Nimefulia

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
“Nimefulia”
“Nimefulia” cover
Kava la Nimefulia
Single ya Benjamin wa Mambo Jambo akiwa na A.T
Imetolewa 26 Juni, 2010
Muundo Upakuzi wa mtandaoni
Imerekodiwa 2010
Aina Dancehall, ragga, Bongo Flava
Urefu 5:47
Studio Mzuka Records
Mtunzi Benjamini wa Mambo Jambo
Mtayarishaji Benjamini wa Mambo Jambo
Mwenendo wa single za Benjamin wa Mambo Jambo akiwa na A.T
"Nimefulia"
(2010)
"My Friend
(2011)

"Nimefulia" ni jina la wimbo uliotoka 26 Juni, 2010 kutungwa na kuimbwa na msanii wa muziki wa kizazi kipya kutoka nchini Tanzania, Benjamin wa Mambo Jambo akiwa na A.T. Wimbo umetayarishwa na Benjamin mwenyewe kupitia studio yake ya Mzuka Records ya Mbezi Beach, Dar es Salaam. Video ya wimbo huu, umeongozwa na Adam Juma wa Visual Lab. Ndani wanaonekana wakiwa mahali pa kuoshea magari kienyeji baada ya kufukuzwa kazi bila maelezo ya maana. Ili kujikimu kimaisha, anaamua kuingia mtaani na kufanya kazi mbalimbali ili aweze kumudu gharama za maisha.

Historia[hariri | hariri chanzo]

Wazo la wimbo[hariri | hariri chanzo]

Picha ya kiwambo ya Nimefulia ikimuonesha A.T kushoto na Benja mkono wa kulia katika seti ya wimbo huu.

Wazo la kutunga wimbo huu alilipata akiwa garini na mtayarishaji wake maarufu Miikka Mwamba huko nchini Finland mnamo kwa wa 2009. Wakiwa safarini nchini humo, Benja anapata wazo la kutunga wimbo huu kwa melodi tu bila maneno. Wazo limekuja baada kusikia wimbo mmoja uliokuwa unapiga katika gari hilo. Halkadhalika akitazama mandhari halisi ya nchini Finland na Tanzania tofauti yake ni ardhi na mbingu. Akaona Bongo kama tumefulia. Isitoshe wakati huo kundi zima la Ze Comedy walikuwa na kipengele cha "Umefulia" na msemo huu katika mwaka wa 2008/2009 ulitamba sana. Akaona heri atie katika mashairi ili kuleta ladha zaidi.

Wazo hili Miika aliunga mkono kwa asilimia mia moja. Na hasa ilitakiwa wimbo huu urekodiwe Finland, ila tu ratiba zilibana kwa wawili hawa ikaishia kuja kufanywa nchini Tanzania. Vilevile hii ndiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa Benjamin kwenda barani Ulaya. Akiwa Tanzania, alitengeneza mdundo wake na kutia sauti pekee.

Aliendelea kusikiliza mwenyewe hadi hapo alipompata A.T na kutia sauti yake katika kiitikio. Awali Benja alikataa kumruhusu A.T atie sauti zake katika wimbo wake, hasa kwa kufuatia A.T alikuwa anaimba miduara na yeye Benjamin anaimba ragga. Kukutana kwa wawili hawa kulisababishwa na Adam Juma aliyemtambulisha A.T kwa Benjamin. Kilichopelekea Benjamin kumkubali A.T ni baada ya kumfanyia wimbo wake wa Nipigie alioimshirikisha Stara Thomas. Kuanzia hapo, Benjamin ikabidi atulie na akubali matokeo ya kumshirikisha A.T katika kibwagizo.

Wimbo wote umetungwa na Benjamin peke yake. Hata mistari ya kwanza katika wimbo huu "Wamemfunga kaka yangu mwanangu muziki" ni sehemu ya Benja ila alimpasia A.T baada ya kushirikishwa. Wazo kuu lilikuwa kuleta ladha mbili za muziki tofauti ili kufanya iwe burudani ya kipekee.

