Württemberg
Württemberg ilikuwa dola ndani ya Ujerumani katika maumbo yake mbalimbali ya kisiasa. Mwanzoni kama sehemu ya Dola Takatifu la Kiroma, kisha ya Shirikisho la Ujerumani, halafu ya Dola ya Ujerumani.
Tangu mwaka 1952 imekuwa sehemu ya jimbo jipya la Baden-Württemberg lililopo kusini-magharibi mwa Ujerumani likipakana na Ufaransa na Uswisi.
Mji mkuu wake na makao ya watawala wake wa kikabaila ulikuwa Stuttgart .
Historia
[hariri | hariri chanzo]Nchi iliundwa mnamo karne ya 11 kutokana na maeneo ya makabaila wa familia ya Württemberg kando ya mto Neckar, tawimto la Rhine.
Tangu mwaka 1495 watawala wake walipewa cheo cha mwinyi (duke). Katika mvurugo mwanzo wa karne ya 19 baada ya uvamizi wa Ufaransa katika Ujerumani chini ya Napoleon, mtawala wa Württemberg alipandishwa cheo tena na kupewa haki ya kumchagua Kaizari. Mwaka 1806, baada ya mwisho wa Dola Takatifu la Kiroma, alipewa hadhi ya mfalme.
Ufalme wa Württemberg ulikuwa nchi ya kujitegemea kabisa na mwanachama wa Shirikisho la Ujerumani hadi mwaka 1871. Mwaka ule ilishiriki katika umoja wa Ujerumani na kujiunga na Dola la Ujerumani. Sawa na dola lingine la kusini, Bavaria, Württemberg ilibaki na haki za pekee, kama jeshi lake, reli yake na posta yake.
Mapinduzi ya mwaka 1918 baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia yalimpindua mfalme na kufanya Württemberg kuwa jamhuri kama sehemu nyingine za Ujerumani. Haki za pekee ndani ya taifa kubwa zilikwisha ilhali Württemberg iliendelea kama jimbo la kujitawala ndani ya Ujerumani.
Baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, washindi waligawa jimbo baina ya utawala wa Marekani na Ufaransa.
Tangu kuanzishwa kwa Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani maeneo hayo yaliungana tena na pamoja na jimbo la Baden jimbo jipya la Baden-Württemberg lilianzishwa.
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- Wurtemberg, katika Encyclopedia 1902
Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Württemberg kama enzi zake au matokeo yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |