Chuo Kikuu Kishiriki cha Jordan
Chuo Kikuu Kishiriki cha Jordan ni tawi la Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Tanzania lililopo Morogoro.[1] Kilianzishwa kama seminari kuu kwa watawa ya mashirika yoyote, ikageuzwa baadaye kuwa Taasisi ya Falsafa na Teolojia na hatimaye Chuo Kishiriki cha Jordan.
Historia
[hariri | hariri chanzo]Wakuu wa mashirika ya kitawa wanaofanya kazi nchini Tanzania walikubaliana mapema na Mkuu wa misheni ya Wasalvatoriani, Fr. Andrew Urbanski, kwamba kulikuwa na hitaji la taasisi ya Elimu ya juu kwa wanashirika wao, haswa wale walioitiwa upadri.
Kwa furaha ya wote waliohusika, maandalizi ya taasisi hiyo yakaanza Kola, katika mji wa Morogoro. Majadiliano juu ya mradi huu yalizinduliwa katika mkutano wa kila mwaka wa Jumuiya ya Viongozi wa Mashirika ya Kidini Tanzania (RSAT) mwaka 1988. Baada ya muda, iliamuliwa kuwa taasisi hiyo iwe na Idara ya Falsafa na Idara ya Teolojia.
Mnamo Desemba 11, 1990, Baraza la Misheni la Wasalvatoria Tanzania lilikubali kuanzisha Seminari Kuu ya Wasalvatoria yenye falsafa na teolojia. Ilikubaliwa kuwa mtakatifu mlezi wa seminari hiyo awe Mwanzilishi wa Wasalvatoria, Padre Francis Mary wa Msalaba Jordan. Wasalvatoria wa Tanzania walipata ruhusa ya kudhamini mradi huo. Askofu Adrian Mkoba, wa Jimbo Katoliki la Morogoro (tarehe 22 Februari, 1988), na Askofu Mkuu Anthony Mayala, aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu Tanzania (katika barua yake ya tarehe 2 Machi mwaka huo), kwa niaba ya Baraza hilo, walitoa nihil obstat na baraka zao.
Tarehe 2 Septemba, 1990, Papa Yohane Paulo wa Pili alibariki jiwe la msingi la seminari hiyo alipokutana na makasisi na watawa, wakati wa ziara yake ya kichungaji katika Kanisa la Mtakatifu Petro, Dar es Salaam. Mkuu mpya wa Misheni ya Wasalvatoria Tanzania, Padre Zdzislaw Tracz, SDS, alipewa jukumu la kutekeleza mpango huo. Alimshirikisha mbunifu wa Kiswisi, Herbert Kramel kutoka Chuo Kikuu cha Zurich, Uswisi, kwa ajili ya usanifu wa majengo. Alikubaliana na kampuni ya ujenzi ya Kiitaliano-Kitanzania, Coastal Steel, kuanza ujenzi mwaka 1991 kule Morogoro-Kola.
Ifikapo katikati ya mwaka 1993, ujenzi wa seminari ulikuwa umefikia hatua ambapo majengo yalikuwa tayari kwa ajili ya kuanza masomo ya Falsafa mnamo Agosti 16. Waalimu sita wa awali walitoka mashirika ya Holy Ghost Missionaries, Consolata Fathers, Wasalvatoria, na mwalimu mmoja wa kiraia aliyefika katikati ya mwaka wa pili. Walimu hawa walitoka Tanzania, Msumbiji, Uholanzi, Poland na Marekani. Wanafunzi wa mwanzo 25 walikuwa wakitoka katika mashirika ya kidini matano.
Mwaka wa pili, wanafunzi wengine 21 walianza masomo yao ya Falsafa. Ilitarajiwa kuwa kila mwaka kungekuwepo na wanafunzi wapya 20 hadi 25 kwa programu hiyo ya miaka mitatu ya Falsafa.
Ifikapo 1995, idadi ya wanafunzi iliongezeka hadi 80, kutoka katika mashirika ya kidini tisa. Seminari Kuu ya Wasalvatoria pia ilianza kupokea wanafunzi wanaoanza mwaka wa kwanza wa masomo ya Teolojia. Mwaka huo huo, seminari hiyo ilipata uhusiano rasmi na Kitivo cha Falsafa cha Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana, Roma. Hali hiyo ilithibitishwa rasmi tarehe 6 Julai, kupitia Waraka #932/95/2.
Mwaka 1998 idadi ya wanafunzi ilikuwa imeongezeka hadi 170, kutoka mashirika ya kidini 15. Idadi ya wafanyakazi wa kitaaluma ilifikia 24, kutoka mashirika ya kidini 12, pamoja na walimu watatu wa kiraia.
Tarehe 26 Januari, 1999, kupitia Waraka #164/99, seminari hiyo ilipata uhusiano rasmi pia na Kitivo cha Teolojia cha chuo hicho hicho cha Urbaniana. Wakati huo huo, uongozi wa seminari pamoja na Makao Makuu ya Jamii ya Mwokozi wa Kimungu waliwasilisha ombi kwa mamlaka za Kanisa kubadili jina la taasisi hiyo kutoka Seminari Kuu ya Wasalvatoria kuwa Taasisi ya Falsafa na Teolojia ya Wasalvatoria. Ombi hilo lilikubaliwa na Mabaraza ya Uinjilishaji na Elimu ya Kikristo pamoja na Chuo Kikuu cha Kipapa Urbaniana tarehe 21 Aprili, 1999.
Tarehe 16 Aprili, 2010, Baraza Kuu la Jamii ya Mwokozi wa Kimungu lilikubali kubadilisha Taasisi ya Wasalvatoria kuwa chuo tanzu cha Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine wa Tanzania kwa jina la Jordan University College. Tarehe 2 Novemba, 2010, chuo hiki kilipata Cheti cha Usajili wa Muda kutoka Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).
Taasisi hiyo iliongozwa na:
- Padre David Brusky, SDS – mkuu wa kwanza wa seminari (1993–1996),
- Padre Stanislaw Golus, SDS – mkuu wa pili wakati wa mpito kutoka seminari kuwa taasisi (1996–1999),
- Padre Julian Bednarz, SDS – mkuu wa tatu (1999–2005),
- Padre Bernard Witek, SDS – mkuu wa mwisho wa taasisi (2005–2010)
Dhamira
[hariri | hariri chanzo]Dhamira ya JUCO ni kuanzisha na kupanua fursa za elimu ya juu nchini Tanzania na nje kwa kutoa programu za shahada na zisizo za shahada.
Maono
[hariri | hariri chanzo]JUCO inalenga kutoa elimu ya juu inayowalenga kuandaa wasomi na viongozi wa Afrika.
Malengo
[hariri | hariri chanzo]Kubadilishwa kwa Taasisi ya Wasalvatoria kutoka kuwa seminari hadi kuwa chuo cha elimu ya juu kulikuwa na malengo yafuatayo:
- Kuchangia kikamilifu zaidi kwa Kanisa la ndani kwa kuwaandaa wagombea wa upadri,
- Na kwa kuzingatia Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Tanzania 2025, kutoa programu za kitaaluma zilizolenga kutatua changamoto za jamii na kuchangia maendeleo ya taifa.
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- ↑ "Wayback Machine" (PDF). web.archive.org. 2015-09-24. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo (PDF) mnamo 2015-09-24. Iliwekwa mnamo 2021-06-19.
| Makala hii kuhusu mambo ya elimu bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Chuo Kikuu Kishiriki cha Jordan kama historia yake, uenezi au maendeleo yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |