Simfoni

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Simfoni (kutoka Kigir. σύμφωνος simphōnos ‚sauti za pamoja‘ kupitia Kiitalia sinfonia) ni muziki iliyoandikwa kwa ajili ya okestra.

Aina hii ya muziki ilianzishwa huko Italia katika karne ya 17. Hapa jina "sinfonia" lilibuniwa. Hadi leo hii majina ya mitindo mbalimbali inayotumia ndani ya sinfonia ni ya kiitalia.

Kwa kawaida kuna sehemu tatu au nne zinazotofautishwa kwa kasi na tabia ya muziki, kwa mfano haraka-polepole-haraka au kinyume chake polepole-haraka-polepole. Watungaji muziki kama Joseph Haydn (simfonia 104), Wolfgang Amadeus Mozart (simfonia zaidi ya 50) na Ludwig van Beethoven (simfonia 9) waliboresha na kukamilisha muziki dhati ya simfonia. Beethoven alikuwa mtungaji wa kwanza aliyeingiza pia sauti za kibinadamu katika simfonia yake ya 9.

Mitindo inayotumiwa ndani ya sehemu za simfonia ni pamoja na sonata, minuet, scherzo au rondo.

Okestra kubwa mara nyingi huitwa "okestra ya simfonia" wakati okestra ndogo huitwa "okestra ya chumba".

Watungaji mashuhuri wengine wa simfonia walikuwa Franz Schubert, Felix Mendelssohn, Robert Schumann, Anton Bruckner, Johannes Brahms, Pyotr Tchaikovsky, Gustav Mahler, Jean Sibelius na Dmitri Shostakovich.