Pearl Harbor

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mahali pa Pearl Harbor kwenye funguvisiwa ya Hawaii
Pearl Harbor wakati wa mashambulio ya Kijapani ya 7 Desemba 1941; picha ilichukuliwa kutoka ndege ya Kijapani.

Pearl Harbor (Kiing. "bandari ya lulu"; Kihawaii: Pu'uloa) ni bandari ya kijeshi ya Marekani kwenye kisiwa cha Oahu katika jimbo la visiwani la Hawaii (Marekani).

Kituo hiki cha kijeshi kipo ndani ya kidaka iliyo bandari asilia ambako meli na manowari zinakaa salama wakati wa dhoruba. Katikati ya kidaka kuna kisiwa kinachoitwa Ford Island ambayo ni kitovu cha kituo cha kijeshi. Tangu Marekani kutwaa Hawaii na vita ya Marekani dhidi Hispania mwaka 1898 bandari hii ilikuwa makao makuu ya kundi la manowari za Marekani katika Bahari Pasifiki.

Pearl Harbor ilikuwa maarufu kutokana na mashambulizi ya ghafla ya Japani dhidi ya manowari za Marekani yaliyotokea hapa tar. 7 Desemba 1941. Hatua hii ilisababisha Marekani kuingia katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia na kujiunga rasmi na mataifa ya ushirikiano.

Katika siku kabla ya 7 Desemba wanamaji wa Japani walifaulu kukaribia funguvisiwa na kundi la manowari pamoja na manowari ndege 6. Eropleni 350 kutoka manowari ndege hizi zilishambulia kituo cha Pearl Harbor katika masaa ya mapema ya 7 Desemba zikafaulu kuzamisha manowari 9 na kuleta uharibifu mkubwa kwa manowari 21 nyingine, tatu kati hizi hazikuweza kutengenezwa tena. Wamarekani 2350 waliuawa. Pia ndege nyingi za kijeshi za kimarekani ziliangamizwa.

Shabaha ya shambulio la Japani ilikuwa kuharibu uwezo wa manowari za Marekani kuingilia katika upanuzi wa mamlaka ya Japani katika Pasifiki hasa kwenye maeneo chini ya utawala wa Uingereza, Uholanzi, Ufaransa na China. Lakini shambulio halikugusa kituo cha nyambizi, akiba za fueli, karahana za kijeshi na ofisi za viongozi vya jeshi. Pia manowari ndege zilizokuwa sehemu ya kundi ya Pearl Harbor hazikuharibiwa kwa sababu zote tatu hazikuwepo Hawaii wakati wa shambulio.

Kwa hiyo uwezo wa Pearl Harbor kuhudumia kundi la manowari haukuharibiwa na baadaye Marekani ilitumia kituo hiki pamoja na visiwa vya Hawaii kama msingi wa vita yake dhidi Japani.

Viungo vya Nje[hariri | hariri chanzo]

Makala hii kuhusu eneo fulani bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu eneo hilo kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Je, unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuiongezea habari.


Usitaje majina ya madiwani na viongozi au maafisa wengine wa sasa maana wanabadilika haraka mno.