Nenda kwa yaliyomo

Pijini na krioli

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Pijini na Krioli ni aina za lugha mpya ambazo zinajitokeza katika mazingira ya pekee. Yafuatayo ni maelezo juu ya tofauti na mahusiano kati ya aina hizo mbili katika asili na matumizi. Lugha zote mbili, Pijini na Krioli, ni lingua franka.

Utangulizi

Pijini ni lugha ambayo hutokea pale ambapo wazungumzaji wa lugha tofauti hukutana; hapo, ili kukidhi haja yao ya kuwasiliana, inawalazimu kuibua au kutumia lugha moja ambayo itawawezesha kuelewana katika nyanja za mawasiliano. Pijini huzuka mara nyingi kwa ajili ya biashara hasa.

Pijini kadhaa zinazoonekana leo zilianza wakati wa ukoloni ambako watu waliotawaliwa na mataifa ya Ulaya kwa hiari yao au kwa kulazimishwa walianza kutumia lugha za Kizungu katika maisha ya kila siku.

Pijini ni lugha ya kijuujuu ambapo jamii mbili au zaidi za waongeaji wa lugha tofauti zinazirahisisha ili kuungana katika lugha yenye maneno pamoja na sheria za 'moja kwa moja' kisarufi. Yaani pijini ni matokeo ya mchanganyiko wa lugha ambao muundo na msamiati wake umerahisishwa sana. Lugha ya aina hii basi huwa haizungumzwi na mtu yeyote kama lugha ya kwanza. Izingatiwe pia kuwa kwa kawaida sehemu kubwa ya msamiati pamoja na muundo wa pijini huwa na misingi katika lugha moja tu kati ya lugha zilizoizaa. Mfano wa Pijini ni ule wa Pijini ya Kiingereza au Kiingereza cha Kipijini kinachotumiwa sana Afrika Magharibi.

Wakati unapofika wa watu kujifunza pijini kama lugha mama, 1ugha hiyo wanayojifunza na kuiongea kienyeji hujulikana kama Krioli. Hiyo inatokea wakati jamii ya wazungumzaji inapoanza kutegemea Pijini kwa kila hali na kuipokeza kwa watoto wao. Kwa hiyo Pijini ni lugha ya kijuujuu inayotokana na kuengaengwa na lugha zinazojitegemea baada ya kuazimwa msamiati na miundo rahisi ya msamiati. Lugha ya aina hiyo inapoanza kuimarika na kupata waongeaji wake yenyewe, inakuwa Krio1i.

Mahusiano baina ya lugha za Pijini na lugha za Krioli

Ingawa lugha za Pijini huzitangulia lugha za Krioli katika kuzuka, lugha hizo zote hutokea katika jamii kwa sababu ya mawasiliano ambapo watu wanaozungumza lugha mbalimbali wamekutana na hapana lugha ambayo wanaelewa wote, yaani pale amabapo kila mmoja huzungumza lugha yake ya kipekee.

Lugha za Pijini na Krioli huzuka ili kuwaunganisha watu wanaozungumza lugha mbalimbali ili waweze kuelewana. Lugha kama hizo, ambazo huwaunganisha watu wa makabila au mataifa mbalimbali, huitwa lugha franka, lugha sambazi, lugha za mawasiliano mapana, lugha za mahusiano na maingiliano, lugha unganishi na hata lugha za biashara. Kwa misingi hii basi, lugha za Pijini na Kirioli kadri muda unapozonga hukua na huenda ukawa lingua franka ambazo hutokana na watu wa lugha mbalimbali kukutana na kuwepo kwa hitaji la mawasiliano baina yao. Hata hivyo, hii itatokea tu pale lugha hiyo itapata wazungumzaji wengi na pia msamiati uliokomaa.

