Mkataba wa Vienna juu ya Mahusiano ya Kidiplomasia

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
     Nchi zilizokubali mkataba      Nchi wanachama wa UM ambazo hazijakubali.

Mkataba wa Vienna juu ya Mahusiano ya Kidiplomasia wa mwaka 1961 ni mkataba wa kimataifa ambao unafafanua mfumo wa uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi huru. Inabainisha haki za wanadiplomasia zinazowawezesha kufanya kazi zao bila hofu ya kulazimishwa au kunyanyaswa na nchi wanapotumwa. Hivyo unaunda msingi wa kisheria wa kinga ya kidiplomasia. Kanuni za mkataba huo zinachukuliwa kuwa msingi mmojawapo katika uhusiano wa kimataifa.

Hadi Oktoba 2018, umeshakubaliwa na nchi 192. [1]

Historia[hariri | hariri chanzo]

Tangu kale mabalozi au wawakilishi rasmi wa nchi au watawala wa kigeni walipewa hadhi maalumu. Hata hivyo, kuna mifano kwamba balozi alikamatwa, kuteswa au hata kuuawa akipeleka ujumbe wake.

Jaribio la kwanza la kuweka kinga ya kidiplomasia katika umbo la kisheria lilitokea katika mapatano ya Mkutano wa Vienna mwaka 1815. Hii ilifuatiwa baadaye na Mkataba kuhusu Maafisa wa Kidiplomasia wa Havana wa mwaka 1928.

Mkataba wa 1961 uliamuliwa baada ya kushauriana katika mikutano ya Umoja wa Mataifa. Tokeo moja maalumu lilikuwa kutambuliwa kwa hali ya kidiplomasia ya nchi ya Mji wa Vatikani (kwa jina la Ukulu mtakatifu).[2]

Miaka miwili baadaye, Umoja wa Mataifa ulipitisha Mkataba wa Vienna juu ya Mahusiano ya Kibalozi (Vienna Convention on Consular Relations).

Muhtasari[hariri | hariri chanzo]

Kwa jumla mkataba unaratibu uhusiano kati ya nchi inayotuma na nchi inayopokea ubalozi na wanadiplomasia wake.

  • Kifungu cha 9: Nchi iliyompokea mwanadiplomasia inaweza kumtangaza wakati wowote na kwa sababu yoyote kuwa mtu asiyetakiwa (persona non grata) . Nchi iliyomtuma inabidi kumrudisha kwao mtu huyu katika kipindi kisicho kirefu, la sivyo mtu huyu anaweza kupoteza kinga yake ya kidiplomasia.
  • Kifungu cha 22: Jengo la ubalozi wa kidiplomasia haliwezi kuingiliwa na nchi inayopokea isipokuwa kwa idhini ya mkuu wa ubalozi huo. Kwa kuongezea, nchi inayopokea lazima ilinde ubalozi kutoka kwa kuingiliwa au uharibifu. Nchi inayopokea hairuhusiwi kamwe kufanya utafiti wa majengo wala kuchukua nyaraka au mali zake. Kifungu cha 30 kinaingiza makao ya kibinafsi ya wanadiplomasia katika ulinzi huo.
  • Kifungu cha 24: kinathibitisha kuwa nyaraka za kidiplomasia haziwezi kushikwa wala kufunguliwa na nchi inayopokea.
  • Kifungu cha 27: Nchi inayopokea lazima iruhusu na kulinda mawasiliano kati ya wanadiplomasia wa ubalozi na nchi iliyowatuma bila makwazo yoyote. Mfuko wa kidiplomasia haupaswi kufunguliwa kamwe, hata kama kuna mashaka ya matumizi mabaya kama magendo. Mjumbe wa kidiplomasia hapaswi kamwe kukamatwa au kuwekwa kizuizini.
  • Kifungu cha 29 Wanadiplomasia hawapaswi kukamatwa kwa namna yoyote au kuwekwa kizuizini. Wana kinga dhidi ya mashtaka ya wenyewe kwa wenyewe au ya jinai, ingawa nchi inayotuma inaweza kuachana na haki hiyo kwa hiari yake chini ya kifungu cha 32.
  • Kifungu cha 31 Kinga cha kidiplomasia hakilindi vitendo vya mwanadiplomasia katika nchi inayopokea akinunua mali, akihusika katika urithi au akiendesha biashara au uchumi nje ya kazi yake rasmi.
  • Kifungu cha 34 kinazungumzia juu ya msamaha wa ushuru wa wanadiplomasia wakati Kifungu cha 36 kinathibitisha kwamba mawakala wa kidiplomasia wamesamehewa ushuru wa forodha.
  • Kifungu cha 37 Wanafamilia wa wanadiplomasia ambao wanaishi katika nchi inayopokea wanastahili kinga nyingi sawa na wanadiplomasia wenyewe.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

 

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]