Mlimbo

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mlimbo wa Senegali (Landolphia heudelotii)
Mlimbo kusi (Viscum capense) juu ya mtishangwe
Mbungo (Saba comorensis)
Mlimbo maridadi (Phragmanthera dschallensis) juu ya mbalibali
Mlimbolimbo (Euphorbia cuneata)
Mlimbolimbo (Cassine aethiopica

Mlimbo, mrimbo na mlimbolimbo ni majina yanayotumika kwa miti, vichaka na mitambaa inayotoa utomvu unaonata (ulimbo au urimbo) na unaoweza kutumiwa ili kuzalisha aina ya mpira. Kwa sababu ya hii spishi kadhaa huitwa mpira pia.

Hapo awali jina mlimbo lilitumika kwa spishi kadhaa za mitambaa kama zile za jenasi Landolphia na Saba. Utomvu wenye kunata wa mimea hii mara nyingi ulitumika kukamata ndege wadogo hadi wa ukubwa wastani. Ni vivyo hivyo kwa spishi fulani za Euphorbia zinazoitwa mlimbolimbo, k.m. E. cuneata. Walakini, ulimbo uliotengenezwa kutoka kwa mlimbolimbo mwingine, Cassine aethiopica, unaandaliwa kutoka kwa majani yake.

Hivi majuzi jina mlimbo limeanza kutumiwa kwa spishi za vimelea-nusu katika familia ya zamani Viscaceae, ambayo sasa imeingizwa ndani ya Santalaceae. Katika spishi hizi utomvu unaonata hauzalishwi katika shina na matawi lakini katika matunda na hautumiki kukamata ndege. Unafanya mbegu kunatika kwenye domo la ndege wanaokula mbegu hizi. Ili kuziondoa ndege hutakiwa kupangusa domo lao kwenye mashina ya miti. Ikiwa mti ni wa spishi sahihi, basi mbegu huota na kimelea hulowea mti huo. Inapendekezwa kutumia mlimbo maridadi kwa vimelea-nusu vya familia inayohusiana Loranthaceae. Mimea hii hutoa idadi kubwa za maua yenye rangi kali.