George Moseti Anyona

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
George Anyona

George Moseti Anyona (1945-2003) alikuwa mwanasiasa wa Kenya. Alikuwa mbunge akiwakilisha Eneo Bunge la Kitutu Masaba. Anajulikana kwa ujasiri wake wa kutetea mfumo wa vyama vingi nchini wakati kulikuwa na chama kimoja tu, KANU

Maisha ya awali[hariri | hariri chanzo]

Anyona alizaliwa mnamo 1945 katika Kijiji cha Tombe, Kitutu Masaba, Wilaya ya Kisii Kati iliyokuwa Mkoani Nyanza nchini Kenya.

Alihudhuria masomo katika Shule ya Msingi ya Tombe na Sengera. Hatimaye alijiunga na Shule ya Upili ya Alliance. Kutoka huko alienda Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda ambapo alisomea Sayansi ya Siasa, Kiingereza, Biashara na Historia.

Siasa[hariri | hariri chanzo]

Anyona alishinda kiti cha ubunge cha Kitutu East mwaka ule ule aliojitosa kwenye ulingo wa siasa. Shida zake za Kisiasa zilianza mnamo 1977 wakati alitiwa kifungoni bila kuhukumiwa kufuatia amri ya rais Jomo Kenyatta. Alifunguliwa mwaka mmoja baadaye na rais Daniel arap Moi punde alipochukua madaraka baada ya kifo cha Jomo Kenyatta.

Mnamo mwaka wa 1982 Anyona alijikuta matatani tena, wakati huu akitiwa gerezani tena bila hukumu pamoja na mwendani wake wa muda Jaramogi Oginga Odinga, kwa kujaribu kuunda chama cha kisiasa Kenya African Social Alliance (KASA) kupinga chama tawala cha KANU.[1].

Punde baada ya kutiwa gerezani, serikali ya Kenya ilinusa hatari ambayo wangeisababisha na ikaharakisha kuziiba mianya katika Katiba. Matokeo ni kupitishwa kwa kifungo kilichoifanya Kenya kuwa na Mfumo wa Chama Kimoja mwaka huo huo[2].

Anyona aliachiliwa mnamo 1984 na tangu hapo akajiondoa kutoka siasa kwa muda. Marejeo yake katika ulingo huo yaliyokuwa yakitarajiwa na wengi yalitimia mnamo 1990 wakati wa kupiigania mfumo wa vyama vingi nchini Kenya. Kwa wakenya wengi , hivi vilikuwa vita ambavyo Anyona na Jaramogi hawangelenga kwa vile ni wao walivianzisha mnamo 1982.

Punde baada ya kurudi katika siasa, Anyona alitiwa mbaroni tena katika hoteli ya Nairobi pamoja na wengine kama vile Profesa Edward Oyugi, Isiah Ngotho Kariuki na Augustus Njeru Kathangu. Walishtakiwa kwa kosa la kupanga mapinduzi dhidi ya serikali.

Walihukumiwa miaka saba gerezani baada ya kesi kali[3]. Kulingana na stakabadhi zilizokabidiwa wakati wa Kesi, ilidaiwa kuwa Anyona hata alikuwa ameunda Baraza la mawazili la ‘’kivuli’’ ili kuingia madarakani baada ya upinduzi. Baadaye Waziri katika Ofisi ya Rais John Keen alidhibitisha kuwa stakabadhi hizo zilikuwa njama ya serikali kumnyamazisha Anyona.

Baada ya kusikizwa kwa malalamiko ya kesi yao wane hao waliachiliwa kwa dhamana mnamo 1992. Hatimaye waliachiliwa huru baada ya serikali kuamua kutoipinga malalamiko ya kesi yao.

Mfumo wa Vyama Vingi[hariri | hariri chanzo]

Kuachiliwa kwa Anyona kulikuja wakati wa uchaguzi wa Desemba 1992 chini ya Mfumo wa Vyama vingi. Macho ya vyama vyote vya upinzani yalimwelekea kuviunga mkono. Hata hivyo Anyona aliamua kuunda chama chake cha Kenya Social Congress licha ya kutarajiwa kujiunga na chama cha mwendani wake Jaramogi Oginga Odinga cha FORD-Kenya ambapo hata alikuwa amechaguliwa mwenyekiti wa tawi la Nyamira. Ni kutoka chama hiki chake ambapo alisimama kwa kiti cha urais lakini akashindwa. Licha ya kushinda kiti cha ubunge katika eneo la Kitutu Masaba, watu hawakuwa wanamtaka kama rais.

Alikuwa mbunge wa pekee nchi nzima kutoka chama cha Kenya Social Congress. Licha ya kutokuwa rais, kujitolea kwake kulimfanya kuwa mfano usioweza kufutika katika akili za watu.

Kifo[hariri | hariri chanzo]

Anyona aliaga mnamo 2003 katika ajali ya gari katika sehemu za Nairobi.

Viungo vya Nje[hariri | hariri chanzo]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

Makala hii kuhusu mwanasiasa fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu George Moseti Anyona kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.