Nenda kwa yaliyomo

Howani Mwana Howani

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Howani Mwana Howani ni moja kati ya tenzi maarufu za Kiswahili zilizoandikwa na mwandishi mwanamke ajulikanaye kama Zaynab Himid Mohammed, mzaliwa wa Malindi katika kisiwa cha Zanzibar nchini Tanzania. [1]

Utenzi huu ni utenzi unaozungumzia sana kuhusu utamaduni wa Mzanzibari. Utenzi huu umezungumzia mambo mbalimbali katika jamii ya Zanzibar, kuanzia masuala ya dini, hasa ya dini ya Kiislamu, pamoja na mila na desturi za Wazanzibari kwa upande wa mwanamke au mtoto wa kike.

Kwa kiasi kikubwa utenzi huu umemlenga mtoto wa kike na kumfunza ni namna gani aishi katika maisha ya ndoa na jamii itakayokuwa inamzunguka. Mtunzi ameanza kwa kumuambia mwanae ayasikilize maneno yake na kuyatia maanani kwa sababu tayari yeye amekua na ana uwezo wa kutambua jambo lipi baya na lipi zuri na kumsisitiza kuhusu kujiepuesha na dunia huku akimkumbusha mtoto wake huyo wa kike kuhusu safari yake ya kuja duniani ambayo ilianzia katika tumbo la mama yake na mama huyo aliweza kuilea mimba hiyo hadi ikakua na kumzaa mwanae japo katika hali ya tabu sana.

Utenzi huu umeelezea mambo mbalimbali katika maisha ya Mzanzibari kwa kipindi kile, ikigusia suala la huduma za matibabu kuwa hafifu sana kiasi cha kuwatia tabu na misukosuko wanawake hasa linapofika suala mwanamke kuhitaji huduma ya kujifungua.

Mtunzi anaelezea pia kupitia utenzi huu kuhusu mambo ambayo yalikuwa yanafanyika katika kipindi kile, hasa wakati wa mwanamke kupata uchungu na muda mfupi anapojifungua mtoto, pia utenzi unaendelea kuelezea kuhusiana na arobaini ya mtoto inapofanyika mara tu baada ya kuzaliwa.

Kupitia utenzi huu, mtunzi anamgusia mwane kuhusu pepo na kumuusia zaidi kumheshimu mama yake kwani pepo inapatikana chini ya miguu ya mama yake, hivyo azingatie sana katika kuheshimu wanawake.

Utenzi unamalizika kwa mtunzi kujitaja jina lake na sehemu aliyotokea.

Utenzi huu umekusanya jumla ya beti mia tatu tisini na nane.

  1. Mohammed, Zaynab Himid. (2004). Howani mwana Howani : tenzi za Zaynab Himid Mohammed. Dar es Salaam: Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. ISBN 9776911645. OCLC 144607717. {{cite book}}: Check |isbn= value: checksum (help)
Makala hii kuhusu kitabu fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Howani Mwana Howani kama Mwandishi wake, hadithi au matoleo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.