Nenda kwa yaliyomo

Carl Friedrich Gauss

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Gauss
Sanamu ya Gauss mjini Braunschweig

Carl Friedrich Gauss (Gauß) (30 Aprili 177723 Februari 1855) alikuwa mtaalamu wa hisabati, fizikia na falaki kutoka nchini Ujerumani.

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Alizaliwa mjini Braunschweig katika Ujerumani ya kaskazini (leo hii jimbo la Saksonia ya chini). Akili zake zilionekana alipokuwa bado mtoto mdogo. Alipokuwa na umri wa miaka mitatu alimwonyesha babake kosa wakati huyu alipopiga hesabu ya mshahara wake. Mtoto alijifundisha mwenyewe kusoma.

Baada ya kuingia katika shule ya msingi alimshtusha mwalimu wake aliyewapa wanafunzi kazi ya kujumlisha namba zote kuanzia 1 hadi 100. Wanafunzi wengine hawakuanza bado kazi Gauss alimwonyesha mwalimu tayari matokeo. Alikuwa alitambua mara moja ya kwamba 100 + 1 = 101, 99 + 2 = 101, 98 + 3 = 101, na jumla ni jozi 50 za namba. Kwa hiyo alipiga 101 * 50 akapata 5050 mara moja. Mwalimu alielewa baada ya muda mdogo ya kwamba mtoto huyu hawezi kujifunza kitu kwake tena akamsaidia kuingia shule ya sekondari mapema.

Alipofikia umri wa miaka 14 alitambulishwa kwa mtemi wake na huyu alimsomesha kwanza kwenye chuo cha ufundi halafu kwenye chuo kikuu cha Goettingen aliposoma kati ya 1795 na 1798. 1799 alichukua digrii ya dokta.

Tangu 1807 alipata cheo cha profesa katika Goettingen akafundisha hisabati na kuwa mkurugenzi wa taasisi ya falaki. Na kazi aliendelea hadi kifo chake mwaka 1855.

Kazi ya kisaysansi[hariri | hariri chanzo]

Gauss alibuni mambo mengi. Alikuwa mtu wa kwanza aliyeonyesha jinsi gani kuchora pembekuminasaba. Alitengeneza jedwali inyoonyesha tarehe ya Pasaka kwa kila mwaka. Alitoa nadharia juu ya namba tasa inayoonyesha jinsi gani namba tasa zinatawanyawa kati ya namba za kawaida. Mbinu wa namba mraba ndogo ulimsaidia kubuni uenezi kawaida wa mchirizo unaoeleza wastani ya vipimo vinavyotofautiana kiasi. Mbinu huu umekuwa msingi wa ueneaji yamkini na takwimu ya kisasa.

Katika falaki alitumia mbinu wa namba mraba ndogo kukadiria njia ya asteoridi kadhaa na kwa njia hii aliweza kutabiri mahali pao angani na kurahisisha kuziona kwa darubini.

Alitumia nadharia zake za hisabati pia kwa upimaji wa nchi akasimamia upimaji wa ufalme wa Hannover ulioleta ramani nzuri za kwanza za Ujerumani ya Kaskazini.

Katika fizikia alishughulika mambo ya sumakuumeme akatengeneza telegrafi ya kwanza iliyowasilisha habari kati ya taasisi ya falaki na ofisi yake.