Shaykh 'Abdullaah Swaalih Al-Farsy
Shaykh 'Abdullaah Swaalih Al-Farsy (12 Februari 1912 - 9 Novemba 1982) alikuwa mwanazuoni na mwanahistoria mkubwa wa Kiislamu na mmojawapo wa washairi wakubwa kutoka Zanzibar lakini baadaye alihamia Mombasa, Kenya kwa kuhofia kukamatwa na serikali ya Zanzibar.
Alifahamika zaidi kwa kutafsiri Qurani kwa Kiswahili. Vilevile alipata kuwa Kadhi Mkuu wa Zanzibar.
Alikuwa mtu mwenye kupendwa na watu, akizungukwa mara nyingi na watu wanaotaka kumsalimia au kupata kutoka kwake mafunzo ya dini.
Umaarufu wake ulikuwa si katika kisiwa cha Zanzibar na nchi za Afrika ya Mashariki peke yake, bali ulienea hadi Somalia, Cape Town upande wa kusini mpaka kufikia Malawi, mahali alipokuwa akitoa darsa zake kabla ya kuhamia Kenya.
Wasifu
Alizaliwa Zanzibar mwezi wa Februari mwaka 1912 katika ukoo maarufu, akajifunza Qur-aan kutoka kwa Fatma Hamid Said (1854-1936), aliyesoma kwa Shaykh Amin bin Ahmed aliyekuwa akifundisha Qur-aan kijiji cha Jongeani mahali alipozaliwa Shaykh Abdullah Farsy na kukulia.
Shaykh Abdullah Saleh Farsy alihifadhi Qur-aan yote pamoja na hadithi nyingi za Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) akiwa na umri mdogo sana, na shauku yake kubwa isiyotoshelezeka ya kujifunza masomo ya Kiislamu na ya kiulimwengu ilionekana pale wenzake walipokuwa wakijishughulisha na michezo na anasa za kidunia, wakati yeye alikuwa kila siku akizama katika kusoma kitabu kipya cha mafunzo ya Kiislamu.
Alikuwa akipenda sana kusoma, kiasi ambacho maisha yake yote yalifungika ndani ya maktaba yake kubwa ya nyumbani.
Alipofariki dunia, Shaykh Abdullah Saleh al-Farsy alikuwa Aalim mwenye kutambulika na kuheshimika kupita wote katika nchi zinazotumia lugha ya Kiswahili. Mchango wake usiokuwa na mfano katika kuelimisha watu dini ya Kiislamu ulifikia kiwango chake cha juu baada ya kuchapicha tafsiri kamili ya mwanzo ya Qur-aan Takatifu ya Kiswahili iliyokubaliwa rasmi yenye kurasa 807.
Elimu yake
Alipokuwa kijana, mwanachuoni huyu mwenye hamasa na uhodari alibahatika wakati ule kuwepo na kuenea kwa vyuo vikongwe vya Kiislamu vilivyojaa wanafunzi chini ya uongozi wa Maulamaa weledi mfano wa Shaykh Abu Bakar bin Abdullah bin Bakathir (1881-1943) aliyekuwa mwanafunzi maarufu wa Sayyid Ahmed bin Abu Bakar al-Sumait (1961-1925)
Katika mwaka wa 1922 Shaykh Abdullah Saleh Farsy alijiunga na chuo cha Msikiti Barza baada ya Maulamaa wawili kumtaka afanya hivyo: Wa kwanza alikuwa Sayyid Hamid bin Mansab (1902-1965) aliyemfunza RISALATUL JAMI'A, yenye mafunzo ya taasisi ya Kiislamu. Imamu huyu wa msikiti wa Forodhani aliyefariki dunia wakati akitoa darsi ndani ya msikiti Gofu alikuwa mwanafunzi wa Shaykh Muhammad Abdul Rahman Makhzymy (1877-1946), mmojawapo wa waalimu wa Shaykh Abdullah Saleh Farsy. Wa pili alikuwa Sayyid Alawy bin Abdul Wahab (1902-1960) aliyemsomesha vitabu 12 vya Fiq'hi katika lugha ya kiarabu pamoja na sharhi ya MATNI YA RAHABIYYAH juu ya elimu ya urithi.
