Uchimbaji wa madini nchini Tanzania

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mgodi wa almasi wa Williamson
Lori kubwa katika Mgodi wa Dhahabu wa Buzwagi

Tanzania ni nchi yenye madini mengi. Uchimbaji madini hufanya zaidi ya 50% ya jumla ya mauzo ya nje ya nchi, ambayo sehemu kubwa inatokana na dhahabu. Nchi ina akiba ya dhahabu ya wakia milioni 10. Uchimbaji wake unazalisha mapato ya zaidi ya dola bilioni. [1]

Almasi pia hupatikana kwa kiasi fulani. Tangu ulipofunguliwa mwaka wa 1940, mgodi wa almasi wa Williamson umezalisha karati milioni 19 (3,800 kg) ya almasi.

Mawe aina ya vito, nikeli, shaba, uranium, kaolin, titanium, cobalt na platinamu pia huchimbwa nchini Tanzania.

Uchimbaji haramu na ufisadi ni matatizo yanayoendelea. Mwaka 2017, serikali ilipitisha mfululizo wa miswada yenye lengo la kuongeza mapato yatokanayo na madini baada ya kashfa iliyosababisha kufukuzwa kazi kwa Waziri wa Nishati na Madini.

Historia[hariri | hariri chanzo]

Sekta ya madini awali ilikuwa ikimilikiwa na kudhibitiwa na serikali. Sheria za uchimbaji madini zililegezwa katika miaka ya 1980 na 1990 ili kuruhusu umiliki binafsi wa migodi na kuingia kwa kampuni za kigeni.

Mwaka 2008, sekta ya madini iliajiri takriban watu milioni moja katika uchimbaji wa kienyeji, ingawa si rahisi kupata takwimu sahihi[2].

Kufikia mwaka 2011, kulikuwa na wachimbaji wadogo 50,000 waliohusika katika uchimbaji wa vito vya rangi.

Mwaka 2015 Benki ya Dunia iliipatia Tanzania mkopo wa dola milioni 45 ili kuboresha sekta ya uchimbaji mdogo wa madini[3].

Uzalishaji na athari[hariri | hariri chanzo]

Uchimbaji haramu wa madini umeenea mahali pengi nchini Tanzania, na unaleta hatari kubwa kwa wale wanaofanya shughuli hiyo. Mnamo mwaka wa 2015, handaki lilianguka katika mgodi haramu karibu na Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu, na kuua watu 19.[4]

Wachimbaji katika migodi midogo nchini Tanzania wanapaswa kufanya kazi katika mashimo chini ya ardhi yenye na upitishaji hewa duni zaidi kuliko wenzao katika migodi ya makampuni makubwa.

Mfichuo wa vumbi ya silika kwenye mgodi mdogo ni zaidi ya mara mia mbili kuliko kwenye mgodi mkubwa, na jumla ya silika zinazopeperuka hewani ni zaidi ya mara mia tatu ya kikomo kinachoruhusiwa katika nchi zinazoendelea. Kifua kikuu ni ugonjwa unaopatikana kati ya wachimbaji madini wa Tanzania kushinda wastani wa wananchi wote.[5]

Rais wa tano wa Tanzania, John Magufuli, aliweka sheria mpya katika sekta ya madini mwaka 2017, ikiwa ni pamoja na ushuru mkubwa kwa madini yanaosafirishwa nje ya nchi na kuipa serikali kiasi kikubwa zaidi cha hisa katika baadhi ya kampuni za uchimbaji madini. Sheria hizo zilikuwa zikipunguza uwekezaji katika sekta hii. [6]

Bidhaa[hariri | hariri chanzo]

Sekta ya madini inatoa mchango mkubwa katika uchumi wa Tanzania hasa kwa uchimbaji wa shaba, dhahabu na fedha pamoja na baadhi ya madini ya viwandani na vito kama vile almasi. Makampuni ya kimataifa ya uchimbaji madini yanatawala sekta hiyo katika uchimbaji wa dhahabu na almasi, huku shughuli za ziada za uchimbaji mdogo zikitawanyika kote nchini[7].

Tanzania ni nchi ya nne ya kuzalisha dhahabu barani Afrika baada ya Afrika Kusini, Mali na Ghana. Mwaka 2010 asilimia 2 za uzalishaji wa dhahabu duniani zilitoka Tanzania[8].

Tanzanite ni kito cha kipekee kwa kuwa kinapatikana katika nchi hiyo pekee.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. The Mining Industry in Tanzania: An Overview, Varun Kareparambil, Linkedin 14.07.017, iliangaliwa 16 Februari 2018
  2. Putting Tanzania's Hidden Economy to Work: Reform, Management, and Protection of its Natural Resource Sector, World Bank 2008. ISBN 9780821374627.
  3. World Bank grants Tanzania $45 million to improve mining sector, Cecilia Jamasmie ining.com, iliangaliwa 11 Mei 2015
  4. Collapse of illegal Tanzanian gold mine kills 19 people, Reuters 17 Aprili 2015
  5. Silica dust in Tanzania artisan gold mines 300 times US limit, study finds, Mining Innovation News, 30 Aprili 2015
  6. Investors wary as Tanzania moves to assert more control over mines, 25 Septemba 2017 Reuters
  7. The Mining Industry in Tanzania: An Overview, Varun Kareparambil
  8. "2011 Minerals Yearbook: Tanzania[Advance Release" (PDF). U.S. Department of the Interior:U.S. Geological Survey. Retrieved 4 June 2015.