Nenda kwa yaliyomo

Sleji

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Sleji inayovutwa na mbwa nchini Kanada
Sleji inayovutwa na farasi nchini Ujerumani
Watoto wanaosukumana kwa sleji nchini Sweden
Sleji ya injini inaendeshwa kama pikipiki


Sleji ni kitolori bila magurudumu kinachovutwa na wanyama au watu kikiteleza hasa juu ya theluji au barafu. Ni chombo cha usafiri kikuu kati ya Eskimo wa nchi za aktiki. Ni usafiri wa kawaida pia katika sehemu nyingine baridi penye theluji nyingi. Ni pia chombo cha michezo au burudani pale ambako theluji inapatikana kwa muda fulani tu.

Kuna pia aina za sleji zinazotumiwa pasipo na theluji lakini kwa kawaida magari yenye magurudumu yalichukua nafasi zao.

Muundo[hariri | hariri chanzo]

Sleji huteleza juu ya uso wa ardhi lakini haina magurudumu. Kwa hiyo ni lazima kupunguza msuguano wake kwa kupunguza eneo la kugusana kati ya sleji na uso wa ardhi. Njia ya kawaida ilikuwa kutumia bao nyembamba kama miguu iliyobeba sleji juu yake. Ni sharti kusugua uso wa bao hizi hadi ni nyororo kabisa. Kwa kuimarisha bao mara nyingi kanda ya chuma hufungwa chini yake na sasa sleji inateleza juu ya kanda nyembaba ya chuma pekee.

Waeskimo walitumia mara nyingi mifupa mirefu ya nyangumi kama miguu ya sleji.

Siku hizi sleji za burudani mara nyingi hutengenezwa kwa plastiki.

Mwendo[hariri | hariri chanzo]

Njia za kuendesha sleji ni kuivuta, kuisukuma au kuteleza kwenye mtelemko.

Sleji husukumwa na watu wakisafirisha mizigo, watu wengine au kujisukuma wenyewe. Kujisukuma wenyewe hutokea kama mguu mmoja unasimama juu ya mhuu wa sleji na mguu mwingine unafanya kazi ya kusukuma.

Kuvuta unaweza kufanywa na mtu lakini kuna pia sleji zinazovutwa na wanyama hasa mbwa au farasi.

Tangu karne ya 20 sleji za injini zimepatikana. Zinalengwa kwa miguu kama sleji ya kawaida lakini mwendo unapatikana kwa njia ya magurudumu na mnyororo.

Sleji pasipo na barafu[hariri | hariri chanzo]

Inajulikana ya kwamba Wamisri wa kale walitumia sleji kwa kuvuta mawe makubwa hadi mahali pa ujenzi wa piramidi. Inaaminiwa ya kwamba walitumia maji na mafuta chini ya miguu ili kupunguza msuguano kwenye ardhi.

Katika mchanga msuguano ni mdogo. Kwa hiyo kuna sleji za mchanga hadi leo hasa kwa burudani na michezo ingawa si kawaida kama sleji za theluji.

Wenyeji wa Hawaii walitumia aina za sleji kwa kuteleza mitelemko ya milima yao; waliweza kuteleza juu ya manyasi mabichi au pia juu ya mchanga kwenye mitelemko na walifanya hivyo kama burudani na kwa mashindano kati ya vijana.

Michezo na burudani[hariri | hariri chanzo]

Mashindano ya mbio kwa sleji ni sehemu ya michezo ya Olimpiki tangu 1964. Kwenye njia za barafu zenye mteleko mkali sleji zinafikia mkasi wa 150 km/h au zaidi. Kwa hiyo ni mchezo wa hatari kiasi na ajali zimetokea mara kadhaa ambako watu wamekufa.

Katika nchi nyingi penye kipindi cha barafu na theluji watoto huwa na sleji ndogo wanazitumia kuteleza chini kwenye mitelemko ya vilima.