Baada ya kuwa mjuzi katika elimu ya taasisi ya Kiislamu katika chuo cha Msikiti Barza, Shaykh Abdullah Saleh Farsy alikuwa mjuzi pia wa elimu ya nahau ya lugha ya Kiarabu. Na alipokuwa na umri wa miaka 20 alikuwa akiandika mashairi ya Kiarabu, dalili ya daraja kubwa ya elimu ambayo Maulamaa wa Zanzibar wakati ule waliweza kuieneza.
Shaykh Abdullah Saleh Farsy alijifunza chini ya Maulamaa wengi wakubwa kama vile Shaykh Ahmed bin Muhammad al-Mlomry (1873-1936) aliyemfundisha vitabu 25 vikiwemo Tafsiri ya Jalalayn kilichoandikwa na Jalal al-Din Mahali (1389-1450) kutoka Misri na Jalal al-Din Suyuti (1445-1505), Syria, na hawa ni Maulamaa wakubwa na maarufu wa madhehebu ya Imam Shafi.
Baada ya kuhitimu darsi zote katika chuo cha Msikiti Barza, Shaykh Abdullah Saleh Farsy aliruhusiwa na Shaykh Ahmed bin Muhammad al-Mlomry kusomesha katika chuo hicho katika mwezi wa Ramadhan chini ya uangalizi wake.
Alijifunza pia kutoka kwa Shaykh Abu Bakar (1881-1943), mtoto wa Shaykh Abdullah bin Abu Bakar Bakathir (1860-1925), mwanafunzi wa Shaykh Ahmed bin Abu Bakar al-Sumait.
Shaykh Abu Bakar bin Abdullah bin Bakathir aliyejifunza kutoka kwake elimu ya Fiq'hi kupita Maulamaa wengi hapo Zanzibar, alikuwa akihudhuria darsi za Shaykh Abdullah Saleh Farsy kwa ajili ya kumpa moyo, kisha akamchagua kuwa Imamu wa Swalah ya Witri kutoka mwaka 1933 mpaka terehe 28 Oktoba 1939, alipomruhusu pia kusoma Qur-aan katika Msikiti Gofu na hatimaye akawa anasalisha Swalah ya Alfajiri mpaka mwaka 1966 alipochukuwa mahali pake mtoto wa dada yake Saleh bin Salim bin Zagar.
Shaykh Abdullah Saleh Farsy alisoma vitabu vingi vya Fiq'hi kutoka kwa Shaykh Muhammad Abdul Rahman al-Makhzymy vikiwemo vitabu vya Fathul Muin na Iqnai, ambavyo mwanzo vilikuwa vikisomeshwa na Shaykh Abdullah bin Abu Bakar bin Bakathir hapo Msikiti Gofu katika mwaka 1917. Alijifunza kutoka kwake pia elimu ya kupanga nyakati za Swalah na kuujua upande wa Qiblah.
Juu ya kuwa hapo mwanzo Shaykh Abdullah Saleh alisoma Minhaaj At Talibiiyn kitabu cha Shaykh Zakariya Muhyddin Yahya Sharaff ad-Din al-Nawawi (1213-1277) ambaye ni mwanachuoni mkubwa wa madhehebu ya Kishafi, lakini baadaye alisoma tena kitabu hicho kwa Shaykh Muhammad Abdul Rahman al-Makhzymy.
