Wikipedia:Makala ya wiki/Rugaruga
Rugaruga ilikuwa jina kwa aina mbalimbali ya askari wa kienyeji katika Afrika ya Mashariki wakati wa karne ya 19 na 20. Jina "Rugaruga" lilikuwa maarufu tangu miaka ya 1860 kama jina la askari wa Mirambo aliyekuwa mtemi wa Wanyamwezi katika magharibi ya Tanzania ya leo.
Mirambo aliwahi kutajirika kama mfanyabiashara kwa njia ya misafara kati ya pwani la Bahari Hindi na Kongo. Alitumia sehemu kubwa ya utajiri wake kujenga jeshi la binafsi. Kwa kusudi hii alinunua bunduki aina ya magobori na kukusanya vijana wengi walioitwa "rugaruga". Kwa kawaida vijana hao walikuwa wanaume walioishi bila ukoo na bila familia waliowahi kutoroka kwenye hali ya utumwa au kuwa wapagaji wa misafara. Mirambo aliwapokea na kuwapa silaha na kwa njia hii alishinda maadui hadi kuwa mtemi mkuu wa Waynamwezi kuanzia 1860 hadi kifo chake mnamo 1884. Rugaruga hawa walihofiwa kote na Mirambo aliweza kupanusha eneo lake kwa msaada wao. Inasemekana ya kwamba kabla ya mapigano walipewa pombe na banghi kwa kusudi ya kuongeza ukali na kupunguza hofu yao ya kifo. Kutokana na askari wa Mirambo jina la "Rugaruga" lilijulikana kote likawa kawaida kwa askari wa watawala wengi. Wajerumani walipotwaa eneo la Afrika ya Mashariki ya Kijerumani walikuta neno hili mahali pengi lilikuwa njia ya kutaja askari au mapolisi wa kienyeji. ►Soma zaidi