Gimba la kukaribia dunia

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Njia ya asteroidi 2012 DA14 iliyokaribia dunia mwezi wa Februari 2013
Katikati: Dunia (earth) yetu; duara ya kijani: njia ya satelaiti zinazozunguka dunia; mstari buluu: njia ya asteroidi 2012DA12; mstari wa kijivu: mzingo wa mwezi ukizunguka dunia

Gimba lililopo karibu na dunia (Ing. Near Earth Object) ni gimba la angani kama vile asteroidi, kometi, kimondo linaloweza kukaribia dunia yaani sayari yetu tunapoishi.

Hali halisi magimba haya hufuata obiti wa kuzunguka jua letu linalokaribia obiti wa dunia yetu. Kwa hiyo inatokea ya kwamba asteroidi n.k. inaweza kufikia karibu na dunia yetu na kuna uwezekano wa mgongano. Migongano na vimondo vidogo hutokea kila siku lakini kama gimba ni kubwa kiasi kuna hatari. Tangu wataalamu wa astronomia wametambua hatari hii kuna jitihada za kutambua na kujua magimba haya.

Hatari kutokana na magimba ya kukaribia dunia[hariri | hariri chanzo]

Sehemu kubwa ya magimba yanayokaribia dunia si hatari kwa sababu ni madogo sana yakiwaka mara baada ya kugongana na molekuli za angahewa.

Hadi juzi wataalamu wa Marekani walitazama magimba yenye kipenyo cha mita 100 na zaidi kuwa na hatari.

Lakini tar. 15 Februari 2013 mlipuko wa kimondo kilichokadiriwa kuwa na kipenyo cha mita 17 pekee kilisababisha uharibifu katika eneo la Chelyabinsk nchini Urusi.[1] Kimondo kikubwa kilichoharibu eneo la kilomita za mraba 2000 huko Tunguska mwaka 1908 imekadiriwa kuwa na kipenyo chini ya mita 100. Kama tukio kama Tunguska lingetokea juu ya mji mkubwa lingeua watu wengi sana.

Uharibifu unaoweza kutokea kwa anguko la kimondo au asteroidi hutegemea masi yake, kipenyo, muundo wake na kiwango cha pembe jinsi inayoingia katika angahewa. Sehemu kubwa ya masi ya vimondo inaweza kuwaka hewani, au kimondo kupasuka kilomita nyingi juu ya uso wa dunia. Kadri jinsi kupasuka kunatokea kwenye kimo kubwa au karibu zaidi na uso wa dunia uwezo wa uharibifu unaongezeka.

Asteroidi na vimondo vingi vinaanguka juu ya maeneo pasipo na watu wengi kama baharini (bahari hufunika zaidi ya 2/3 ya uso wa dunia) au porini. Lakini asteroidi kubwa zaidi ni hatari hata kwa bindamu na maisha yote duniani. Asteroidi kubwa inayojulikana kuwa njiani ya kukaribia dunia ni (29075) 1950 DA lenye kipenyo cha kilomita 1.1 ambalo litakaribia dunia kiasi kisichojulikana bado kikamilifu mwaka 2280.

Wataalamu wa biolojia na jiolojia huamini ya kwamba kupotea kwa Dinosauri kulisababishwa na pigo la asteroidi kubwa iliyogonga dunia kwenye eneo la Yucatan, kusababisha kasoko kubwa iliyopeleka vumbi na moshi nyingi kwenye anagahewa na hivyo kuzuia nuru ya jua kufika kwenye uso wa dunia, kupoa kwa ghafla kwa halijoto na kufa kwa mimea na wanyama wengi duniani.

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya Nje[hariri | hariri chanzo]

How to stop an asteroid hitting earth, Guardian Tuesday 30 June 2015

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. Russian meteor strike had force of nuclear bomb; Indian Express 16.02.2013