Yoga

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mazoezi ya Yoga katika kikundi

Yoga ni mazoezi ya kiroho na kimwili yenye asili katika falsafa ya Uhindi. Tangu miaka ya 1980 yoga ilisambaa pia nje ya Uhindi katika nchi za magharibi kama mazoezi ya kimwili. Katika utamaduni wa Kihindi yoga inatekelezwa pamoja na jitihada za kiroho na kidini kwenye msingi wa Uhindu na pia Ubuddha. Mtu anayefanya mazoezi ya yoga huitwa yogi.

Shabaha za Yoga[hariri | hariri chanzo]

Shabaha ya mazoezi ya yoga ni kujikamilisha kama binadamu mwenye mwili, nafsi na roho. Hapa ni wazo muhimu kutawala tamaa za mwili na roho zinazotazamiwa kama kizuizi kwenye njia ya kufikia ukamilifu. Kwa hiyo mwanafunzi wa yoga apate kujifunza nidhamu ya ndani na nidhamu ya kimwili.

Njia muhimu kuelekea shabaha hii ni kufanya mazoezi ya kudhibiti pumzi na kumakinisha fikra na hisia. Watendaji na walimu wa yoga huamini ya kwamba mazoezi haya yanachangia kwenye afya ya kimwili na kiroho. Kujifunza mikao fulani ya mwili ni mbinu ya kufikia shabaha za yoga.

Yoga katika Magharibi[hariri | hariri chanzo]

Yoga ilisambazwa na walimu kutoka Uhindini katika Ulaya na Marekani. Katika nchi hizi za magharibi ni zaidi mazoezi ya kimwili na elimu ya mikao yaliyopokelewa bila kuelewa asili katika roho ya Uhindu na falsafa yake. Yoga imependekezwa kama mbinu za kunpunza matatizo ya afya, kuimarisha musuli na hasa uti wa mgongo kwa watu wanaoketi muda mrefu ofisini, na kupunguza dhiki na shinikizo ya maisha ya kisasa (stress). Kwa hiyo matumizi yayoga inafanana kiasi na aina ya michezo.

Yoga na dini nyingine[hariri | hariri chanzo]

Kiasi mazoezi ya yoga yanaweza kufanana na taamuli za kiroho jinsi zinavyopatikana pia katika dini kama Ukristo na Uislamu.

Ubuddha[hariri | hariri chanzo]

Madhehebu kadhaa za Ubuddha yanajua mazoezi yanayofanana na yoga, hasa upande wa Zen. Hapa njia za kutawala pumzi na fikra zinafundishwa pia, pamoja na mikao mbalimbali ya mwili. Ilhali kulikuwa na kipindi ca athira kubwa ya Kibuddha katika Uhindi inawezekana ya kwamba sehemu za mazoezi ya Yoga zina asili katika Ubuddha.

Ukristo[hariri | hariri chanzo]

  • Kuna wakristo wanaotoa onyo dhidi ya matumizi ya yoga wakikazia asili yake katika Uhindu[1]
  • katika kanisa katoliki mazoezi ya yoga yametumiwa kwa idhini ya papa na maaskofu ndani ya mazoezi ya kiroho[2]

Uislamu[hariri | hariri chanzo]

  • walimu na viongozi mbalimbali wa Uislamu wamekataza matumizi ya yoga, kwa mfano Misri, Indonesia na Malaysia[3]
  • jumuiya za Wasufi wanatumia mbinu za kusimamia pumzi na mikao kadhaa yenye asili katika yoga. [4]

Mifano ya mazoezi ya yoga[hariri | hariri chanzo]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. Dr Ankerberg, John & Dr Weldon, John, Encyclopedia of New Age Beliefs, Harvest House Publishers, 1996
  2. Trying to reconcile the ways of the Vatican and of te East, New York Times January 7, 1990
  3. Fatwa ya Halmashauri Kuu ya Waislamu wa Malaysia inatangaza yoga kuwa haraam, ikitofautisha na mazoezi ya kimwili tu. Jalada kutoka ya awali juu ya 2008-12-22. Iliwekwa mnamo 2008-12-22.
  4. Carl W. Ernst, Situating Sufism and Yoga, review of article in Journal of the Royal Asiatic Society, Third Series, Vol. 15, No. 1 (Apr., 2005), pp. 15- 43. Jalada kutoka ya awali juu ya 2014-08-24. Iliwekwa mnamo 2015-05-21.

Kujisomea[hariri | hariri chanzo]