Katika lugha hizo mbili, Pijini hupatikana au kuzalika kwanza. Pijini ikiendelea kuwepo na kutumika kama chombo cha mawasiliano huzalisha Krioli. Kwa hiyo, Pijini ndiyo inayokua na kuzaa Krioli. Hivyo basi lugha hizo mbili zina msingi mmoja, ingawa Krioli huwa imekolea na kupiga hatua zaidi kama lugha kamili. Kwa kifupi, Krioli hutokana na Pijini na hapawezi kamwe kuwepo lugha ya Krioli bila kutanguliwa na lugha ya Pijini. Kwa msingi huo, lugha ya Pijini na ile ya Krioli ni kama pande mbili za shilingi moja.

Pijini na Krioli zina uhusiano mkubwa kwa kuwa zote ni lugha kama zilivyo lugha nyingine zozote zile, kwa sababu hutumika katika mawasiliano na pia bila kujali zinapopatikana ulimwenguni. Pijini na Krioli zinazo sifa na sura za kilimwengu ambazo huzifananisha na kuzitofautisha na lugha nyinginezo. Sarufi za lugha hizo mbili zinafanana kote ulimwenguni zinapoongelewa.

Msamiati wa lugha za Pijini na Krioli huwa sawa na hufanana kote zinapoongewa. Pijini hutumika katika shughuli za kijamii kana kwamba ni lugha ya kwanza (asili), msamiati wake huongezeka kwa kiasi kikubwa ili kuweza kutosheleza mahitaji ya kila siku ya mawasiliano ya watumizi wake.

Katika hali kama hizo, lugha hizi huwa si Pijini hasa, bali hugeuka na kuwa Pijini pana. Kama lugha, Pijini pana huendelea kupanuka kwa kubadilika kimuundo kiasi cha kufikia hatua inayoipa hadhi ya kuwa lugha ya Krioli. Ile hatua ya kubadilika Pijini pana hadi kuwa Krioli hutokana na kupatikana kwa kizazi kinachozungumza lugha hiyo kama lugha asili.

Mbali na kupata wazungumzaji asilia, Krioli huwa na msamiati wake mpana na miundo changamano ya kisarufi na maana. Ingawa Krioli ina msamiati mpana kuliko Pijini, la msingi ni kuwa Pijini ndiyo huzaa Krioli.

Lugha za Pijini na Krioli huangaliwa na baadhi ya watu kama zisizo muhimu kutokana na asili zake na pia hali za umaskini ambazo wengi wa wale wanaozizungumza hujikita kwamo. Lugha za Pijini na Krioli zinapatikana hasa katika mataifa ya Ulimwengu wa Tatu.

Kihistoria, lugha za Pijini na Krioli zimekuwa zikibezwa kwa muda mrefu kutokana na ukweli kuwa lugha hizo zimezuka hivi karibuni tu. Kwa hiyo lugha za Pijini na Krioli hazina historia ndefu kwa sababu zilijitokeza kama zao la ukoloni pamoja na watawala na wafanyabiashara walioingiliana na wenyeji.

Pia, msingi wa lugha zote huathiriwa na msamiati kutoka lugha anzishi husika japokuwa huwepo lugha moja inayojitokeza kama msingi wa Pijini husika. Madhara hayo ya Pijini kutawaliwa na lugha moja baina ya lugha iliyokopa msamiati kutoka kwake, hukopwa pia na Krioli inayokuzwa. Ikiwa msingi wa Pijini husika utajikita sana katika lugha moja, kwa mfano lugha ya Kifaransa, Krioli itakayozalika nayo vilevile itakuwa na misingi katika hicho Kifaransa, si katika Kiingereza au Kijerumani.