Msimamo wa kisheria wa kitabu hiki hapo Zanzibar umeanzia zama za Imam Abu Hamid bin Muhammad al-Ghazzali (1058-1111), aliyekuwa mwanafunzi wa Imam wa Haramayn Ahmed Malik al-Jawayti (1085) kutoka kwa Ayoub al-Buwati (845), mwanafunzi wa Imam Muhammad Idriys al-Shafi'i (767-820), mwanzilishi wa Madrasa ya Shafi'i, yenye wafuasi wengi Zanzibar na Misri.
Shaykh Muhsin bin Ali bin Issa Barwan aliyekuwa mwalimu wake Msikiti Gofu, alikuwa mwanachuoni wa mwanzo katika mwaka 1944 kumruhusu Shaykh Abdullah Saleh Farsy kusomesha Jalalayn Msikiti Barza katika mwezi wa Ramadhani. Baadaye Shaykh Abdullah Saleh Farsy alijifunza kwa Shaykh al-Amin Ali bin Abdullah bin Nafi al-Mazrui mwaka (1875-1947), aliyeupendezesha kwa watu Uislamu wa kisasa kama ulivyoshereheshwa na Shekh Muhammad Abduh (1845-1905), aliyemsomesha Shaykh Ahmed Muhammad Mlomry katika chuo kikuu cha al Azhar, Misri.
Shaykh Abdullah Saleh Farsy alipewa Ijaza (shahada) na Shaykh ‘Umar bin Ahmad bin Abu Bakar al-Sumait (1896) aliyemsomesha vitabu vya Fiq'hi, Mantiq (Logic) na Hadith, pamoja na vitabu vingine. Bahati mbaya mwanachuoni huyu alirudi Yemen katika mwaka wa 1965 kutokana na udikteta uliokuwepo Zanzibar chini ya serikali iliyoongozwa na mkiristo Julius Kambarage Nyerere.
Umahiri aliouonyesha Shaykh Abdullah Saleh Farsy katika elimu ya mambo ya kidunia ulikuwa mkubwa pia. Alikuwa hodari sana katika elimu hiyo, na alipokuwa Central Primary School aliyojiunga nayo mwaka 1924, mwalimu wa lugha ya Kiingereza alishindwa kuamua darasa lipi ampeleke. Shaykh Abdullah Saleh Farsy aliyemaliza miaka minane inayotakiwa katika shule ya msingi katika muda wa miaka mitano tu.
Miongoni mwa walimu wake maarufu alikuwa Shaykh Abdullah bin Ahmed bin Seif (1900-1940) na Shaykh Abdul Bary kutoka chuo kikuu cha Al-Azhar aliyeajiriwa na Sayyid Ali bin Humoud mwaka (1902-1911).
Elimu juu ya Quran
Aliandika tafsiri yake ya Qur-aan Takatifu kuanzia mwaka wa 1950 hadi mwaka 1967, wakati fikra za umoja wa Kiislamu na Uislamu wa kisasa ulipokuwa ukifanyiwa kampeni kubwa hapo Zanzibar.
Wakati huo huo Tafsiri hii ilikuwa ni jibu la tafsiri ya Qur-aan Tukufu aliyoiandika Padri Godfrey Dale kwa ajili ya kuwawepesishia wahubiri wa Kiafrika walioajiriwa na University Mission to Central Africa (UMCA), iliyoanzishwa mwaka 1873 na David Livingstone (1813-1873) huko Zanzibar.
Tafsiri ya Padri Dale iliyoandikwa kwa Kiswahili cha Kiunguja ilikuwa na kurasa 542 pamoja na kurasa 142 za sharhi, ilipigwa chapa mwaka 1923 huko London na jumuiya ya kueneza elimu ya Kikristo (Society for Promoting Christian Knowledge).
Kwa vile tafsiri hiyo iliandikwa kwa njia ya kuutetea Ukristo, jambo lisilokubalika kwa Waislamu, Shaykh Mubarak bin Ahmed bin Ahmad, mkuu wa Makadiani Afrika Mashariki (Ahmadiyah Muslim in East Africa) aliamua kuanza kuandika tafsiri yake mwaka 1936 iliyokubaliwa na kutambuliwa na wamisionari hapo Zanzibar.
