Manowari
Manowari ni meli yenye silaha iliyojengwa kwa kusudi la kuitumia katika vita.
Asili ya neno "manowari" ni Kiingereza cha karne za 16 hadi 19 BK ambapo "man-of-war" au kifupi chake "man-o'-war" (mtu wa vita) linataja hasa jahazi kubwa la vita lakini pia jahazi au meli yoyote ya kivita.
Muundo wa manowari
[hariri | hariri chanzo]Muundo wake huwa ni tofauti na meli zinazokusudiwa kubeba mizigo au watu.
Tabia muhimu za manowari ni kasi na kinga pamoja na uwezo wa kubeba silaha. Hasa tabia za kasi na kinga zimeshindana mara nyingi katika historia ya ujenzi ya meli hizi.
Manowari inaweza kukingwa dhidi ya silaha kwa kuweka mabamba mazito ya metali nje ya bodi yake au kujenga bodi yake moja kwa moja kwa kutumia metali nzito. Ila tu kinga inaongeza uzito na kupunguza mkasi; kwa hiyo manowari yenye kinga mzuri inaweza kuwa lengo la silaha za adui kwa sababu mwendo wake ni polepole mno.
Manowari yenye kasi kubwa inahitaji kupunguza uzito wake hivyo haiwezi kujikinga vile. Ikipigwa na silaha za adui inazama haraka lakini faida yake ni mwendo unaoepukana na kupigwa.
Mara nyingi katika historia kutokea kwa aina mpya ya kinga kulibatilisha silaha za mashambulio yaliyokuwepo. Lakini baadaye silaha mpya ziliweza kutoboa kinga mpya na kulibatilisha. Hadi sasa imekuwa mashindano ya kurudiarudia.
Silaha za manowari
[hariri | hariri chanzo]Zamani manowari zilibeba hasa wanajeshi wenye silaha kama pinde na mishale na pia vifaa vya kurusha mawe au vyombo vya moto kwa jahazi nyingine.
Mara nyingi ilishambulia kwa kukaribia boti au jahazi nyingine ili askari zake waliweza kurukia meli ile na kuiteka sawa na mapigano kwenye nchi kavu.
Njia nyingine ilikuwa kumgonga mwadui na kwa kusudi hii omo la manowari liliimarishwa kwa metali lililengwa kwa upande wa pembeni ya jahazi ya adui kwa shabaha ya kuutoboa na kuuvunja ili izame.
Tangu kupatikana kwa baruti manowari zilibeba mizinga.
Katika karne ya 20 manowari zilianza kubeba makombora kama silaha za kulenga mbali.
Historia
[hariri | hariri chanzo]Manowari zimepatikana tangu zamani za jeshi la Babiloni au Misri hadi leo.
Asili ya manowari ni katika maboti madogo yaliyoendeshwa kwa makafi. Maboti makubwa yaliweza kuendeshwa na watu wengi hivyo kupata kasi nzuri. Zaidi ya hayo yaliweza hata kubeba askari wanaorusha mishale au mikuki au kurukia maboti mengine.
Manowari ya pekee imejulikana kwa jeshi la Wamisri, Wababiloni au Wachina tangu milenia ya 1 KK. Zilikuwa manchani zilizoendeshwa kwa makasia pamoja na tanga. Katika bahari isiyo na dhoruba kali makafi yalitumiwa kwenye manowari hadi karne ya 18 BK.
Kwa muda mrefu manowari kubwa zilijengwa kwa muundo wa jahazi. Mataifa yaliyofaulu hasa walikuwa kwanza Wachina baadaye Wareno.
Majahazi hayo yalikuwa ya ubao.
Tangu karne ya 19 BK injini mpya za mvuke ziliruhusu kuongeza kinga kwa kutumia maganda ya metali juu ya ubao. Baadaye meli zote zilijengwa kwa chuma. Manowari aina ya "Dreadnought" ilipatikana tangu mwaka 1906 ikikingwa kwa chuma kinene na kuwa pia na bunduki kubwa.
Karne ya 20 iliona aina mpya za manowari:
- nyambizi (au sabmarini - chombo cha bahari kinachosafiri chini ya mawimbi)
- manowari ndege zinazobeba ndege za kivita
- Hovercraft: boti kubwa linalokaa takriban mita moja juu ya maji ikilala kwenye mto wa hewa inayopulizwa chini - inatembea baharini na pia kwenye nchi kavu tambarare pasipo na korongo au milima.
Makala hii kuhusu mambo ya siasa bado ni mbegu. Unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuongezea habari. |