Kura juu ya katiba mpya ya Kenya (2005)
Kura ya maoni juu ya katiba mpya ya Kenya ilipigwa tarehe 21 Novemba 2005. Asilimia 58 ya Wakenya waliopiga kura waliikataa.
Rais wa Kenya na baadhi ya mawaziri walipiga kampeni kutaka Wakenya waiunge mkono katiba hiyo. Kundi lililokuwa likiiunga mkono katiba mpya lilikuwa likiwakilishwa na alama ya ndizi na kundi lililokuwa likiipinga lilitumia alama ya machungwa.
Ingawa watu wanane walikufa katika fujo zilizohusiana na kura hiyo, kwa ujumla zoezi hili lilifanyika kwa amani. Suala ambalo lilikuwa likijadiliwa sana ni kiasi cha madaraka ambacho rais anapaswa kupewa. Katiba mpya ilikuwa impe madakaraka makubwa sana rais wa Kenya wakati ambapo wanaoipinga katiba hiyo walitaka kuwe na Waziri Mkuu ambaye atagawana madaraka na Rais.
Suala la umiliki wa ardhi nalo lilipewa kipaumbele kwenye mjadala wa kufaa au kutofaa kwa katiba hiyo. Katiba mpya ilikuwa ikiweka vikwazo kwa watu wasio Wakenya kumiliki ardhi, ilikuwa iruhusu wanawake kumiliki ardhi (kwa kurithi), na ilitaka iundwe tume ya ardhi ambayo ingekuwa na wajibu wa kugawa ardhi na kuondoa uwezekano wa viongozi wa serikali kupeana ardhi. Tume hii pia ingekuwa ndio msikilizaji mkuu wa kesi za ardhi na ingekuwa na jukumu la kurudisha ardhi kwa makundi na watu binafsi ambao waliipoteza miaka iliyopita.