Fresh Jumbe

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Fresh Jumbe
Fresh Jumbe katika pozi.
Fresh Jumbe katika pozi.
Maelezo ya awali
Jina la kuzaliwa Fresh Jumbe Mkuu Waziri Kungugu Kitandamilima
Amezaliwa 19 Oktoba 1968 (1968-10-19) (umri 55)
Asili yake Tanga, Tanzania
Aina ya muziki Dansi
R&B
Hip Hop
Kazi yake Mwimbaji
Mwanamuziki
Mtunzi wa nyimbo
Mtayarishaji wa rekodi
Ala Besi gitaa
Kinanda
Sauti
Miaka ya kazi 1988 - hadi leo

Fresh Jumbe Mkuu (jina la utani "Kungugu Kitanda Milima"; amezaliwa 19 Oktoba 1968) ni mwimbaji, mtunzi,mtayarishaji-mwanamuziki kutoka nchi Tanzania, ambaye ana makazi yake na shughuli zake za kimuziki kwa ujumla anazifanyia mjini Tokyo, Japani.

Fresh aliandika na kuimba nyimbo nyingi zilizovuma nchini mwake Tanzania kabla ya kuhamia Kenya, London Uingereza na kisha Tokyo Japan katika miaka ya 90.

Baadhi ya nyimbo zake zinazofahamika nchini Tanzania ni ‘TUHIFADHI MAZINGIRA’ (Tulinde Mazingira), ‘Penzi ni kikohozi’, Pamela, Conjesta, Ama zake ama zangu, ‘Elimu ni msingi wa maisha’ na nyingine nyingi.

Fresh hasa huimba katika lugha yake ya asili (Kiswahili), lakini pia kwa Kiingereza na Kijapani.

Sasa anaishi na kufanya biashara yake ya muziki na Studio huko Tokyo ambako anaongoza bendi inayoitwa 'THE TANZANITES'. Pia anaendesha Studio ya Fresh Productions ambayo anaitumia kurekodi muziki wake na mwanamuziki mwingine.

Wasifu

Maisha ya awali

Fresh Jumbe Mkuu Waziri Kungugu Kitandamilima alizaliwa tar. 19 Oktoba 1968 katika hospitali ya Ngamiani iliyopo katikati ya jiji la Tanga, Tanzania. Anatoka kwenye familia ya watoto nane, wanne wa kiume na wanne wa kike.

Wazazi wake wote wawili wametokea wilaya ya Pangani mkoani Tanga. Mama yake anatokea katika kijiji cha Bweni kinachoangalia mto Pangani na baba kwenye tarafa ya Mkwaja kijiji cha Buyuni kitopeni kilichopo mpakani kabisa kati ya wilaya ya Pangani na Bagamoyo.

Akiwa Tanga sehemu anayoiita nyumbani ni Makorora “Mti Mkavu” karibu kabisa na shule ya msingi Makorora ambayo ndipo alipoanzia elimu yake ya msingi kabla ya kuelekea Bakwata Sekondari kwa ajili ya elimu ya sekondari.

Fresh Jumbe ni mmojawapo wa wanamuziki wanaofanya muziki wa dansi akiwa nchi za nje. Na inaaminika kuwa analiwakilisha taifa lake katika nyanja za muziki huo vilivyo. Rasmi anafanyia shughuli zake za muziki nchini Japan. Lakini awali alikuwa na baadhi ya bendi za muziki huo kama vile Sikinde, Msondo, Bicco Stars, Safari Sound na nyingine nyingi tu. Kwa hakika Fresh Jumbe ni mojawapo ya majina ambayo washika dau katika medani za muziki hawawezi kuyasahau.

Tangu akiwa mdogo Fresh Jumbe alikuwa na ndoto ya kuwa mwimbaji. Kipindi fulani wakati akiwa bado katika shule ya msingi kule Tanga, aliwahi kuapa kuwa maisha yake ya ukubwani, kama yatakuwa ni ya kimasikini au ni yakitajiri au vyovyote vile, basi yatakuwa yametokana na miziki.

