Zege

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Zege inamwagwa katika fremu yake. Inatoka katika bomba na mjenzi inaigawa juu ya wavu wa nondo za feleji zitakazokaa ndani ya ukuta. Mfanyakazi wa pili anatumia chombo cha kitingishi kinachoondoa nafasi za upepo katika zege iliyomwagika
Zege inamwagwa kwa mkono ndani ya fremu ya kuwa sehemu ya ukuta juu ya dirisha na mlango; nondo isiyofunikwa bado inaonekana itahakikisha uimara wa sehemu hii

,

Zege ni rojo maalumu inayoandaliwa kwa ajili ya ujenzi wa majengo mbalimbali, hasa ya ghorofa.

Ni mchanganyiko wa saruji, mchanga, mawe na maji. Kuna pia nyongeza nyingine zinazoweza kuungwa katika zege kama vile rangi, unga wa mawe, majivu au kemikali mbalimali zinazoboresha tabia kadhaa za zege.

Baada kuchanganya viungo vyote maji huongezwa Hadi kufikia hali ya uji mzito. Katikati hali hi zege inaweza kumwagwa kwenye nafasi iliyoandaliwa. Baada ya muda huganda na kuwa imara kama jiwe.

Nyenzo inayotumiwa zaidi duniani[hariri | hariri chanzo]

Leo hii zege ni nyenzo ya ujenzi inayotumiwa zaidi duniani kuliko mawe au matofali.[1]

Zege ya kumwagwa[hariri | hariri chanzo]

Sehemu zote za zege huchanganywa hadi kufikia hali ya kufanana na uji au kinyunga cha kutengenezea mkate. Katika hali hii zege inaweza kumwagwa katika fremu au kizingio. Kutokana na umbo la fremu yote inapokea umbo lake. Baada ya kumwagwa zege inaganda na kuwa ngumu kama mwamba. Baadaye fremu huondolewa na kuacha ukuta, msingi au sehemu ya jengo iliyokusudiwa.

Zege iliyoimarishwa[hariri | hariri chanzo]

Zege ina nguvu kubwa dhidi ya shindikizo au mkazo lakini ni dhaifu zaidi dhidi ya nguvu za mvutano. Tabia hii ni faida kama msingi wa zege inatakiwa kupokea uzito wa kuta za juu. Lakini kwa sehemu nyingine ambako mvutano unaweza kutokea zege inahitaji kuimarishwa. Hapa wajenzi wanatumia nondo na nyavu za feleji ndani ya zege. Feleji ni imara sana ikivutwa na kwa njia ya kuunganisha feleji na zege katika ukuta faida za nyenzo zote mbili zinaunganishwa.

Zege inayosafirishwa[hariri | hariri chanzo]

Kwa majengo makubwa zege inatengenezwa katika kituo au kiwanda cha pekee ikisafirishwa kwa lori; malori haya hubeba zege katika tangi inayozunguka kwa kusudi ya kuzuia kushikana kwa zege na tangi. Mahali pa ujenzi zege inamwagikwa au kupelewa kwenye ghorofa za juu kwa pampu maana zege bichi huwa na tabia ya kiowevu au tope. Kwa majengo madogo zege huchanganywa palepale; kwa kazi ndogo watu hukoroga saruji, mchanga na maji kwa mkoo katika sufuria kubwa. Kwa kawaida hutumia mashine inayozungusha sufuria kubwa na mchanganyiko hutengenezwa ndani yake.

Uharibifu wa zege[hariri | hariri chanzo]

Kutu kwenye vyuma vya ukuta wa zege; upanuzi wa vyuma umeshavunja sehemu ya ukuta

Majengo ya zege hudumu miaka mingi. Hadi leo kuna majengo ya Roma ya Kale yaliyotengenezwa kwa zege miaka 2,000 iliyopita. Lakini majengo ya kisasa mara nyingi huonyesha uharibifu kutokana makosa katika ujenzi, kasoro katika matumizi ya vipande vya mchanganyiko na sababu nyingine.

Mara nyingi tatizo kubwa ni kutu ya vyuma ndani ya zege. Hasa kama ganda la zege la nje ya vyuma ni nyembamba au mchanganyiko ulikuwa na kasoro unyevu wa maji unaweza kufika kwenye vyuma ndani ya zege. Hivyo vyuma vinaanza kushika kutu. Ilhali kutu inapanuka na kuhitaji nafasi zaidi kuliko chuma safi upanuzi huu unaweza kupasua zege na kusababisha kutokea kwa ufa na mashimo yanayoongeza kuingia kwa maji ndani ya ukuta na kutu zaidi.[2]

Sababu nyingine ni majengo yaliyo karibu na bahari na kushambuliwa na chumvi hewani; pia mvua asidi hushambulia zege na kuingia ndani yake kusababisha kutu.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. Uzalishaji wa saruji ya mwaka 2014 ulikuwa tani milioni 4,180, na karibu yote hutumiwa kwa matumizi katika mchanganyiko wa zege. Taz. Taarifa ya US United States Geological Survey 2015
  2. Majengo ya Waroma wa kale hayakuwa na vyuma vya kuimarisha zege; hivyo yalihitaji kuta nene zaidi lakini hayakuona uharibifu kutokana na kutu ndani ya ukuta

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Wikimedia Commons ina media kuhusu: