Nenda kwa yaliyomo

Wangwa

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Nyangwa)
Makala hii kuhusu "Wangwa" inatumia neno au maneno ambayo si ya kawaida; matumizi yake ni jaribio kwa jambo linalotajwa.
Wasomaji wanaombwa kuchangia mawazo yao.

Kamusi za Kiswahili ama zinatofautiana kuhusu matumizi ya neno hili au hazieleweki au hazina neno kwa jambo linalojadiliwa.

Wangwa wa Kivalina (upande wa kushoto) huko Alaska, Marekani umeunganika na bahari.

Wangwa (ing. lagoon) ni eneo la maji lililotengwa na bahari lakini kuna njia kwa maji kuingia na kutoka. Kama wangwa uko kwenye pwani na mito inaishia humo maji yake ni mchanganyiko wa maji ya chumvi na maji matamu. Kama wangwa haupokei maji ya mto na pia kuna njia nyembamba upande wa bahari tu inawezekana maji yake huwa na kiwango cha juu cha chumvi kutokana na uvukizaji.

Nyangwa zinaweza kutokea pale ambapo maji karibu na ufukoni hayana kina kirefu na mtelemko chini ya maji si mkali. Sharti lingine ni kwamba mawimbi ya kugonga ufukoni yasiwe makubwa mno.

Kawaida wangwa unatenganishwa na bahari kwa ulimi mwembamba wa nchi kavu uliojengwa na mkondo wa bahari uliobeba mchanga au matope, au na matope ya mto unaoishia humo. Katika bahari za tropiki matumbawe yanaweza kujenga ulimi huo.

Kuna pia nyangwa ndani ya atolli (kisiwa chenye umbo la mviringo) iliyojengwa na matumbawe na hapo pasipo na mito maji yake ni ya chumvi tu.

Nyangwa ni muhimu katika ekolojia ya bahari. Kuna samaki wengi kwa sababu spishi nyingi zinatega mayai katika nyangwa kwa sababu kina kifupi kinapunguza hatari kwa samaki changa ya kushambuliwa mara moja na samaki wakubwa. Ufuko wa nyangwa za tropiki unajaa mara nyingi miti ya mikoko na kati ya mizizi ya mikoko ni mahali pa spishi nyingi sana za viumbehai.