viumbe binafsi wanavyolingana na mazingira wanamoishi. Baada ya vizazi vingi, idadi ya tabia zinazolingana na mazingira fulani imeongezeka, na tabia zisizolingana zimepungua.[2] Uteuzi asilia ni mchakato wa kuondoa wale wasiofaa. [3]
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- ↑ Darwin, Charles (annotated by James T. Costa). 2009. The annotated Origin: a facsimile of the first edition of On the Origin of Species. Harvard, Cambridge, Mass.
- ↑ Evolution 101: Natural Selection from the Understanding Evolution webpages made by the University of California at Berkeley
- ↑ Mayr, Ernst. 2001. What evolution is. Harvard. p117.
Makala hii kuhusu mambo ya biolojia bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Uteuzi asilia kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |