Periplus ya Bahari ya Eritrea

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Majina, mahali na njia za biashara katika Periplus

Periplus ya Bahari ya Eritrea ni kitabu cha mwongozo kwa ajili ya mabaharia kilichoandikwa mn. mw. 70 b.K.. "Periplus" ni neno la Kigiriki linalomaanisha tendo la kuzunguka baharini kwa merikebu; Bahari ya Eritrea ni jina la kale kwa ajili ya Bahari ya Shamu pamoja na Bahari Hindi. Jina limeundwa na watu wa nchi za mashariki ya Bahari ya Mediteraneo na Misri waliotumia lugha ya Kigiriki wakati wa miaka 2000 iliyopita.

Kitabu hiki kimeandikwa na mwenyeji wa Aleksandria / Misri iliyokuwa mji mkubwa wakati ule na kitovu cha biashara ya kimataifa kati ya Dola la Roma, Afrika ya Mashariki na Bara Hindi.

Kitabu cha Periplus kinaeleza mabandari kuanzia Misri hadi Afrika ya Mashariki kwa upande moja na hadi Bara Hindi kwa upande mwingine. Kinataja majina ya mabandari, bidhaa zilizopelekwa huko na bidhaa zilizopatikana kila mahali. Pia kuna habari za kando juu ya watu, watawala ni mila zao.

Maelezo ni mengi kuhusu pwani la Eritrea na Somalia hadi Pembe la Afrika; kuelekea kusini majina ya mabandari ni machache; mwisho wa eneo lililojulikana ni mji wa Rhapta katika nchi za Azania.