Kaharabu
Kaharabu (kutoka Kiajemi کهربا kahroba; kwa Kiingereza amber) ni rezini (si utomvu) ya kisukuku cha miti iliyokua miaka milioni iliyopita. Inaweza kufanana na aina za sandarusi lakini kwa jumla umri wake ni mkubwa na ni mgumu zaidi kuliko sandarusi. Aina bora za kaharabu zinajulikana pia kwa jina la kitaalamu la succinit.
Matumizi yake ni hasa kwa mapambo, kama kito, lakini pia kama sehemu ya dawa la mitishamba.
Kaharabu inatokea katika sehemu nyingi za dunia; kiwango kikubwa kabisa duniani (hadi sasa 90%) kimepatikana kutoka pwani za Bahari Baltiki, hasa eneo la Samland[1]
Kaharabu ilitokea katika mazingira ya misitu ya miti yenye rezini husika iliyoendelea kuwa kisukuku katika mchakato wa kufunikwa na maganda manene ya udongo yaliyosababisha shinikizo la tani nyingi na joto kwa miaka elfu na zaidi.
Matumizi na biashara ya kaharabi inajulikana kutokana na utafiti wa kiakiolojia tangu miaka 12,000 hivi.[2] Wagiriki wa Kale waliita kaharaba kwa jina "elektron" wakatambua ya kwamba kipande cha kaharaba baada ya kusuguliwa kinavuta sehemu ndogo za kitambaa au nyuzi kwake. Hapa ni asili ya neno "electric" (umeme) katika lugha za Ulaya.
Katika elimu ya historia ya viumbehai kaharabu ni muhimu kwa sababu mara nyingi vipande vyake vinatunza wadudu na viumbe wengine wadogo waliokaa kwenye miti na kufunikwa ndani ya kitone cha rezini bichi. Wadudu hao wamehifadhiwa hivyo kwa miaka milioni kadhaa na leo wanapatikana kwa uchunguzi wa kitaalamu.
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- ↑ http://gurukul.ucc.american.edu/ted/amber.htm Archived 6 Julai 2012 at the Wayback Machine. Amber Trade and the Environment in the Kaliningrad Oblast. Gurukul.ucc.american.edu. Retrieved on 19 September 2012.
- ↑ I.S. Vassilishin & V.I.Pantschenko: Bernstein in der Ukraine. In: Bernstein – Tränen der Götter. S. 333–340, Bochum 1996.