Nenda kwa yaliyomo

Simaki

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Arcturus)
Simaki (Alfa Bootis, Arcturus)
Simaki - Arcturus inaonekana kama nyota pacha katika picha hii iliyopigiwa na darubini ya angani Hubble.Simaki A ni nyota kubwa, Simaki B iko chini yake upande wa kushoto.
Kundinyota Bakari (Bootes)
Mwangaza unaonekana 0.05
Kundi la spektra K0 III
Paralaksi (mas) 88.83 ± 0.54
Mwangaza halisi 36.7
Masi M☉ 1.08
Nusukipenyo R☉ 25.4
Mng’aro L☉ 170
Jotoridi usoni wa nyota (K) 4286
Muda wa mzunguko siku 48
Majina mbadala α Boötis, 16 Boötes, BD+19°2777, GCTP 3242.00, GJ 541, HD 124897, HIP 69673, HR 5340, LHS 48, SAO 100944.


Simaki (Arcturus) katika kundinyota yake ya Bakari – Bootes jinsi inavyoonekana kwa mtazamaji wa Afrika ya Mashariki
Ulinganifu wa ukubwa baina ya Arcturus (Simaki) na Jua; hata hivyo masi halisi ya Simaki inafanana na Jua

Simaki (ing. na lat. Arcturus ark-tu-rus, pia α Alpha Bootis, kifupi Alpha Boo, α Boo) ni nyota angavu zaidi katika kundinyota ya Bakari (Bootes). Ni pia nyota angavu ya nne kwenye anga la usiku. Mwangaza unaoonekana ni -0.05 mag.

Simaki ilijulikana kwa mabaharia Waswahili tangu miaka mingi wakifuata njia yao baharini wakati wa usiku kwa msaada wa nyota. [1]. Walipokea jina hili kutoka Waarabu wanaosema السماك الرامح as-simak ar-rami ambalo linamaanisha “mwenye kushika mkuki aliyeinuliwa juu”[2]. Hapa Waarabu walichagua hadithi kutoka kwa mitholojia ya Kigiriki iliyosimuliwa kuhusu kundinyota ya Bakari ambako masimulizi mbili tofauti zilichanganika. Hadithi ya mchunga au kuendesha ng’ombe ilikuwa msingi wa jina “Bakari” kwa kundinyota lakini “Mshika mkuki” inarejelea hadithi mbadala kuhusu mwindaji anayemfuata Dubu Mkubwa (kundinyota jirani) akishika mkuki wa kuwinda na kusindikizwa na Mbwa Wawindaji. Masimuliza haya hayapatikani kwa Ptolemaio katika kitabu chake cha Almagesti lakini yalishuhudiwa kati ya Wagiriki angalau tangu Hesiodo.

Katika matumizi ya kimataifa Umoja wa Kimataifa wa Astronomia ulichagua jina la Kigiriki "Arcturus" kwa maana "mchunga dubu"[3].

Simaki - Arcturus ina mwangaza unaoonekana wa -0.05 mag na mwangaza halisi ni -0.30. Hivyo no nyota angavu ya nne baada ya Shira (Sirius) (Vmag −1.46), Suheli (Canopus) (Vmag −0.72) na Rijili Kantori (Alpha Centauri) (Vmag −0.27).

Simaki ni nyota ya karibu kiasi ikiwa umbali wake na Dunia ni miaka nuru 36.7 [4].

Masi yake ni M☉ 1.08 na nusukipenyo chake R☉ 25.4 (vizio vya kulinganisha na Jua letu) [5]. Ni nyota jitu jekundu katika kundi la spektra K0 III. Ilhali masi yake inalingana takriban na Jua letu kipenyo chake ni kubwa zaidi mara 25 na sababu yake ni ya kwamba jitu jekundu ni nyota iliyopanuka baada ya kuishia hidrojeni katika kitovu chake; katika hali hii kitovu cha nyota kinajikaza na myeyungano wa hidrojeni unahamia kwenye tabaka za nje za nyota. Hii inasababisha kupanuka kwa nyota na kuongezeka kwa mwangaza wake.

Kuna dalili ya kwamba Simaki ni nyota maradufu lakini hii haijathibitishwa bado. [6]

  1. ling. Knappert 1993
  2. Lane Arabic-English, uk. 1446 Book I-4: " سِمَاك A thing with which a thing is raised, elevated, upraised, or uplifted"; . Allen uk. 100 anatafsiri jina hivi « The Arabs knew Arcturus as Al Simak al Ramih.. the Lofty.« 
  3. Naming Stars, tovuti ya Umoja wa Kimataifa wa Astronomia (Ukia), iliangaliwa Novemba 2017
  4. I. Ramírez; C. Allende Prieto (December 2011) wanataja parsek 11.3, taz. chini
  5. I. Ramírez; C. Allende Prieto (December 2011)
  6. Verhoelst, T.; Bordé, P. J.; Perrin, G.; Decin, L.; et al. (2005). "Is Arcturus a well-understood K giant?", tazama chini

Viungo vya Nje

[hariri | hariri chanzo]
  • Allen, Richard Hinckley: Star-Names and their Meanings; kwa G. E. Stechert New York, Leipzig, London, Paris 1899, ukurasa 59 (online kwenye archive.org)
  • Bond, Howard E.; Schaefer, Gail H.; Gilliland, Ronald L.; Holberg, Jay B.; Mason, Brian D.; Lindenblad, Irving W.; Seitz-Mcleese, Miranda; Arnett, W. David; Demarque, Pierre; Spada, Federico; Young, Patrick A.; Barstow, Martin A.; Burleigh, Matthew R.; Gudehus, Donald (2017). "The Arcturus System and Its Astrophysical Puzzles: Hubble Space Telescope and Ground-based Astrometry". The Astrophysical Journal. 840 (2): 70, online hapa
  • Knappert, Jan: The Swahili Names of Stars, Planets and Constellations; The Indian Ocean Review September 1993 Volume 6 No. 3 September 1993, kurasa 6-7, ISSN 1031-2331
  • Lane, Edward William : An Arabic - English Lexicon by in eight parts – 1872 (Perseus Collection Arabic Materials Digitized Text Version v1.1 of reprint Beirut – Lebanon 1968)

online hapa

  • van Leeuwen, F. (November 2007). "Validation of the new Hipparcos reduction". Astronomy and Astrophysics. 474 (2): 653–64. online hapa
  • I. Ramírez; C. Allende Prieto (December 2011). "Fundamental Parameters and Chemical Composition of Arcturus". The Astrophysical Journal. 743 (2): 135. online hapa
  • Verhoelst, T.; Bordé, P. J.; Perrin, G.; Decin, L.; et al. (2005). "Is Arcturus a well-understood K giant?". Astronomy & Astrophysics. 435: 289. online hapa