Katika mwaka 1942 nakala ya tafsiri ya Makadiani iliyopigwa taipu ilipelekwa mbele ya kamati ya lugha ya Kiswahili (Inter-Territorial (Swahili) Language) kwa ajili ya kukubaliwa rasmi kilugha. Na katika mwezi wa Aprili mwaka 1944, kamati ilijibu kwa kuikubali lugha iliyotumika ikitaka baadhi ya marekebisho kufanyika. Juu ya kuwa masahihisho yote hayakufanyika kama ilivyotakiwa, tafsiri hiyo ikapelekwa mbele ya baadhi ya viongozi wa Makadiani wa Afrika ya Mashariki na kukubaliwa kuwa lugha iliyotumika ni nzuri na yenye kukubalika.
Shaykh Amri bin Abeid (1924-1964), aliyejifunza Ukadiani huko Pakistan mwaka (1954-1956) alijaribu kuitetea tafsiri ya Makadiani, lakini tafsiri hiyo iliyopigwa chapa kwa mara ya mwanzo mwaka 1953 ilisababisha mgogoro mkubwa kutoka kwa Masunni waliowatuhumu Makadiani kuwa wamebadilisha na kugeuza baadhi ya maneno kwa kusudi la kuunga mkono fikra zao.
Ili kupambana na tafsiri za Wakristo na Makadiani zilizogeuzwa na kubadilishwa ilionekana kuwepo umuhimu na dharura ya kupatikana tafsiri yenye kutambuliwa rasmi. Jukumu hilo akabebeshwa Shaykh Abdullah Saleh Farsy, aliyekuwa akimuomba Mwenyezi Mungu ampe umri mrefu asife kabla ya kuikamilisha tafsiri hiyo.
Fikra hii adhimu ilianza baada ya Shaykh kupiga chapa kitabu chake cha mwanzo kiitwacho 'Maisha ya Mtume Muhammad' (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) kilichofuatiliwa na kitabu cha Sura za Swalah na Tafsiri zake mwaka (1950).
Kabla ya kudhihirisha kutoridhika kwake na tafsiri ya Makadiani katika kijitabu kidogo ‘Upotofu wa Tafsiri ya Makadiani’, Shaykh Abdullah Saleh alikwishawahi kuandika tafsiri na sharhi ya Surah Yaseen, Al-Waqiah na Al- Mulk kilichopigwa chapa na A.A. Vasingstake, Uingereza na kutolewa mwaka 1950 Zanzibar.
Tafsiri yake aliyoiandika kwa kuitegemea zaidi tafsiri ya Jalalayn ilianza kupigwa chapa juzuu baada ya juzuu, na baina ya mwaka 1956 na 1961 juzuu kumi na mbili zilikwishapigwa chapa.
Kutokana na upungufu wa fedha, tafsiri iliyokamilika ilipigwa chapa mwaka 1969 na wadhamini walikuwa The Islamic Foundation. Msaada mkubwa uliotolewa na Sultani wa Qatar, Shaykh Ahmad bin Ali uliwezesha kugawiwa bure misahafu 4,000 na kuuzwa misahafu mingine 3,000 kwa bei nafuu ya shilingi kumi tu.
