Nenda kwa yaliyomo

Saadani Abdu Kandoro

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Kushoto: Iddi Faiz Mafungo, Sheikh Mohamed Ramia, Julius Nyerere, Saadan Abdu Kandoro na Haruna Taratibu.

Saadani Abdu Kandoro (alizaliwa katika eneo la Kasingirima-Ujiji mkoani Kigoma tarehe 8 Desemba 1926) alikuwa mwanasiasa na mshairi nchini Tanzania. Anahesabiwa kati ya wanasiasa waliopigania uhuru wa Tanganyika wakishirikiana na Julius Nyerere[1].

Baada ya kumaliza elimu ya msingi katika shule ya msingi Ujiji alijiunga na shule ya upili ya serikali huko Iringa na baadaye Chuo cha Ualimu cha Bwiru, Mwanza.

Mwaka 1944 aliingia katika utumushi wa serikali ya kikoloni kwenye idara ya kuweka hazina Uyui Tabora.

Aliendelea kujishughulisha na katika kuanzisha vyama vya ushirika na hatimae akawa diwani wa Advisory Coucil ya mji wa Tabora .

Tangu 1940 alishiriki katika Tanganyika African Association (TAA).

Mnamo mwaka 1954 alikuwa miongoni mwa watu 17 walioanzisha chama cha TANU mjini Dar es Salaam.

Ilipofika mwaka 1962, aliteuliwa kuwa katibu wa TANU na kamishna wa wilaya ya Mafia. Mwaka 1964 aliendelea kuwa katibu wilaya ya Mafia ambapo alihudumu hadi mwaka 1970 ambapo aliacha kazi hiyo na kuamua kujishughulisha na ukulima.

Mashairi

[hariri | hariri chanzo]

Pamoja na Ushairi na siasa, Saadani A. Kandoro amendika mashairi mengi ya malumbano akipambana na magwiji wa ushairi na wanasiasa wakubwa wa Tanzania akiwemo mwalimu Julius Nyerere.

Shairi hili aliandikiwa na Mwalimu Nyerere kama ujumbe:

Sheikh Kandoro sikia 1. Sheria husaidia Kuijenga Tanzania Siyo kazi ya sheria Nchi kutuharibia.

2. Kila nchi ina nia Inayoikusudia Vilevile ina njia Itakayoipitia.

3. Tanzania tuna nia Ya kujenga ujamia Na njia ya kupitia Ni wote kusaidia.

4. Kijiji chaturadhia Kisima kujipatia Lamgambo limelia Watu wakahudhuria.

5. Wakakubali kwa nia Kisima kujichimbia Aliye wakatalia Kukuye wakamlia.

6. Akaenda kushtakia Kwa hakimu wa sheria Kwamba wamemuonea Kuku wake kumlia.

7. Hakimu akasikia Akaita jumuia Wakaja akawambia Nyinyi mwavunja sheria.

8) Basi nawahukumia Faini shilingi mia Na sabini za fidia Au jela kuingia.

9) Hakimi wakamwambia Itatushinda fidia Hata na faini pia Heri jela kuingia.

10. Wakafungwa kwa sheria Na maji wakamwachia Mwenye kuku kuumia Pamwe na hakimu pia.

11. Huko ni kusaidia Adui wa jummuia Nasi kazi za sheria Ila ya maharamia.

12. Kazi hasa ya sheria Kusaidia raia Si nia kuwavunjia Wanapojisaidia.

Saadani Kandoro aliandika shairi lifuatalo kumjibu Mwalimu Julius Nyerere:

1. Labeka muheshimiwa Julius msifiwa Kambarage muelewa Bwana nakuitikia.

2. Nakuitikia sheria Kwamba inasaidia Kuijenga Tanzania Na ni nguzo ya dunia.

3. Kutoheshimu sheria Huleta wingi udhia Amani ikapotea Nchi zikaangamia

4. Ni msumeno sheria Methali hii natia Haitaki kubabia Pendeleo liso njia.

5. La mgambo likilia Watu wote hudhuria Kisima kujichimbia Hilo lataka sheria.

6. Kuna wavivu wa nia La mgambo likilia Nao wanajikalia Haendikuhudhuria.

7. Mfano huo hatua Wengine hufuatia Na wao hujikalia Kazi zetu husinzia.

8. Kimila nimesikia Waweza kumfikia Kuku wake kujilia Lakini siyo sheria.

9. Kwa kuwa siyo sheria Mvivu kujistakia Na walao huumia Pia huyozwa fidia

10. Twazidi kukulilia Lifanywe hasa sheria By law kujitia Naweza kusaidia.

11. Yaweza kusaidia Kuku tukijilia Pasiwepo hata njia Mvivu kukimbilia.

12. Kuku tumejilia Pasiwe la kuponyea Hakimu kumuendea Kwamba ilipwe fidia.

13. Mkwazo twaukazia Bila nyuma kurudia Twataka kuendelea Kuinuwa Tanzania.

14. Taifa kuitikia Kazi kuzishangilia Ndio tunalo Lilia Ndipo tunakazania

15. Ndipo tunakazania Na tena tunakania Kuishangaza dunia Lengo letu kutimia.

16. Bila nguvu kuzitia Mkazo wa kisharia Unafaa kufutia Kazi zikaendelea.

Mbali na Mwalimu Nyerere, Kandoro pia walikuwa akiandikiana mashairi na washairi wakubwa huku akishindana na magwiji hapo kama kina Moses Mnyampala, Salahe Kibwana, Mdanzi Hanasa na wengine wengi.

Alifanikiwa kutoa kitabu maarufu "Mashairi ya Saadani" ambacho kilichapishwa na Shirika la Magazeti ya Chama Ltd.

  1. http://www.oxfordreference.com/view/10.1093/acref/9780195382075.001.0001/acref-9780195382075-e-1012, Kandoro kwenye Dictionary of African Biography, kupitia oxfordreference.com

Marejeo ya Nje

[hariri | hariri chanzo]
Makala hii kuhusu mwanasiasa fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Saadani Abdu Kandoro kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.