Maudhui na uchambuzi[hariri | hariri chanzo]

Sampuli ya Nimefulia kama jinsi inavyoimbwa na Benja na A.T.

Muundo wa mashairi umefuata mitindo yote miwili ya kimapokeo na kimambo leo. Mfano mstari wa kwanza unasema "Wamemfunga kaka yangu mwanamuziki, niliyekuwa namtegemea anitoe kwenye dhiki". Upande A "ki" na upande B kuna "ki", yaani mwanamuziki na dhiki. Huo ni muundo au mtindo wa kimapokeo. Hajaishia hapo, anasema "aliyekuwa anazunguka kutafuta riziki, tupate kula nisome pia niondokane na dhiki". Maneno haya au ufunguzi huo unaweza kuwa aidha wa kisiasa au lengo katika maisha ya kweli. Benjamin anajibu "siwezi kukubali, siwezi kukubali" huku A.T akijibu "yale yalitokea huenda yamekusudiwa" huku Benjamin akirudia maneno sawa na ya awali. Matukio haya, yanaweza kuwa ya yametendwa na wanadamu aidha kwa makusudi au bahati mbaya. A.T na Benjamin wanaona maisha magumu huku watu akijilimbikizia mali huku wengine wakiishi maisha ya tabu. A.T anajibu baada ya Benjamin "siwezi kukubali" akimaanisha hali hiyo, kwa "zama za mabepari naona zinajirudia" huku akimaliza na "nimefulia".

Usaliti[hariri | hariri chanzo]

Wimbo unaonesha usaliti katika jamii iliyotuzunguka. Kabla ya maisha ya Benja kwenda kombo, alikuwa na marafiki wengi, lakini punde upepo umeenda kusi, wote wamekimbia. Hasa kwa kufuatia hana cha kuwapa katika maisha yake. Ananuka dhiki. Anasema hivi: "Wale masela wangu wa karibu hivi sasa siwaoni". Halafu "waliojifanya wananipenda kwa sana sasa nao siwaoni" hapa anamaanisha wapenzi zake. Hata wale waliokuwa wanatumia ote nao hawaonekani.

Ufundi na lugha[hariri | hariri chanzo]

Katika kusukumia maneno, anachanganya maneno ya Kiingereza na Kiswahili. Mfano kwenye kutaja waliomsaliti anasisitiza kwa Kiingereza: So damn haters kaitaja baada ya "waliojifanya wananipenda kwa sana sasa nao siwaoni". "I'm a broke one" kaitaja baada ya "Hata wale waliokuwa wanatumia ote nao hawaonekani".

Siasa, ufisadi na ukosoaji[hariri | hariri chanzo]

Katika wimbo anakosoa tabia za wanasiasa katika kutoa ahadi ambazo hawawezi kuzitimiza. Ben anachukizwa na utaratibu huo. Mfano anasema "Uliniahidi utajenga barabara za juu na chini, kila kitu utaboresha elimu na mambo yote" lakini "hadi sasa huna lolote ulilofanya umesepaaa". Ben analia tabia za baadhi ya viongozi kujilimbikizia mimali. Anarejea katika wimbo kwa kusema "mgodi wenyewe umetaifishwa" halafu "shamba la bibi yako limebinafsishwa" tena "soko la babu yako nalo limebinafsishwa". Mara nyingi hawa wazabuni na waseti ni wenyewe vigogo wa serikali. Matukio haya yalikuwa ya kawaida kwa karibia tawala zote zilizopita. Katika wimbo anasikitikia hali hiyo kwa majonzi jinsi ubadhilifu na dhulma dhidi ya wanyonge kutoka kwa vigogo wa serikalini.

Tazama[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya Nje[hariri | hariri chanzo]

Video katika YouTube