Kuanzia mwaka 1950 hadi 1960 kampeni kubwa dhidi ya Makadiani ilifanywa na Jamaat al Islam huko Pakistan chini ya uongozi wa Shaykh Maududi (1903-1979) aliyezikaribisha juhudi kubwa za Shaykh Abdullah Saleh Farsy, juu ya khitilafu iliyokuwepo baina ya misimamo ya Zanzibar na Pakistani, kwani Shaykh Abdullah Saleh Farsy hakuwa akiona tofauti yoyote baina ya Makadiani na Ahmadiya waliojitenga na Makadiyani. (Ahmadiya ni kundi lililojitenga na Makadiani kutokana na baadhi ya khitilafu baina yao) Islamic Foundation ya Nairobi yenye kuunga mkono Jamaat al Islam ya Pakistan, ndiyo iliyopiga chapa kwa mara ya mwanzo Tafsiri ya Shaykh Abdullah Saleh Farsy, aliyeandika kuwa Maududi ameikubali tafsiri yake ya QURANI TAKATIFU. Na Shaykh Abdullah Saleh Farsy naye alieleza kuikubali kwake tafsiri ya Maududi inayoitwa 'Qur'an Fahmi Ke Bunyadi Usul' (Msingi wa kuifahamu Qur-aan), na akaruhusu uandikwa utangulizi wa Tafhim Al-Qur-aan katika Qurani Takatifu.
Mafundisho yake
Kuanzia tarehe 7 Januari 1960 hadi 19 Februari 1960 Shaykh Farsy alikuwa safarini Nyasaland 'Malawi' na Rhodesia ya Kusini akitoa darsa na kuwahutubia Waislamu na kuwanasihi juu ya umuhimu wa kujifunza masomo ya dini.
Tarehe 11 Aprili 1960 baada ya kurudi kutoka Nyasaland, Shaykh Farsy aliandika ripoti aliyoeleza ndani yake umuhimu wa mafunzo ya dini. Aliwataka wanaohusika kutilia nguvu umuhimu wa kuwapatia Waislamu elimu katika skuli za serikali.
Aliandika: "Kwanza, upeo wa elimu ya watoto wa Kiislamu ni duni ukilinganisha na wasiokuwa Waislamu katika Nyasaland. Kuwepo kwa jamii mbili katika nchi, mojawapo imeelimka na nyengine haijaelimika ni hatari kwa serikali na kwa jamii. Serikali ni baba wa wananchi wote, na kwa ajili hiyo inapaswa kutopendelea upande mmoja."
Aliendelea kueleza: "Serikali inatoa misaada mbali mbali kuipa skuli za wamishionari bila ya kuzilamisha kujiunga na skuli za serikali. Jukumu la serikali ya Nyasaland lazima liwe kuinyanyua daraja ya elimu kwa Waisalmu iwe sawa na ile ya jamii nyingine nchini.”
Matakwa ya Shaykh Farsy juu ya kuelimishwa Waislamu hayakuwa kutaka wajengewe skuli zao tu, bali yalikuwa makubwa kuliko hivyo. Alitilia mkazo jambo la kuajiriwa waalimu wa dini ya Kiislamu katika skuli za serikali pia. Alisema: "Shule za serikali hazina budi kuwa na walimu watakaosomesha mafunzo ya Kiislamu wenye kulipwa na serikali. Inashangaza kuona kuwa waalimu wa Kikristo katika shule hizo wanalipwa na serikali wakati waalimu wa Kiislamu wanalipwa na jamii. Haya hayafahamiki."
Kupitia darsi zake za misikitini na kwa njia ya vitabu, Shaykh Farsy alitumia juhudi zake zote katika kuwaelimisha vijana misingi asili ya Kiislamu. Alihimiza na kutilia nguvu umuhimu wa kufufua, kufuata na kuyafahamu mafundisho sahihi ya dini kama yalivyokuwa wakati wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) na Sahaba zake (Radhiya Llahu anhum) pamoja na mafundisho ya watu wema waliotangulia 'Salafus Swaalih'.
Mafundisho haya yalikuwa yakifundishwa kabla yake na Shaykh Al-Amin na Shaykh Muhammad Kassim hapo Mombasa. Lengo la Shaykh Farsy lilikuwa kubwa kupita wadhifa wake wa Kadhi mkuu wa Kenya. Lengo lake lilikuwa ni kupata jukwaa litakalomwezesha kuifufua na kuieneza elimu sahihi ya dini kama ilivyokuwa wakati wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam), na kuwakataza watu kufuata uzushi ‘bid’aah’ na itikadi zisizo na misingi ya Kiislamu, na mambo yaliyo batili ambayo hao wanaoyaeneza wanajaribu kuyanasibisha na Uislamu.