Aliapa kuwa uimbaji ndio utakaoongoza maisha yake. Kwahiyo ndoto yake hiyo nilianza kuifuatilia mapema tu akiwa bado mdogo kabisa na matokeo yake ni kuwa, mpaka leo maisha yake ni muziki na muziki ndiyo maisha yake.

Shughuli za muziki

Jumbe alivutiwa sana na marehemu Marijani Rajabu kutokana na utungaji wake, uimbaji wake na ufanyaji wake wa kazi akiwa jukwaani alimfanya atake kuwa kama yeye.

Mwingine ni kaka yake binamu "Marika Mwakichui" ambaye alikuwa mwimbaji wa bendi ya Tanga International ya Tanga. Yeye pia alikuwa mwimbaji mzuri na ndiye aliyempandisha kwenye jukwaa kwa mara ya kwanza ili aimbe baada ya kugundua uwezo wake wa kuimba akiwa bado yuko darasa la sita.

Alimpa moyo sana na kumwambia kuwa yeye anaweza kabisa kuimba kuliko hata baadhi ya waimbaji wakubwa wa wakati ule. Hivyo shukrani za dhati zikamwendea ndugu huyo kwa msukumo na msaada aliompa na kumfanya ajiamini na aingie kikamili kwenye muziki mpaka kufikia alipofikia leo hii.

Kuanza kupata umaaurufu

Mnamo mwaka wa 1988 akiwa katika bendi ya Safari Sound "Ndekule", Taasisi ya Kuhifadhi Mazingira ya Tanzania kupitia chama cha muziki wa dansi Tanzania "CHAMUDATA" iliteua baadhi ya watungaji iliyoamini kuwa ni watungaji wazuri, ili watunge nyimbo mbili za uhifadhi wa mazingira ili zikawakilishe nchi ya Tanzania kwenye Tamasha la kuhifadhi mazingira la Afrika katika siku ya mazingira duniani. Kwa wakati huo kwa upande wa Afrika, tamasha lilifanyika mjini Nairobi, Kenya.

Jumbe alikuwa mmoja kati ya walioteliwa kutunga nyimbo hizo. Walioitwa katika katika utunzi huo alikuwa Cosmass Chidumule, marehemu Hemedi Maneti, Jah Kimbute, marehemu Eddy Sheggy, marehemu Jerry Nashon "Dudumizi" na wengine kadhaa.

Walipewa maelekezo ya kila mtu kutunga nyimbo moja ya mazingira. Pia walielezwa ni masuala gani muhimu yanayotakiwa kuzungumzwa kwenye hizo nyimbo. Wakapewa wiki mbili za kutunga nyimbo. Pia waliambiwa kuwa, haya ni mashindano na washindi wawili watakaopatikana, yaani watakaotunga nyimbo mbili za kwanza zitakazokubalika zaidi na Taasisi ya Mazingira ya Tanzania, watapata zawadi ya pesa na pia wao ndiyo watakuwa wawakilishi wa nchi kwenye hilo tamasha la mazingira huko mjini Nairobi. Kwa bahati nzuri, nyimbo yake ikawa namba moja na ya Cosmass Chidumule ikawa ya pili.

Zawadi zikatolewa kwa washindi na pia wakapelekwa Nairobi kuiwakilisha nchi kwenye tamasha hilo. Hilo ndilo lilikuwa chimbuko la wimbo wa "Tuhifadhi Mazingira" na ndiyo wimbo pekee uliyomleta juu katika masiha ya muziki.[1]

Muziki

Albamu

Single

Marejeo

  1. "Mahojiano ya Fresh Jumbe na CB - "Bongo Celebrity"". Ilihifadhi kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2009-04-02. Iliwekwa mnamo 2008-11-03. 

Viungo vya nje

Makala hii kuhusu mwanamuziki/wanamuziki fulani wa Tanzania bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Fresh Jumbe kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.