Nenda kwa yaliyomo

Charles de Gaulle

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Jenerali Charles de Gaulle

Charles-André-Joseph-Marie de Gaulle (22 Novemba 1890 - 9 Novemba 1970) alikuwa mwanajeshi, mwanasiasa na Rais wa Ufaransa.

Mwanajeshi

[hariri | hariri chanzo]

Alijiunga na jeshi 1908 kabla ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia. Alikamatwa na Wajerumani wakati wa mapigano ya Verdun na kuwa mfungwa wa vita. Baada ya 1918 aliandika vitabu kadhaa juu ya nadharia ya vita na hasa juu ya mahitaji ya kutumia mitambo ya kisasa jeshini akisisitiza haja ya kutegemea vifaru na ndege za kivita.

Tangazo la De Gaulle anapoita Wafaransa wote kuendelea na vita dhidi ya Ujerumani
De Gaulle pamoja na rais wa Marekani Roosevelt na kiongozi wa Uingereza Churchill huko Casablanca 1942

Vita Kuu ya Pili

[hariri | hariri chanzo]

Wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia alikuwa mkuu wa kikosi cha vifaru kwa cheo cha kanali. Akiongoza sehemu ya pekee ya jeshi la Ufaransa iliyofaulu kurudisha mashambulio ya Wajerumani alipandishwa cheo cha jenerali. Wakati serikali ya Ufaransa iliandaa kusimamisha vita alikataa akahamia Uingereza tar. 17 Juni 1940 kwa shabaha ya kuendeleza vita.

Kiongozi wa Ufaransa Huru

[hariri | hariri chanzo]

Hapa aliunda kamati ya "Ufaransa Huru" akikusanya wanajeshi Wafaransa walioweza kukimbia Uingereza pamoja na sehemu za jeshi la Ufaransa katika koloni zilizoshirikiana naye badala ya serikali ya Vichy chini ya Jemadari Petain. De Gaulle alikuwa mkuu wa Jeshi Huru la Kifaransa.

Baada ya uvamizi wa Marekani katika Afrika ya Kaskazini De Gaulle alihamia Algiers na kuunda Kamati ya Ukombozi wa Ufaransa iliyojiita serikali ya muda ya Ufaransa. De Gaulle aliingia 1944 akaamuru kikosi cha Jeshi Huru ya Kifaransa kuingia Paris ili mji ukombolewe na Wafaransa wenyewe.

Kiongozi wa serikali baada ya vita

[hariri | hariri chanzo]

Baada ya Vita alikuwa kiongozi wa serikali ya kwanza akashiriki katika majadiliano ya nchi washindi juu ya Ujerumani pamoja na Marekani, Uingereza na Umoja wa Kisovyeti. 20 Januari 1946 akajiuzulu kwa sababu hakupendezwa na fitina ya vyama vya kisiasa serikalini pamoja na mabadiliko ya katiba ya Jamhuri ya Nne ya Ufaransa. Alikaa kwake nyumbani na kuandika vitabu.

Kurudi katika siasa 1958

[hariri | hariri chanzo]

1958 alirudi katika siasa wakati wa vita ya kikoloni huko Algeria iliyoangusha serikali. Rais wa taifa alimpa nafasi ya waziri mkuu na bunge lilikubali kumpa madaraka ya dharura. De Gaulle aliandaa katiba mpya iliyoongeza madaraka ya rais ikakubaliwa katika kura ya wananchi hivyo kuunda Jamhuri ya Tano ya Ufaransa.

Rais wa Jamhuri ya Tano 1958-1969

[hariri | hariri chanzo]

Katika Novemba 1958 De Gaulle alishinda uchaguzi akachaguliwa na bunge kuwa rais. Alirudishwa mara ya pili 1965 akipigiwa kura na wanachi wote.

Kaburi la De Gaulle

Akiwa rais alifuata siasa ya kujitegemea kwa Ufaransa. Alijenga jeshi la kinyuklia na kuiondoa Ufaransa katika ushirikiano wa kijeshi wa NATO hata akiendelea kushiriki kisiasa. Aliondoa Wafaransa katika Algeria na kuwasilisha uhuru wa nchi hiyo 1962. Alijiondoa pia katika koloni nyingine hasa Afrika.

Katika siasa ya nje alitafuta msimamo wa pekee na Marekani. Alilenga kujenga Umoja wa Ulaya kwa kukaribiana na Ujerumani lakini alizuia Uingereza isiingie.

Baada ya kushindwa katika kura ya wananchi juu ya katiba alijiuzulu 28 Aprili 1969.

Charles de Gaulle aliaga dunia tar. 9 Novemba 1970 akazikwa kwake nyumbani Colombey-les-Deux-Églises.

Makala hii kuhusu mwanasiasa fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Charles de Gaulle kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.