Shaykh Farsy alifanikiwa kiasi kikubwa sana, na watu wengi waliokuwa wakihudhuria darsa zake walikuwa wakihisi kuwa mafunzo yake yanaingia moja kwa moja ndani ya nyoyo zao. Kwa juhudi zake, alifanikiwa kuanzisha kizazi kilichoiendeleza kazi yake hiyo ya kupiga vita uzushi na ushirikina, na kufanikiwa kuondoa itikadi nyingi ambazo watu wakati huo walikuwa wakidhani kuwa yamo katika dini.
Safari zake
Baada ya kukamilisha masomo yake katika Chuo cha Ualimu 'Teachers Training College (TTC)', Shaykh Abdullah alisomesha shule za msingi kuanzia mwaka 1932 hadi 1947, na kutokana na jitihada zake kubwa katika kazi, alipewa cheo cha Mkaguzi mkuu wa shule za msingi za Unguja na Pemba kuanzia mwaka 1949 hadi mwaka 1952. Kisha akapewa cheo cha Principal wa Muslim Academy Secondary School kuanzia mwaka 1952 hadi 1956 kabla ya kuchaguliwa kuwa Mwalimu mkuu 'Headmaster' wa Arabic Medium School kuanzia mwaka 1957 hadi 1960.
Mwezi wa Machi mwaka 1960, Shaykh alikwenda kuhiji na katika mwaka wa 1967 alijiuzulu kazi katika Wizara ya Elimu alipokuwa mwalimu katika Chuo cha Ualimu 'Teachers' Training College.
Katika mwaka 1960, alichaguliwa kuwa Kadhi mkuu wa Zanzibar, na aliendelea na kazi hiyo muda wa miaka saba, mpaka alipoamua kuiacha na kuhamia Kenya baada ya mapinduzi ya 12 Januari 1964 yaliyosababisha umwagaji mwingi wa damu huko Zanzibar pamoja na kukamatwa na kutiwa ndani bila sababu kwa viongozi wengi wa kisiasa na wa kidini.
Mwenyeji wake huko Kenya alikuwa Shaykh Muhammad Kassim al-Mazrui, sahibu yake wa zamani tokea waliposoma pamoja chini ya mwalimu wao Shaykh al-Amin bin Ali al-Mazrui, aliyekuwa akifundisha dini huko Zanzibar.
Shaykh Abdullah Saleh Farsy hakuwa mgeni huko Kenya ambako sifa zake kuwa mwanachuoni mkubwa zilitangulia kufika kabla yake. Shaykh Muhammad Kassim al-Mazrui ndiye aliyempendekeza kwa Rais Jomo Kenyatta kupewa cheo cha Kadhi mkuu wa Kenya, jambo ambalo Rais Kenyatta alilikubali bila kipingamizi.
Kwa muda wa miaka 14 alikuwa Kadhi mkuu wa Kenya, daraja yenye heshima kubwa sana aliyoitumikia kwa muda wote huo kwa ikhlasi, hekima, uwezo wa hali ya juu, na uerevu mkubwa sana mpaka alipoamua kustaafu katika mwaka 1980.
Kifo chake
Shaykh Abdullah Saleh Farsy alifariki dunia tarehe 9 Novemba mwaka 1982 karibu miezi minane tokea alipoondoka Kenya kuelekea Muscat - Oman kwa ajili ya kuungana na aila yake.
Huzuni kubwa iliyoingia nyoyoni mwa Waislamu wa Afrika Mashariki kutokana na kifo chake itaendelea muda mrefu sana, na pengo lake kamwe si rahisi kuzibika, na watu wataendelea kufaidika na elimu aliyowarithisha daima milele.
