William Herschel

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Wilhelm - William Herschel mnamo mwaka 1785
Herschel jinsi alivyosafisha kiakisi cha darubini pamoja na dadake Caroline

Friedrich Wilhelm Herschel (kwa Kiingereza: Frederick William, 15 Novemba 173825 Agosti 1822) alikuwa mtungaji wa muziki na mwanaastronomia kutoka nchini Ujerumani aliyeishi na kufanikiwa Uingereza.

Alipata umaarufu hasa kama mgunduzi wa sayari ya Uranus. Kasoko moja kwenye Mwezi ilipewa jina la Kasoko ya Herschel kwa heshima ya michango wake, pamoja na kasoko kwenye Mirihi na kwenye mwezi Mimas wa Zohali.

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Herschel alizaliwa katika familia ya Walutheri katika utemi wa Hannover kwenye kaskazini ya Ujerumani[1]. Familia ilikuwa ya asili ya Kiyahudi kutoka Moravia. Babake alikuwa mwanamuziki katika bendi la jeshi la mtemi. Wakati ule watemi wa Hannover walikuwa pia wafalme wa Uingereza. Wilhelm alimfuata baba kama mpiga filimbi wa oboe na fidla kattika bendi ya kijeshi. Kwa njia hii kijana Wilhelm alifika Uingereza kwa umri wa miaka 19 alipobaki na kuendelea kuishi.

Herschel aliendelea na kazi ya muziki akaendelea kuwa kiongozi wa bendi hadi kushika nafasi ya mkurugenzi wa muziki katika mji wa Bath alipoishi pamoja na dadake Caroline. Alikuwa pia mpiga kinanda za filimbi kanisani. Alitunga muziki ya kiroho na ya burudani.

Tangu miaka ya 1770 alianza kushughulikia mambo ya hisabati alikovutwa kutokana na kazi ya kutunga muziki na kutafakari nadharia ya muziki. Kupitia rafiki mmoja alivutwa na astronomia. Alianza kutengeneza na kuuza vifaa vya darubini alizoweza kuboresha.

Mwaka 1780 aliweza kugundua sayari ya Uranus. Hii ilikuwa sayari ya kwanza iliyogunduliwa Tango nyakati ya kalte na hadi wakati ule haikujulikana. Ugunduzi huu ulisababisha kupokelewa kwake katika Shirika la Kifalme la Sayansi pamoja na mshahara uliomwezesha kutumia wakati wake kwa sayansi. Katika miaka iliyofuata alichaguliwa kama mwanachama katika shirika mbalimbali za kisayansi za Ujerumani na Marekani. Mnamo 1820 alikuwa mwenyekiti wa kwanza wa Shirika la Kifalme la Astronomia la Uingereza. Alipokufa mwaka 1822 marafiki waliweka kwenze jiwe la kaburi yake maneno ya Kilatini "Caelorum perrupit claustra" (Alivuka mipaka ya anga)

Kazi ya astronomia[hariri | hariri chanzo]

Herschel alitumia vifaa vyake aliyoboresha mwenyewe kwa kuchungulia upya nyota zote. Baada ya kugundua Uranus aligundua pia miezi yake miwili pamoja na pete za sayari hii. Aliendelea kutambua miezi miwili ya Zohali.

Alikuwa mtafiti wa kwanza aliyechungulia spektra ya nuru ya nyota. Alikuwa pia wa kwanza wa kutambua mnururisho wa infraredi katika nuru ya Jua.

  1. leo katika Jimbo la Saksonia Chini