Nenda kwa yaliyomo

Mmomonyoko

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Erosion)
Bonde la mto wa Colorado/Marekani (Grand Canyon) ni tokeo la mmomonyoko wa maji

Mmomonyoko (kwa Kiingereza erosion) ni hali ya kuvunjika au kumegekamegeka kwa udongo au mwamba kutokana na athira ya upepo, maji, barafu, joto au mwendo wa ardhi. Kazi za binadamu zimekuwa pia sababu muhimu ya mmomonyoko.

Katika mazingira yanayokaliwa na binadamu, na hasa kwa kilimo, mmomonyoko unaleta hatari.

Mmomonyoko wa asili

[hariri | hariri chanzo]

Mmomonyoko ni kati ya nguvu muhimu zinazofinyanga uso wa dunia. Uso wa mabonde na milima ya dunia ni matokeo ya mmomonyoko.

Mmomonyoko wa maji

[hariri | hariri chanzo]
Mmomonyoko kwenye shamba la ngano, Marekani; ni mfano wa kazi ya maji lakini inaonyesha pia athari ya kibinadamu - miti yote imekatwa ili kupata mashamba makubwa

Maji ni kati ya nguvu kuu za mmomonyoko. Mwendo wa maji unasukuma sehemu ndogo za ardhi na kuzipeleka mbali kabisa. Hata vipande vya mwamba vinaweza kukatwa hasa kwa mawe madogo yanayorushwa na maji dhidi ya miamba mikubwa.

Mwendo wa maji ya mito unaweza kuchimba mabonde makubwa. Ukali wake unategemea na kiasi cha maji, kasi yake na aina ya ardhi, kama ina mtelemko mkubwa au kama maji yamepita kwenye ardhi au juu ya miamba. Kama mtelemko ni mkubwa na ardhi ni laini ni rahisi kwa maji kukata bonde refu na kubwa.

Hata mtelemko wa mvua unaleta mmomonyoko. Matone yenyewe hugongagonga sehemu ndogo za ardhi na kuzibeba kidogo jinsi inavyoonekana vizuri baada ya mvua kwenye eneo penye mchanga.

Maji ya mvua yakitelemka milimani yanaweza kubeba udongo mwingi.

Udongo wote pamoja na mawe madogo unaobebwa na maji hutuamishwa mahali fulani kama mashapo. Kwa njia hiyo maji yanaweza kutenganisha aina mbalimbali za mashapo. Kwa kawaida sehemu nzito hutelemka kwanza na kukaa kama mwendo wa maji unaanza kupungua wakati mto umetoka kwenye mtelemko na kuingia eneo la tambarare. Kwa njia hii aina za mashapo kama vile changarawe, mchanga, matamahuluku na udongo kabisa zinapatikana.

Mmomonyoko wa pwani

[hariri | hariri chanzo]
Mmomonyoko kwenye pwani la Ufaransa

Mmomonyoko kwenye mwambao wa bahari au ziwa ni aina ya pekee ya mmomonyoko wa maji. Unatokea hasa kutokana na nguvu ya mawimbi na mikondo. Mikondo ya baharini hubeba muda wote mashapo kwa kuyachukua hapa na kuyatuamisha pale. Kama kiasi kilichochukuliwa kinazidi kiasi kilichotuamishwa mmomonyoko unatokea. Pale panapotuamishwa zaidi kuliko kuchukuliwa fungu linatokea.

Watu wakijenga karibu mno na bahari -kwa mfano mahoteli ya kitalii- wataona mara nyingi ya kwamba nyumba zinachukuliwa na bahari baada ya miaka kadhaa kwa sababu ya mmomonyoko wa pwani wa kawaida.

Mmomonyoko wa upepo

[hariri | hariri chanzo]
Nguzo zilizokatwa na upepo na mchanga katika jangwa la Australia

Upepo unaweza kupuliza chembe ndogo za udongo kama udongo huu ni laini na kavu. Aina hii ya mmomonyoko hutokea hasa pasipo na mimea inayofunika udongo wa juu. Jangwani kiasi kikubwa cha udongo au mchanga huhamishwa na dhoruba.

Upepo ukibeba machanga unaweza kusababisha hata mmomonyoko kwa miamba. Mchanga unarushwa na upepo kwa kasi kubwa dhidi ya mwamba na kuisagasaga.

Mmomonyoko wa barafu

[hariri | hariri chanzo]
Bonde la Yosemite (Marekani) lilikatwa na barafuto miaka milioni 2 iliyopita.

Barafu ikipatikana kama barafuto (ganda nene la barafu inayoanza kutiririka polepole na kujisukuma mbele)ina uwezo wa kuvunja mawe na miamba mikubwa kabisa na kuzisukuma mbali. Barafuto isipoishia baharini inatoa mito inayoendeleza kazi ya mmomonyoko wa maji.

Njia nyingine ya barafu kufinyanga uso wa dunia hutokea pale ambako maji yanaingia kwa mashimo au safu ndogo katika mwamba. Hali ya hewa ikishuka chini ya 0° C majai haya yanaganda na kupanuka hivyo kuvunja mwamba.

Mmomonyoko uliosababishwa na wanadamu

[hariri | hariri chanzo]
Mmomonyoko kwenye Wilaya ya Kondoa.

Mabadiliko kutokana na kazi za kibinadamu yalisababisha mara nyingi mmomonyoko wa ghafla unaoshtusha na kuleta hasara. Mfano ni kukata miti hasa kwenye mitelemko ya milima au kulima milimani. Kazi hizi zinapunguza au kuondoa kabisa funiko la mimea na kuacha udongo bila hifadhi. Maji ya mvua na upepo hazina vizuizi tena.

Matokeo yake ni mafuriko ya ghafla kwa sababu wakati wa mvua maji huteremka haraka na mara moja yakichimba mifereji, kuharibu nyumba, kuua watu na kuondoa ardhi yenye rutuba kwenye mashamba.

Njia nyingine ni mmomonyoko kutokana na kuzidi kwa mifugo. Kazi ya kukanyaga kwa miguu mingi hasa kwenye njia zilezile zinazotumika kuzunguka kati ya boma, maji na sokoni kumeleta uharibifu mwingi. Kwato za mifugo kama ng'ombe, mbuzi, punda na wanyama wengine wafugwao huathiri udongo mara wanapokanyaga mara kwa mara na hivyo hufanya udongo huo kuwa rahisi kusombwa na wakala wa mmomonyoko, kama vile maji, barafu na upepo.

Makala hii kuhusu eneo fulani bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu eneo hilo kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Je, unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuiongezea habari.


Usitaje majina ya madiwani na viongozi au maafisa wengine wa sasa maana wanabadilika haraka mno.