Hanse

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Miji muhimu na njia kuu za biashara ya Hanse
"Adler von Lübeck" ilikuwa manowari ya Hanse 1566-1588 na meli kubwa duniani wakati wake

Hanse (Kijerumani:die Hanse, Kiholanzi: de Hanze,Kisweden: Hansan, ing. Hanseatic League) ilikuwa shirikisho la miji ya biashara katika Ulaya ya Kaskazini na hasa ushirikiano wa wafanyabiashara wa miji hii.

Ushirikiano wa kusaidiana[hariri | hariri chanzo]

Ushirikiano huu ulikuwa mwanzoni na shabaha ya kusaidiana katika ulinzi wa njia za biashara dhidi ya majambazi na maharamia. Wanfanyabiashara wa Hanse waliendelea kupeana msaada pia katika mambo ya biashara yenyewe kwa kupunguza mashindano kati yao wenyewe na dhidi ya biashara isiyokuwa ya Hanse.

Kilele cha Hanse[hariri | hariri chanzo]

Kati karne ya 13 hadi 16 shirikisho la Hanse ilikuwa na nguvu kubwa ya kiuchumi, kisiasa na kijeshi. Msingi wa uwezo wake ulikuwa biashara yenye faida kubwa katika Bahari ya Baltiki. Malighafi kutoka Urusi ya Kaskazini na Skandinavia kama vile ngano, ubao, nta na ngozi ya manyoya zilipelekwa Ulaya ya Kati wakati bidhaa kutoka miji ya Ulaya ziliuzwa kwa faida nzuri. Wafanyabiashara wa Hanse walitawala kabisa biashara kwenye Bahari ya Baltiki hawakuruhusu wengine kuingia hapa. Mji wa Novgorod ulikuwa kituo muhimu cha Hanse katika Urusi.

Kitovu cha Hanse kilikuwa miji ya Ujerumani ya Kaskazini kama vile Lübeck, Hamburg na Danzig. Miji ya Hanse ilikuwa pia na maeneo ya ghala maalumu hadi London na Uholanzi. Wawakilishi wa miji ya Hanse walikutana katika mikutano na kuamua juu ya siasa ya pamoja. Wakati wa karne ya 14 manowari na wanajeshi wa Hanse ziliweza kumshinda hata mfalme wa Denmark aliyelazimishwa kukubali kipaumbele cha Hanse katika Baltiki.

Kurudi nyuma tangu karne ya 16[hariri | hariri chanzo]

Tangu karne ya 15 uwezo wa Hanse ulianza kupungua kwa sababu watawala makabaila wa bara walipanusha maeneo yao. Novgorod iliharibika vitani na kuwa sehemu ya utemi wa Moskva. Miji midogo zaidi ya Hanse ililazimishwa kukubali ukuu wa watawala jirani. Kwa hiyo nguvu ya ushirikiano wa Hanse kwa jumla lipungua polepole. Vita ya miaka 30 (1618-1648) katika Ujerumani iliharibu Hanse ya awali kabisa. Miji iliyobaki ilikutana mara ya mwisho mwaka 1669 lakini nguvu ya zamani haikuweza kurudishwa.

Ndani ya Ujerumani ni miji ya Hamburg na Bremen pekee iliyoweza kutetea uhuru wao wa kisiasa hadi mwaka 1871 ilipojiunga na Wajerumani wengine katika Dola la Ujerumani. Humo ilihifadhi cheo cha miji ya ya kujitawala na hadi leo hii ni Hamburg na Bremen ni majimbo mawili katika Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani.

Miji ya Hanse[hariri | hariri chanzo]

Miji ifuatayo ilikuwa wanachama wa Hanse ya zamani na inaendelea kutumia jina la "mji wa Hanse" hadi leo hii:

Miji ya Hanse ("Hansestadt") leo katika Ujerumani[hariri | hariri chanzo]

Miji ya Hanse ("Hanzestad") leo katika Uholanzi[hariri | hariri chanzo]

Hanse Mpya[hariri | hariri chanzo]

Miji 100 ya Ulaya iliyowahi kuwa wanachama wa Hanse ya Kale imejiunga tena kwa "Hanse mpya" yenye shabaha ya kutunza urithi wa pamoja wa kiutamduni na kukuza utalii kwenye njia za biashara ya zamani.

Kwa jumla Hanse bado inakumbukwa kama ushirikiano ulioweza kuunganisha miji katika nchi mbalimbali.

Jina la Hanse laendelea kutumiwa katika makampuni na taasisi mbalimbali kama vile kampuni ya ndege Lufthansa au klabu ya soka Hansa Rostock.