Nenda kwa yaliyomo

Shelly-Ann Fraser

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mwanariadha Shelly-Ann Fraser Jamaika
Uzalendo: Jamaika
Mbio: 100m
Klabu: MVP Track & Field
Pahali pa kuzaliwa: Kingston,Jamaika
Siku ya Kuzaliwa: 27 Desemba 1986
Urefu: 1.60m
Uzito: 52kg
Rekodi za medali
Anawakilisha nchi Jamaika
Riadha ya Wanawake
Michezo ya Olimpiki
Dhahabu 2008 Beijing Mbio ya mita 100
Mashindano ya Mabingwa wa Dunia ya IAAF
Dhahabu 2009 Berlin Mbio ya 100 m
Dhahabu 2009 Berlin Mbio ya 4 x 100m
Fedha 2007 Osaka Mbio ya 4 x 100m

Shelly-Ann Fraser, OD (alizaliwa 27 Desemba 1986) ni mwanariadha wa nchi ya Jamaika ambaye amebobea katika mbio ya 100m. Alizaliwa katika jiji la Kingston, Jamaika, Fraser ndiye bingwa mtetezi wa Olimpiki na Dunia katika mbio ya 100m, akikimbia katika muda wa 10.78s (Olimpiki) na 10.73s (Dunia). Yeye ndiye mwanamke pekee aliyeshikilia mataji ya ubingwa wa Olimpiki na Dunia yote mawili kwa wakati mmoja. Ametoshana na Christine Arron kama mwanamke wa nne wa kasi kabisa katika historia ya mbio ya 100m. Alisoma katika Shule ya Upili ya Wolmer's ya Wasichana na akawakilisha shule yake katika mashindano mengi ya riadha.

Olimpiki ya 2008 ya Beijing

[hariri | hariri chanzo]

Fraser alifanya mazoezi ya kabla ya Olimpiki pamoja na mwenzake Mjamaika, Asafa Powell. Alikuwa mwanamke wa kwanza wa Jamaika kushinda medali ya dhahabu katika mbio ya Olimpiki ya 100m. Katika mbio ya awamu ya kwanza ya kuhitimu, alikimbia na kuwa wa kwanza kwa muda wa sekunde 11.35 na kufaulu kuingia mbio ya awamu ya pili. Aliboresha muda wake kuwa 11.06s huku akimaliza katika nafasi ya kwanza tena katika awamu ya pili. Alimaliza katika nafasi ya kwanza katika mbio ya nusu fainali, akiwashinda Muna Lee na Lauryn Williams katika muda wa sekunde 11.00.

Katika mbio ya fainali, wanariadha wa Jamaika walimaliza katika nafasi tatu za kwanza. Washindi wa nafasi ya pili walichaguliwa kwa kutumia usaidizi wa picha na wakawa Sherone Simpson na Kerron Stewart. (Wanawake hawa wawili walituzwa medali za fedha; medali ya shaba haikutuzwa yeyote.) Muda wa Fraser ulikuwa muda bora wa kibinafsi wa sekunde 10.78, sekunde 0.20 kasi kuliko Wajamaika wenzake(Simpson na Stewart). Muda wake wa Olimpiki ulikuwa wa pili kwa kasi katika mbio ya 100m uliokimbiwa na mwanamke Mjamaika, ulishindwa na sekunde 0.04 na ule wa rekodi ya Merlene Ottey ya 10.74s.

Akiwa pamoja na Sheri-Ann Brooks, Aleen Bailey na Veronica Campbell-Brown alihusika katika mbio ya 4 x 100. Katika raundi ya kwanza, Jamaika ilishinda Urusi,Ujerumani na Uchina. Muda wa Jamaika ulikuwa muda wa sekunde 42.24 ambao ulikuwa muda bora kabisa kati ya muda za mataifa kumi na sita yaliyoshiriki. Kutokana na matokeo hayo, timu ya Jamaika ilihitimu kushiriki katika fainali, Brooks na Bailey wakibadilishwa na Sherone Simpson na Kerron Stewart. Hata hivyo ,wanariadha wa Jamaika hawakumaliza mbio hiyo kutokana na kosa la kubadilisha kijiti maalum kati ya wanariadha wao wawili.

Mashindano ya Mabingwa wa Dunia ya 2009 Berlin

[hariri | hariri chanzo]

Fraser alishinda taji la mbio ya 100m la Jamaika katika mwezi wa Juni 2009, akishinda kwa muda wa 10.88s dhidi ya upepo mkali (-1.5 m/s). Hii ilimfanya kuhitimu kushiriki katika Mashindano ya Mabingwa wa Dunia ya 2009. Fraser alikimbia mbio sana akimshinda mshindani mwenzake wa Jamaika , Kerron Stewart, aliyekuwa akimkaribia sana katika mbio hiyo. Alishinda mbio hiyo kwa muda wa sekunde 10.73 - muda wa kasi wa nne katika historia ya mashindano hayo na muda huu ndio rekodi ya Jamaika ya hivi sasa.

  1. ^ a b Fraser Expects Great Results in 100 Metres, Jamaica Observer,
  2. ^ Jamaica's Shelly-Ann Fraser wins Women's 100m Olympic gold Ilihifadhiwa 1 Desemba 2008 kwenye Wayback Machine.
  3. ^ "Smiling Fraser just loves to make Jamaica happy" Ilihifadhiwa 13 Juni 2012 kwenye Wayback Machine.. (2009-08-18). International Association of Athletics Federations.
  4. ^ a b Athlete biography: Shelly-Ann Fraser, beijing2008.cn,
  5. Foster, Anthony (2009-06-28). Bolt 9.86 and Fraser 10.88; Walker and Phillips excel over hurdles - JAM Champs. IAAF. Retrieved on 2009-06-28.

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]