Nenda kwa yaliyomo

Zenji Flava

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Zenji Flava ni jina maarufu la muziki wa hip hop kutoka Zanzibar. Aina hii ya muziki ilianza mwanzoni mwa miaka ya 1990. Jina linajengwa na nenomsimu la Kiunguja maarufu kama Zenji, yaani "Zanzibar", na flava, ambayo imetokana na mvurugo wa neno la Kiingereza la "flavour", hivyo kwa pamoja inaleta maana ya "ladha ya Zanzibari".

Muziki huu, kama Bongo Flava, ambayo awali ilitumika hata katika kutaja hip hop ya Tanzania bara (kwa sasa ni tofauti kimaana kwa vile hip hop ni hip hop na Bongo Flava ni kitu kingine tofauti), Zenji Flava kikawaida huimbwa pia kwa Kiswahili. Utofauti wa vijiaina hivi ni kuwa Zanzibari hip hop ina athira kidogo ya taarab, na kuna ladha kwa mbali ya muziki wa Kiarabu na Kihindi kwa mbali. Waimbaji wa rap/hip hop ya Zenji wa awali kabisa alikuwa Coo Para na Cool Muza tangu mwaka 1996. Harakati hizi ziliendelea hadi hapo 2001 Cool Para alipobahatika kwenda kufanya onesho la huko Ulaya - Ujerumani na Uholanzi.

Muziki huu miaka ya 1990, hasa kulikuwa na kina Struggling Islanders na kina DJ Saleh wa Zanzibar Televisheni. Si kama muziki ulioungwa mkono sana katika miaka ya 1990, lakini akina Cool Para walikuwa wanatumia kanda za Saleh Jabri ambaye alitumia ala ya O.P.P na Ice Ice Baby ya Vanilla Ice. Ilikuwa kawaida kupanda stejini na kuanza kurap nyimbo hizo kwa Kiswahili na ilileta hamasa kubwa sana kwa wakati huo, japo si wengi waliojaribu kujihusisha na muziki huu.

Kuanzia miaka ya 2000, ndiyo hasa kukaanza kutokea wasanii wengine wa muziki huu kama vile akina Ali Haji,[1] Offside Trick, 2 Berry wametengana lakini mmoja alijiita Berry Black na mwengine Berry White, Wazenji Kijiwe na Shaka Zulu. Wengine waliokuwa kama kundi ni pamoja na Brooklyn, Four Nature, Jumbo Camp, Queen Love, na K Jam. Kipindi hiki cha 2000 ndiyo hasa Zenji Flava imepamba moto kukiwa na wasanii vijana walioboresha na kuifanya kuwa ya kisasa zaidi. Cool Para aliweza kuchanganya taarab na hip hop kuwa kitu kimoja kuipa jina la taarap. Hata kuna wimbo alifanya na East Africa Melody mwaka 2000 uliitwa "Loo Umezoea". Awali katika miaka ya 1990, hata ukifanya hip hop vile inavyotakikana, yaani, kutetea wanyonge, kukemea mambo mabaya kuhusu serikali ilikuwa unaishia pabaya. Huenda hili lilipelekea muziki huu uchelewe kukua kwa kasi huko Zenji.

Haukuungwa mkono sana katika miaka ya 1990, ila kulikuwa na DJ Saleh ambaye alithubutu kupiga muziki huu kwa hali na mali katika redio na TV za Zenji kwa kiasi kikubwa. DJ Saleh nae alikuwa mmoja kati ya wanarap wa awali wa Zenji. Iko tofauti kidogo na Tanzania bara wale waliokuwa wanaunga mkono muziki huu ilikuwa Ma-DJ wa redio kama vile Taji Liundi na Mike Mhagama wote kutoka Radio One. Halafu baadaye harakati za mkono kwa mkono kutoka kwa Sebastian Maganga wa Radio Uhuru. Lakini DJ Saleh yeye alikuwa anafanya rap na kipindi katika TV na redio. Hii ilitoa mwangaza kwa vijana wa Zenji kuweza kusikia muziki huu. Japokuwa haikuwa rahisi kupiga nyimbo zenye kukemea serikali. Akina "Struggling Islanders" wao waliimba sana harakati za mtu mweusi na walilenga hasa watu waijue historia yao. Muziki wa starehe haukuwa na nafasi sana kwa hawa jamaa. Struggling Islanders lilianzishwa na Cool Para na Cool Muza mwaka 1997.

  1. History of Zenji Flava Archived Julai 18, 2011, at the Wayback Machine


Makala hii kuhusu maeneo ya Tanzania bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Zenji Flava kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.