Nyadhifa zake
- Mwalimu – Shule za msingi (1932 - 1947)
- Mkaguzi mkuu wa Shule za Msingi - Zanzibar na Pemba (1949 - 1952)
- Principal - Muslim Academy Secondary School (1952 - 1956)
- Mwalimu mkuu - Arabic Medium School (1957 - 1960)
- Kadhi mkuu wa Zanzibar (1960 - 1967)
- Mwalimu - Teacher Training College (? - 1967)
- Kadhi mkuu wa Kenya (1974 - 1980)
Darsa zake
Alipokuwa Mombasa, Kenya Shaykh Farsy alikuwa akitoa darsa zake katika misikiti ifuatayo:
- Msikiti Sakina (Majengo) kila Jumanne
- Msikiti Al-Azhar (Guraya) kila Al Khamisi
- Msikiti Shihab (Mwembe Tayari) kila Jumatano
- Msikiti Mlango wa papa (mji wa Kale) Jumatatu
- Msikiti Ridhwaan (King’orani) Ijumaa
- Msikiti Muhammad Rashid (Kaloleni Mazui) Jumatatu-mara moja kila mwezi
- Tunah (Majengo) Ijumaa moja
- Msikiti Nur (Ijumaa moja) Malindi, Kenya
- Msikiti Shaykh Nassor. (Jumamosi baada ya Swala ya Magharibi)
Vitabu vyake
- Tafsiri ya Qurani Takatifu. Ilipigwa chapa mara ya mwanzo mwaka 1969
- Maisha ya Nabii Muhammad
- Mawaidha ya Dini
- Tarehe ya Imam Shafi na Wanazuoni wakubwa wa Afrika ya Mashariki
- Baadhi ya Wanachuoni wa Kishafi wa Mashariki ya Afrika.
- Sayyid Said bin Sultan
- Urathi
- Jawabu za Masuala ya dini (sehemu ya kwanza, pili na tatu)
- Tafsiri ya Suratul Kahf na hukumu ya swala ya Ijumaa
- Sura za swala na tafisir zake
- Swala na maamrisho yake
- Ndoa na maamrisho yake
- Saumu na maamrisho yake
- Mambo anayofanyiwa Maiti na Bidaa za Matanga na hukumu za Eda
- Bidaa I na II
- Khitilafu za Madhehebu Nne katika swala
- Sifa za Mtume, mawaidha na Dua
- Mashairi I-II
- Maisha ya Sayyidnal Hassan
- Maisha ya Sayyidnal Hussein
- Utukufu wa swala na namna ya kusali
- Mafunzo ya dini
- Tafsiri ya Maulidi Barzanji neno kwa neno
- Wakeze Mtume wakubwa na wanawe wengine
- Wakeze Mtume wadogo
- Tafsiri ya Baadhi ya Sura za Qurani: Yasin, Waqia na Mulk Sayyidna Khalid bin Al-Walid
- Vyakula alivokula Mtume
- Tunda la Quran
- Upotofu juu ya Tafsiri ya Makadiani
- Kisa cha Miraji
- Maisha Ya Mtume Muhammad
Vitabu vya Kiarabu
- Al-Busa’idiyyun hukkaam Zinjibar. Muscat: Ministry of National Heritage and Culture 1982.
Vitabu vyake visivyopigwa chapa
- Inayatullaahi al-adhym bi al Qurani al-Karim
- Irfaani al ihsaan bi tarjamati al qarii Hafs bin Sulaymaan
- Nuru al basira wal al basar fi taraajimi al quraa al arba’atashar
- Al khulafau al Amawiyin [28]
Viungo vya Nje
- Shaykh 'Abdullaah Swaalih Al-Farsy Katika IslamTanzania
Makala hii kuhusu mtu huyo bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Shaykh 'Abdullaah Swaalih Al-Farsy kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |