Barabara ya Julius K. Nyerere

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Barabara ya Julius K. Nyerere (pia Nyerere Road) ni kati ya barabara kuu kwenye jiji la Dar es Salaam, na inapitia maeneo mbalimbali ya jiji, ikiunganisha vitongoji vingi na maeneo muhimu ya biashara na makazi. Barabara ya Nyerere ni kiungo muhimu cha usafirishaji na usafiri wa umma, pia ni njia kuu ya kufika na kuondoka kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.

Inachukua jina lake kutoka kwa Hayati Julius Kambarage Nyerere, ambaye alikuwa rais wa kwanza wa Tanzania baada ya uhuru. Zamani ilijulikana kwa jina la Pugu Road maana inaelekea kutoka kitovu cha jiji kwenda Pugu upande wa kusini-magharibi. Sehemu ya kwanza ya Pugu Road ya zamani siku hizi inaitwa Nkrumah Street.

Barabara hii inaanza kwenye njiapanda ya Gerezani Street, inapita kituo cha reli ya Tazara na kufika kwenye uwanja wa ndege, ikiendelea hadi Gongo la Mboto.

Kwenye njiapanda ya barabara ya Nyerere na barabara ya Nelson Mandela kuna daraja la Mfugale ambalo limesaidia kupunguza msongamano wa magari kwenye njiapanda hii.