Kanisa la Biblia Publishers
Kanisa la Biblia Publishers ni idara ya Maandiko ya Kanisa la Biblia Tanzania.
Kazi yake ni kutafsiri, kuandaa na kutoa maelezo ya Biblia kwa Kiswahili. Inachapisha vitabu kwa msomaji wa Biblia anayetaka kuelewa vizuri zaidi, ili apate kuelewa mwenyewe, kuwafundisha wengine neno la Mungu na kutafsiri maana yake kwa maisha ya kila siku.
Kanisa la Biblia Publishers inadhamiria kukuza ufahamu wa Biblia Afrika Mashariki kwa njia ya kusambaza maandiko ya Kikristo yanayosaidia kuelewa Maandiko kwa manufaa binafsi, kwa kukua kiroho na kwa kutoa mafundisho.
Historia
[hariri | hariri chanzo]Vitabu vya kwanza „Panorama ya Biblia“ na „Imani Yetu Ndiyo Ushindi“ vilitolewa mwaka 1980 na kuchapishwa na Nusch-Druck Gummersbach, Ujerumani. Vitabu vyote viwili vilitafsiriwa kutoka Kijerumani na Helmut Gräf, aliyekuwa mwanzilishi wa Chuo cha Biblia Nanjoka, Tunduru, Mkoa wa Ruvuma, Tanzania. Palikuwa na uhitaji wa kuandika au kutafsiri vitabu vinavyoeleza Biblia kwa walimu na wanafunzi wa Biblia Afrika Mashariki.
Kisha Helmut Gräf alianza kutafsiri ufafanuzi wa Agano Jipya katika vitabu 5 vinavyoitwa “Agano Jipya Lasema” No. 1 hadi 5, na baadaye aliongeza vitabu 10 vya “Agano la Kale Lasema” No. 1 hadi 10. Huu ni ufafanuzi wa kwanza wa Kiswahili wa Biblia nzima. Mfululizo una vitabu 15 na ulitolewa tangu mwaka 1986 hadi 1990.
Baadaye vitabu vyote 15 vilijumlishwa katika kitabu kimoja kinene kinachoitwa “Bibla Inasema” na kutolewa mwaka 2000 Dodoma. Kazi ya kusambaza vitabu haikuwa rahisi kutoka Tunduru, kusini mwa Tanzania. Kwa hiyo Kanisa la Biblia Publishers walihamia mji mkuu wa Tanzania, Dodoma. Kutoka hapo katikati ya nchi usambazaji uliendelea vizuri tangu mwaka 1993.
Wakati wa ujenzi wa kituo cha maandiko Dodoma kuanzia mwaka 1991 Helmut Gräf aliendelea kutafisiri “Kamusi ya Biblia” kutoka Kiingereza. Kitabu hiki muhimu cha rejea kilichoandikwa na Don Fleming kilitolewa Dodoma mwaka 1995.
Hatua nyingine kubwa ilikuwa kutafsiri na kutoa vitabu viwili vya Erich Sauer kutoka Kijerumani kuhusu Historia ya Wokovu. Vitabu viwili “The Dawn of World Redemption” na “The Triumph of the Crucified” vilitolewa mwaka 2003 katika kitabu kimoja kinachoitwa “Ufunuo wa Mungu na Itikio la Imani”. Kwa kutumia kitabu hiki msomaji wa “Panorama ya Biblia” anaelewa vizuri zaidi historia ya Mungu na wanadamu.
Kitabu cha mwisho kilichotolewa kimeandikwa na John Stott na kinaitwa „Wito wa Viongozi wa Kikristo“. Kitabu hiki kinafundisha mikakati ya uongozi kufuatana na 1 Wakorintho sura ya 1 hadi 4.