Tofauti zilizopo baina ya Pijini na Krioli

Ingawa Pijini ndiyo huizaa Krioli, pana tofauti za kutosha zinazopinga hoja kuwa pana mahusiano baina ya lugha ya Pijini na Krioli. Japo lugha za Pijini na Krioli zinao uingiliano mwingi, zipo tofauti za hapa na pale. Tofauti hizo ni kama zifuatavyo:

Lugha ya Pijini huwa haina wazungumzaji asilia na kwa hali hii, Pijini haiwezi kudaiwa na yeyote yule kuwa ni lugha yake ya kwanza ilhali Krioli hupatikana kutokana na kuwepo kwa kizazi kinachozungumza Pijini kama lugha asilia na Pijini hiyo huwa pana kutokana na kuwa na msamiati mpana. Lugha za Pijini huwa hazina wazawa wanaoweza kuzidai kuwa ni lugha za waliowazaa na kuwalea; kinyume na lugha za Krioli zilizo na wazawa asili.

Kiulinganishi, muundo wa lugha za Krioli huwa imara kuliko lugha za Pijini. Hii ni kwa sababu lugha za Krioli huangaliwa kama lugha za kawaida na kwa hivyo zaweza kufanyiwa juhudi za kupangwa. Juhudi hizo za kupangwa kwa lugha za Krioli huzifanya kupewa hadhi ya kutumiwa kama lugha za taifa au hata lugha rasmi.

Pijini huwa ni zao la maingiliano ya watu walio na lugha tofauti lakini ambao wanapenda kuwasiliana. Kutokana na hali hiyo, Pijini huwa na muundo sahili kusudi mawasiliano yaweze kusahilishwa bila ugumu mkubwa. Hivyo basi, lugha za Pijini huwa na muundo wa vokali ulio na vokali tano za msingi ambazo ni a, e, i, o, u. Maumbo ya maneno mara nyingi hujikita katika yale ya lugha-msingi ya Pijini husika. Pijini huwa na msamiati finyu. Muundo wa sentensi za lugha za Pijini huwa sahili na wakati mwingine usio wa sentensi zilizokamilika kisarufi.

Lugha za Pijini huwa na mawanda finyu ya matumizi kwa sababu mara nyingi hujikita katika shughuli iliyosababisha kuzuka kwake. Yaani, Pijini ikiwa imezuka kwa sababu za biashara au za vita, msamiati wake utajikita katika sajili hiyo fulani. Krioli hujitokeza kuwa tofauti kabisa na Pijini katika kitengo cha msamiati na miundo wa kisarufi. Krioli huwa na msamiati mpana na miundo changamano ya kisarufi na maana.

Lugha ya Pijini hutokana na maingiliano ya watu. Hivi ni kusema kuwa Pijini ni zao la hali ya wingilugha katika jamii. Huzuka tu baina ya wazungumzaji wa lugha tofauti wanaohitaji lugha moja ya dharura ya mawasiliano. Krioli ni lugha ambayo wazungumzaji wake hujifunza kama lugha yao ya kwanza tangu wanapozaliwa.

Hadhi ya Krioli huwa juu kuliko ya Pijini ambayo hadhi yake huwa ya kiwango cha chini. Hali hiyo hutokea pale ambapo lugha za Krioli hupangwa na muundo wake wa kisarufi kuimarishwa na kubainishwa. Jambo hilo huchangia hadhi ya lugha za Krioli kupanda na kuwa tofauti na ile ipewayo lugha za Pijini na mawanda ya matumizi ya lugha za Krioli hupanuka ili kukidhi mahitaji ya mawasiliano ya watumiaji wake wote.

Tofauti nyingine baina ya lugha ya Pijini na Krioli ni kuwa, wakati mwingine Pijini hukosa kukua na kuimarika hadi kufikia kiwango cha Krioli. Jambo hilo hutokana na kuwa shughuli iliyopelekea kuzuka kwa Pijini fulani kukosa umuhimu na hivyo kupelekea Pijini husika kudidimia na kujifia mbali. Jambo hilo huwa halitokei katika lugha ya Krioli.

Tazama pia

Marejeo

Makala hii kuhusu mambo ya lugha bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Pijini na krioli kama historia yake, uenezi au maendeleo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.