Togo ya Kijerumani
Togo ya Kijerumani ilikuwa koloni ya Ujerumani kati ya 1884 na Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia.
Chanzo cha koloni
[hariri | hariri chanzo]Wafanyabiashara Wajerumani kutoka Hamburg na Bremen waliwahi kuwa na ofisi zao hasa huko Aneho kuanzia miaka ya 1870 BK. 1882 kampuni ya Woermann ilianzisha usafiri kwa meli kati ya Hamburg na Afrika na kufanya Togo kituo kimoja.
Wakati ule pwani la Togo ya leo ilikuwa bado eneo huru kati ya Pwani la Dhahabu (Ghana) chini ya Uingereza na eneo la Porto Novo (Benin) chini ya Ufaransa. Lakini Waingereza walisikitika ya kuwa biashara ya watu wa Aneho na Lome ilipanuka na nchi za Ulaya bila kuwaletea mapato ya ushuru kwa sababu bidhaa zilifika nje ya eneo lao.
1884 Mwingereza aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Kitta (Gold Coast - Ghana) alijaribu kutuma wanajeshi Aneho lakini alishindwa. Baada ya tukio hili chifu Mlapa alikuwa tayari kufanya mapatano ya ulinzi na konsuli wa Ujerumani Gustav Nachtigal. Mkataba wa ulinzi ulitiwa sahihi tarehe 6 Julai 1884. Hii ilikuwa mwanzo wa ukoloni wa Ujerumani katika Togo. Katika Septemba mtawala wa Porto Seguro alifanya mkataba wa ulinzi wa pili na mfanyabiashara Mjerumani Randad.
Katika mapatano ya 1885 na 1887 Ufaransa ulikubali utawala wa Kijerumani na mpaka kati ya Togo na Dahomey (Benin). Mkataba wa Helgoland-Zanzibar iliondoa wasiwasi juu ya mipaka na eneo la Kiingereza upande wa magharibi. Mwaka 1914 koloni ilikuwa na eneo la 87,200 km².
Utawala
[hariri | hariri chanzo]Koloni iliongozwa na maafisa waliokuwa mwanzoni na cheo cha kamishna wa Kaisari, halafu nkuu wa nchi, halafu gavana.
- 1884/1885 Freiherr von Soden, Kamishna Mkuu wa Kaisari kwa Togoland
- 1885-1889 Ernst Falkenthal, kamishna, yeye alianzisha kikosi cha polisi ya Togo Novemba 1885.
- 1889-1895 Jesko von Puttkamer, kamishna, tangu 1893 Mkuu wa Nchi (Landeshauptmann)
- 1895-1902 August Köhler, Mkuu wa nchi, tangu 1898 gavana
- 1902-1903 Waldemar Horn , gavana
- 1904-1910 Graf Zech, gavana
- 1910-1912 Edmund Brückner, gavana
- 1912-1914 Herzog Adolf Friedrich zu Mecklenburg, gavana aliyekabidhi koloni mkonono mwa Waingereza na Wafaransa
Upanuzi wa Wajerumani ulianza kwa njia ya mikataba na machifu mbalimbali. Lakini kadiri utawala wao jinsi ilivyoingia zaidi ndani walikuta pia upinzani hasa kwa Wakabya na Wakonkomba hadi mwaka 1898. Kwa ujumla Wajerumani waliweza kupanuka bila jeshi kamili lakini kwa kutumia kikosi chao cha askari 700 wa polisi.
Uchumi
[hariri | hariri chanzo]Wajerumani waliona ya kwamba wenyeji walikuwa na michikichi na kakao. Wajerumani walijenga bandari ya Lome na kuanzisha mashamba makubwa hasa ya michikichi na viwanda vya mawese. Wakajenga reli. Sehemu kubwa ya kazi hizi zilitekelezwa na wenyeji kwa njia ya kazi za kulazimishwa.
Togo ilikuwa kielelezo cha koloni za Ujerumani hasa kwa sababu iliendelea vizuri kiuchumi. Kinyume cha koloni zote nyingine Togo haikupokea misaada kutoka Berlin lakini iliweza kugharamia utawala wake kutokana na mapato yake yenyewe.
Elimu
[hariri | hariri chanzo]Elimu ya shule ilibaki zaidi mkononi mwa misioni ya kikatoliki na kiprotestant. Mnamo mwaka 1910 nchi ilikuwa na shule 196 za kikatoliki na shule 163 za kiprotestant. Wakatoliki walikuwa pia na shule ya ufundi. Kwa ujumla Wamisionari Wajerumani walipendelea lugha za kienyeji kama lugha za mafundisho. Wamisionari wa Shirika la Misioni ya Bremen waliendesha shule zote kwa Kiewe. Serikali ya kikoloni ilikuwa na shule 4 pekee zilizofundisha kwa Kijerumani.
Vita Kuu na mwisho wa koloni ya Kijerumani
[hariri | hariri chanzo]Mwanzoni wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia Waingereza na Wafaransa waliingia Togo kutoka pande zote. Wajerumani walikabidhi Lome kwa Waingereza tar. 8 Agosti 1914 wakarudi nyuma hadi Atakpame. Hapa walijisalimisha tarehe 27 Agosti 1914.
Nchi iligawiwa kati ya Wafaransa na Waingereza chini ya mamlaka ya Shirikisho la Mataifa. Togo ya Kiingereza ilitawaliwa pamoja na Pwani la Dhahabu (Ghana) ikabaki kwa Ghana hata baada ya uhuru.